Watanzania sasa hivi wamekuwa wakitoa tuhuma na
lawama mbali mbali kwa TOC. Hii ni fadhaa inayotokana na kwamba kwa muda mrefu
sasa, Tanzanaia imekosa medali katika mashindano ya kimataifa. Kumekuwepo pia
na malalamiko dhidi ya TOC ya kuwa mbali na Serikali na pengine taasisi
nyengine nyingi katika kushaurikana na kuweka mikakakti ya pamoja ya kuratibu
harakati za kuleta ushindi nchini kwetu.
Kuna lawama pia za kukiuka katiba na miongozo ya IOC ambayo haina budi
kuangaliwa kwa makini.
Kwa ujumla, watanzania kwa kutumia sauti zao,
wanakosa raha wanayoiptarajia katika medani za michezo Tanzania. Hivyo basi,
kuna haja ya kuwa na Mabadiliko ndani ya TOC kwa kuingiza damu changa zenye
nguvu, weledi na uzoezu wa kimataifa ili kuandaa mazingira mazuri ya ushindi.
Sababu kuu za kuomba nafasi hii ya juu ndani ya
TOC (Rais) ni pamoja na kuwa na sifa, uwezo, uzalendo na hamu ya kuleta
mabadiliko katika tasnia ya michezo kwa kuptipa Kamati ya Olimpiki Tanzania.
Pia naamini kwamba kwa kuwa katiba bora na
inayofuatwa na watu wote, uwezo na utaalamu wa endeshaji na utawala wa taasisi
za kiraia nilio nao; timu nzuri ya wajumbe na viongozi wa TOC wenye sifa na
hamu ya kuendeleza michezo itapatika, kutakuwa na mwanzo wa mabadiliko ambayo
watanzania wanayatamani kwa muda mrefu.
Mabadiliko ndani ya TOC yanahitajika sasa kwa kuwa na mafiga matatu makuu makini na
mahiri na sikivu. Pia ikiwa kutakuwa na wajumbe imara wa Kamati Tendaji ili kwenda
na hali ya sasa ya sayansi na teknolojia na kukidhi kiu ya Watanzania,
mabadiliko yatakuwepo.
Mtazamo wangu ni kuleta Mabadiliko ya kimfumo
(systemic), kiutawana (managerial) na uendeshaji na Kimkakati (strategic) ndani
ta TOC mpya, yenye matumaini na itayoendeshwa kisayansi.
Katika kutekeleza mabadiliko hayo, TOC mpya
itaongozwa na maadili (misingi mikuu) ifuatayo:
Umoja miongoni mwa
viongzo wa TOC, watendaji na Umoja wa Vyama na wanamichezo. Hakutokuwa na
ubaguzi katika kutoa huduma za TOC.
Ukweli na Uwazi. Huu
ni msingi mkuu na viongozi wote watatakiwa kuusimamia ipasavyo. Majungu na
kuunda kambi hakutopewa fursa ndani ya TOC mpya.
Uwajibikaji: Kila mtu
atatakiwa kufanya kazi zake kwa weledi wa hali ya juu na kuhakikisha kuwa dhamira
na malengo ya TOC waliyowekwa yanafikiwa. Vikao vya Kamati vitatumika kuelezana
ukweli na kuwasaidia wale ambao hawaendani na kasi ya mabadiliko.
Umoja na Mshikamamo:
TOC itaongozwa na Utanzania Kwanza. Uzalendo na upendo wa nchi siku zote
utawekwa mbele. Ubinafsi na choyo hautokuwa nafasi katika kazi za kamati katika
miaka 4 ijayo.
Dira ya TOC katika miaka 4 ijayo ni kuiona “Tanzania
imerejesha imani kwa wananchi katika michezo ya Olimpiki kwa kuanzisha mfumo
bora wa kupata ushindi katika mashindano ya Kimataifa”.
Hili litafikiwa kwa kuandaa mipango itakayosaidia kuongeza
wigo wa ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania na hatimae kupata ushindi (medali)
katika mashindano ya Kimataifa na hivyo kurejesha heshima kwa nchi yetu.
Mafanikio haya yatakuja ikiwa kutakuwa na uongozi bora na makini na sikivu
wenye mtazamo wa mabadiliko chanya; ushirikiano mkubwa wa wadau hasa vyama,
viongozi wa jamii na wanahabari; maandalizi ya mapema ya wanamichezo; kuwa na
vifaa na miundombinu za michezo na utashi wa kisiasa.
Mabadiliko ambayo watanzania wayatarajie katika
miaka 4 ijayo ni pamoja na yale ya
kimfumo, kiutawala na uendeshaji na kimkakati.
Mabadiliko ya Kimfumo
yatahusisha zaidi marekebisho ya katiba ili iende na matakwa ya sasa. Kuna haja
ya Katiba kuweka mazingira ambayo haki inaweza kutendeka bila ya mizengwe na
pia kuondosha utata ambao unaweza kujitokeza kiuntendaji. Kanuni za uendeshaji
(Uchaguzi na za utawala wa fedha) zitaandaliwa na kusimamiwa na wahusika ili
kuweka uwanja sawa wa uendeshaji wa kazi za Kamati.
Mabadiliko mengine ni ya Kiutawala na Utendaji ndani ya TOC. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba
kila mtendaji anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa katiba na kanuni ya TOC bila ya
kuingilia majukumu ya mtu mwengine. Watendaji wa TOC nao watapimwa kwa matokeo
ya utendaji wao na wale ambao hawaendani na kasi ya mabadiliko watawajibishwa
kwa mujibu wa sheria za kazi na kanuni zake. Utendaji utapimwa kwa matokeo ya
kila mfanyakazi (Perfomance appraisal) kulingana na malengo tyake ya mwaka. Hatoonewa
mtu ila pia hatobebwa mtu. Motisha kwa wafanyakazi ikiwemo maslahi yao
yataangaliwa na kufanyiwa marekebisho kila inapostahiki. Vongozi wote wa TOC
wataomba sana kufanya kazi zo kwa mujibu wa Katiba na si vyenginevyo. Vikao vya
Kamati tendaji vitatumika kama mfumo rasmi ya kujadili utendaji wa TOC.
Katika mabadiliko ya kimkakati ndani ya miaka 4 ijayo, watanzania wategemee kuimarika
sana kwa uhusiano wa TOC na wadau wengine. Kwanza TOC itashirikiana kwa karibu na Serikali kuu na zile za Mitaa.
Mahusiano na mashauriano na Wizara zinayohusu michezo na hasa mabaraza la michezo
yataimarishwa yataimarishwa zaidi Tanzania bara na Zanzibar. Ofisi ya Waziri
Mkuu (TAMISEMI) nayo itakuwa mdau muhimu sana wa TOC ili kuona michezo
inafanyika maeneo yote ya Tanzania, ikiwemo mijini na vijijini na fursa
zinapatika kwa wanachi wote bila ya ubaguzi hasa kwa kupitia Makatibu wa Serikali
wa Mikoa (RAS). Uhusiano wa karibu na Wizara za kisekta (elimu, afya,
miundombinu, ulinzi na usalama, mawasiliano nk) utazingatiwa na kuimarishwa zaidi.
TOC mpya pia itaimarisha mahusiano kati ya wadau wa mandeleo, wafadhili na makampuni binafisi
yaliyopo nchini na nje ya nchi. TOC mpya itajipanga kutafuta na wadhamini
(sponsors) kutoka kwa mashirika na makampuni makubwa duniani ili kupata nyenzo
za kuendeleza michezo. Wananchi wataombwa kutoa maoni yaokuhusu hili juu ya
namna bora ya ushirikiano huo.
Uhusiano wa Kamati za Olimpiki za nchi za jiarani na mabara mengine
utaimarishwa ili kujifunza na kubadilishana mawazo juu ya uendeshaji bora wa
Kazi za Olimpiki. Mafunzo kwa wajumbe wa TOC ili kwenda sambamba na mabadiliko yatatolewa.
Katiba ya TOC inatoa uwezo wa kuunda kamati mbali mbali. Katika miaka 4 ijayo, kamati hizi
zitatakiwa kufanya kazi na kutoa taarifa zake kwa TOC. Kwa kadri hali na uwezo
utakavyoongezeka, kamati hizi zitawezeshwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Watanzania pia watarajie kuwaona watu maarufu katika masuala ya michezo
wakiombwa kutoa ushauri wao na namna ya keundeleza Michezo. Mikutano maalum
na wadau (wananchi, wanasiasa, wasomi, wanamichezo, waandishi wa habari,
wanahadhiri, wachambuzi wa mambo ya kijamii na kiuchumu nk) itaandaliwa ili
kupata mawazo zaidi ya uendelezaji wa michezo Tanzania hasa katika siku za
kuadhimisha sherehe za olimpoki za kila mwaka. Afisa wa Uhusiano atatakiwa
kuhakikisha TOC iko karibu sana na Watanzania. Matumizi ya Mitandao (blog na
tovuti na simu) itatumika kuelimisha na kupata maoni ya wadau. Tunataka TOC yenye kazi ya 3G (3rd Generation).
Mabadiliko mengine ni ya kuwa na Mipango inayoonyesha malengo mahsusi na
yanayotekelezeka. Hii ni pamoja na kuwa Uratibu mzuri wa kazi za TOC, Mafunzo
kwa wanamichezo na viongozi, miundo mbinu (Kuwa na eneo la kujenga Kijiji cha
Olimiki Tanzania bara na kuendeleza kijiji cha Olimpiki kilichopo Zanzibar) na
kadhalika. TOC mpya itaanza kufikiria uwekezaji wa muda mferu wa miundombinu ya
Michezo Tanzania.
Vyama Taifa watarajie mahusiano
bora zaini na TOC mpya.
Makamo wa Rais atatakiwa kuhakikisha mashauriano baina ya TOC na Vyama
yanaimarika kila uchao. Hii itajumuisha kuwa na Kalenda za Michezo
zinazoonyesha mashindano mbali mbali. TOC inaweza kuvisaidia vyama kupata vyenzo
au utaalamu ili kuona kwamba vipaji vinaibuliwa na kunakuwa na ongezeko la
wanaridha na wanamichezo Tanzania wanaoshiriki katika mashindano ya Kimataifa.
TOC kwa kushirikiana na vyama watahakikisha viwango vinavyotakiwa kimataifa
vinapatikana na washiriki wanaostahiki pekee ndio wanakwenda katika mashidano
husika.
Watanzania pia watarajie uhusiano bora zaidi wa TOC na vyombo
vya habari na wananchi. Maoni, taarifa na mambo yahayohusu michezo
yatatolewa kwa waandishi ili nao wawajulishe watanzania. Midahalo ya namna bora
ya kuendeleza miechezo ikiwemo ya kuibua vipaji itaandaliwa na TOC kwa
mushirikiana na vyombo vya habari. Siku za maadhimisho ya Olimpiki zitatumika
kuwa karibu sana na wadau ili kuopata mawazo na maoni yao.
TOC mpya inapanga kutaleta mabadiliko ya kuchechemua hamasa ya michezo katika
mawizara, taasisi za umma na binafsi, vyuo vikuu, shule na kwa jamii ili
kutekeleza nia ya Michezo kwa wote itakayowajumuisha watu wenye ulemavu.
Lengo moja la TOC ni kuendeleza amani, TOC mpya itashirikiana na Serikali,
asasi za kiraia na wadau wengine ili kuhakikisha amani ya Tanzania inaimarika.
Michezo na mashindano mbali mbali yatahamasishwa kushajiisha umoja, upendo na
mshikamamo miongoni mwa wananchi.
Maadili katika michezo nayo yatasimamiwa na TOC.
Wanamichezo watakaotumia madawa na kubainika hawatopata fursa na kushiriki
mashindano. Uwekezaji katika kituo cha kupima matumizi ya madawa utatafutwa ili
kuifanya Tanzania kuwapima wachezaji. Afya za wachezaji na ziongozi pia
zitatetewa. Dhana ya kuwa na Bima kwa wachezaji itapelekewa kwa vyama vyote. TOC inaweza kuwaunganisha vyama na
Makampuni ya Bima ili kupata punguzo maalum kwa wachezaji na viongozi wa
michezo.
Utekelezaji wa Mabadiliko haya kwa kiaisi kukubwa
sana utategemea umoja, upendo, umakini na ushirikiano wa washika dau mbali
mbali. Watananzania na wapiga kura wanaombwa
kuiunga mkono timu ya Mabadiliko ili katika miaka 4 ijayo kuwe na matumani na
ushinidi kwenye mashindano ya Kimataifa na kuiletea heshima nchi yetu.
Inawezeka, haitokuwa ajabu kama kukiwa na nia ya dhati na viogozi bora na
makini, Tanzania itaona mabadilko.
Mungu Ibariki
Afrika, Mungu ibariki Tanzania,
Khamis Said
Mgombea wa
Urais, TOC
Imetolewa leo
04/12/2012 ( kwa matumizi ya Umma)
Wasifu: Khamis Said ni Makamo
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo (BTMZ)
Zanzibar. Pia ni muanzilishi na kiongozi wa chama cha wafanya mazoezi
Zanzibar. Pia ni kiongozi wa juu kabisa
katika chama cha wanfanya mazoezi ya viungo Zanzibar. Awali, amekuwa mchezaji
wa soka, table tennis na Volleball. Alipata pia mafunzo wa kuogelea wakati
akisoma Chuo cha Bahari na Uvuvi Zanzibar.
Ana uzoefu wa uongozi wa zaidi ya miaka 22. Amefaya kazi
Serikalini kwa miaka 7 badae kwa miaka 16 sasa anafanya kazi katika Shirika la
Maendelo la Kimataifa. Ameshahudhuria mikutano ya Kitaifa na Kimataifa ndani na
nje ya nchi.
Amekuwa Katibu wa Kamati inayoratibu mashindano ya
Mapinduzi maarufu Mapinduzi Cup kuanzia
2011 mpaka sasa na kuwa na mafanikio makubwa katika mashindano yaliyopita
amabayo yalijumisha tumu za Zanzibar, Tanzania bara na nchi za jirani. Ametoa
muongozo kwa vyama Taifa Zanzibar na mafunzo ya ndani ya uendeshaji.
Mwaka 2012, ameweza kuandika mapendekezo ya Miradi kwa
ajili ya Zanzibar inaratijia kupata msaada mkubwa wa vifaa vya michezo wenye thamani ya Tshs 0.6
billion. Pia ameandika miradi mengine ya kuendeleza viwanja vya michezo
Zanzibar yenye thamani ya Tshs 750 milioni. Juhudi za kutafuta wafadhili zinaendelea.
Hivi sasa ameanzisha mawasiliano na mashirika ya
kimataifa ya kuendeleza michezo na kuna dalili za kupata makocha wa kimataifa
wa kufundisha soka Zanzibar kwa miaka mitatu ili kuwanoa watoto na vijana
katika mashule na vijijini. Msaada huu unaweza kuja Tanzania Bara pia.
Elimu: Mtaalamu wa Sayasi ya
Jamii (Social Scientist). Amepata shahada
ya kwanza ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma alioipata chuo Kikuu Huria cha
Tanzania. Pia ana shahada ya Pili (Masters) ya Elimu, Afya na Maendeleo ya
Kimataifa aliyoipata Chuo Kikuu cha London, nchini Uingereza. Ni mzoefu sana wa
Komputa na anajua programu zote za Microsoft Office.
Tabia: Msikivu, mweli,
muaminifu na anaechukia dhuluma na rushwa. Anapenda haki na kufanyakazi kwa
pamoja. Anakubali kukosolewa na ni mwepesi wa kujifunza haraka sana na
kubadilika kutokana na mazingira.
Familia: Ana
mke na watoto watatu
Mabadiliko ni lazima TOC, watanzania wasifanye makosa, watakuja kujuta, all the best. TAKUKURU kuwei makini sana
ReplyDelete