Kiungo
wa Simba, Mussa Mudde, akijaribu kupiga shuti mbele ya mchezaji wa
Tusker ya Kenya, katika mchezo wao wa kimataifa wa kirafiki uliopiga leo
katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo, Simba
walipigwa bao 3-0.
KOCHA Mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig, aliyetarajiwa
kuwapo uwanjani wakati kikosi hicho kilipomenyana na Tusker FC katika mchezo wa
kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ameshindwa kutokea uwanjani hapo
na kuwaacha midomo wazi mashabiki wa timu hiyo.
Awali katika taarifa yake, Simba ilidai kwamba Liewig
angetambulishwa rasmi kuinoa timu hiyo wakati wa mchezo huo, lakini kukosekana
kwake ni jambo lililowaacha njia panda mashabiki wa timu hiyo waliofurika
kwenye kumshuhudia kocha wao mpya.
Mechi hiyo ambayo ilitarajiwa na mashabiki wa timu hiyo
kwamba watashuhudia kikosi kamili kikishuka dimbani ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza mwezi ujao,
badala yake ni kikosi B cha timu hiyo ndicho kilichoanzishwa.
Tusker FC ambao siku kadha zilizopita waliinyuka Yanga bao
1-0, waliendeleza makali yao na kuzichapa timu za hapa nchini baada ya kuinyuka
Simba mabao 3-0 katika mchezo wa
kirafiki uliofanyika kwenye dimba la Taifa, Dar es Salaam jana.
Mabao mawili ya Jesse Were na moja la Fredrick Onyango
yalitosha kuitoa kimasomaso Tusker katika mchezo ambao mashabiki wa Simba
walishindwa kupata burudani kutoka kwa nyota wao wa kimataifa kutokana na
kutokuwapo katika mchezo huo.
Katika mchezo huo, Simba ilianza kumtumia tena kiungo wake
mshambuliaji, Haruna Moshi 'Boban', aliyeingia kipindi cha pili kujaribu kuweka
mambo sawa, lakini mambo yaliendelea kuwa magumu kwa kikosi hicho cha Wekundu
wa Msimbazi.
Boban alicheza mechi hiyo akitokea kwenye adhabu ya kufungiwa
mechi kadha za duru la kwanza la Ligi Kuu Bara kwa madai ya kwamba ni utovu wa
nidhamu.
Kama timu tumeona hilo sio tatizo na kwamba kocha wetu
mtu atatua hapa nchini Jumatatu. Kuhusu wachezaji wengi, Okwi (Emmanuel) na
kipa wetu Abel Dhaira na Sunzu (Felix) watatua hapa nchini kesho (leo).
Kuhusu wale wachezaji waliokuwa kwenye timu ya taifa,
Kapombe (Shomari), Ngassa (Mrisho) na wengineo watajiunga rasmi na timu
Jumatatu.
Katika mchezo wa jana, Simba ilijaribu kufanya mabadiliko
kadha ya kuwaingiza wachezaji wake, Boban, Edward Christopher, Nassor Chollo,
Emily Isyaka, Salum Kinje, Jonas Mkude na Ramadhan Singano, lakini hakukuwa na
mabadiliko yoyote na hivyo hadi mwisho wa mchezo, Simba ilikubali kipigo.
Simba: William Mwete, Haruna Shamte, Paul Ngalema, Hassan
Hatibu, Komain Keita, Mussa Mudde, Haroun Athuman, Abdallah Seseme, Abdallah
Juma, Ramadhan Chomo, Kiggy Makassy.
Tusker FC: Samwel Odhiambo, Luje Ochieng, Jeremiah Bright,
Mana Odhiambo, Joseph Shikokoti, Khalid Aucho, Edwin Ombasa, Fredrick Onyango,
Jesse Were, Robert Omonuk. Refa: Hashim Abdallah kutoka Dar es Salaam.
SOURCE:http://handenikwetu.blogspot.com
No comments:
Post a Comment