Na Mwandishi wetu,
Kampala
Kocha wa Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim
Poulsen amesema mechi ya kesho
(Jumamosi) dhidi ya Somalia katika michuano ya Cecafa Challenge yanayoendelea
Jijini Kampala, ni ya kufa na kupona na kikosi chake kiko tayari kukamilisha
kazi.
Kocha huyo aliyasema hayo wakati Stars, inayodhaminiwa na
Bia ya Kilimanajro Premium Lager, ikifanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo
wake na Somalia ili kukamilisha michezo ya Kundi B inayojumuisha Burundi,
Tanzania, Somalia na Sudan.
“Mechi hii ni sawa na kuwa na risasi moja na risasi hii
unatakiwa kuitumia vizuri..ndio mtihani tunaokabiliwa nao katika mechi hii
maana lazima tushinde ili tusinonge mbele katika mashindano haya,” alisema n
akikosi chake kitapambana hadi dakika ya mwisho.
Alisema ana imani na kikosi chake kwani wachezaji wote wana
ari ya ushindi na kuendelea na mashindano kwani wameshaonesha kiwango kikubwa
katika mechi mbili zilizopita huku Stars ikishinda mechi moja shidi ya Sudan na
kufungwa nyingine na Burundi.
“Katika mechi hii hakuna mchezo na nimeshawaambia wachezaji
kabisa maana hapa ukifungwa unaondoka,” alisema.
Kocha Poulsen pia alisema amefarajika kurejea kwa mchezaji Shomari
kapombe ambaye alijeruhiwa katika mechi dhidi ya Burundi juzi.
Kwa mujibu wa daktari wa timu, Dk Mwanandi Mwankemwa,
mchezaji Mwinyi Kazimoto hataweza kucheza kwa kuwa bado anaendelea kupata nafuu
kwa hivyo wamemshauri kocha ampumzishe katika mechi hii na baadaye Stars
ikifuzu kucheza mechi zijazo.
Meneja wa Bia ya Kilimanajro Premium Lager, George Kavishe
alisema mechi hii ni muhimu kwa Stars na kuwaomba watanzania wanaoishi Kampala
kujitokeza kwa wingi kuishangilia.
“Vijana hawa wanahitaji sapoti kutoka kwa wadau wote hasa katika mechi hii ya kesho itakayoamua
kama Tanzania itafuzuu kuendelea au la….sisi tukiwa wadhamini wa timu
tunafuatilia kwa karibu na tunawaomba Tanzania waishangilie na kuipa moyo timu
yao,” alisema.
Kikosi kinachotarajiwa kuanza katika mchezo huu dhidi ya
Somalia ni Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe, Kelvin
Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, John Bocco, Shaban Nditi na
Salum Abubakary.
Mchezaji Amir Maftah ameachwa maana ana kadi mbili za njano.
No comments:
Post a Comment