Na Fadhili Athumani, Moshi
23, Desemba
BINGWA mtetezi wa Ligi daraja la Tatu ya Mkoa wa Kilimanjaro, Timu ya Soweto FC kutoka Moshi mjini, imeanza vibaya kampeni ya kutetea ubingwa wake kwa kukubali kipigo cha mbwa mwizi kutoka kwa Newgeneration FC nayo ya Mjini hapa ya goli 4-2.
Mabingwa hao, walijikuta wakiruhusu goli la mapema, katika dakika ya 22 tu, kipindi cha kwanza, baada ya mabeki walionekana kumsahau Mchezaji hatari wa Newgeneration FC, Peter Julius, aliyeunganisha krosi ya Chikoma Jafari na kuiandikia timu goli la kuongoza.
Mara baada ya goli hilo wachezaji wa Newgeneration waliamka huku wakitandaza soka safi na kuishambulia lango la Soweto, mashambulizi yaliyozaa matunda katika dakika ya 38 kipindi cha kwanza, kwa goli la Chikoma Julius ambaye alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Soweto FC.
Ikiwa imesalia dakika moja tu kipindi cha kwa kimalizike, Chikoma Julius ambaye anatarajia kufanya majaribio na tinu ya Azam FC ya Dar es salaam, mapema Januari mmwakani alirudi tena kumsalimia mlinda mlango wa Soweto FC, Bruno John na kufanikiwa kufanya timu yake iende mapumziko ikiongoza kwa goli 3-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Soweto wakionesha uhai na kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambapo katika dakika ya 52, walifankiwa kupata goli la kwaza kupitia kwa Brian Shilela, aliyepiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwamoja wavuni na kufanya matokeo yasomeke 3-1.
Magoli mengine yalifungwa na Chikoma Julius, aliyeondoka na mpira kwa kufunga magoli matatu kwa mguu wake, “Hat-trik” huku goli la pili la Soweto likifungwa na Mrisho Mindu na hadi mwamuzi wa mchezo, Thomas Mkombozi anapuliza kipenga matokeo yalikuwa ni 4-2.
Matokeo ya michezo mingine iliyochezwa Jumamosi ambayo ilikuwa ni siku ya Uzinduzi wa ligi daraja la Tatu mkoani hapa kwa msimu wa mwaka 2012/2013, ukiacha mchezo huu, uliochezwa katika kituo cha Moshi, kwenye uwanja wa Mimoria Jamhuri, Machava FC ya Moshi mjini ilioibamiza Kurugenzi FC ya Same, 4-1 katika kituo cha Holili.
Katika kituo cha Himo, Kilototoni ikiwakaribisha Kilimanjaro FC, ilijikuta iking’ang’niwa shati na vijana hao wa mjini, kwa kufungana goli 1-1. Ligi hiyo itaendelea leo (Jumapili) kwa michezo mitatu katika vituo vya Hino, Moshi na Holili ambapo katika kituo cha Moshi kwenye uwanja wa Jamhuri Mimoria, Forest FC iliumana na Kia Junction.
Kituo cha Holili, kitashuhudia Tarakea FC ikiumana na Mwanga FC, wakati huo huo Vijana FC ikushuka dimbani kutafuta heshima kutoka kwa Kralle FC.
No comments:
Post a Comment