Search This Blog

Tuesday, November 27, 2012

YANGA IMEPANGA KUMUUZA NIYONZIMA.



KLABU ya soka ya Yanga imepanga kumuuza kiungo wake, Haruna Niyonzima kwa dau la dola 150,000 za kimarekani ambazo ni zaidi ya Sh. 225 milioni kwenda El-Merreikh ya Sudan iliyoomba kumnunua.

Jumamosi wiki iliyopita, El-Merreikh iliiandikia Yanga ikionyesha nia yake ya kutaka kumnunua Niyonzima na kuomba iambiwe thamani ya mchezaji huyo ili iweze kumsajili haraka iwezekanavyo.

Mtandao huu una uhakika El-Merreikh ambayo makao makuu yake yapo mjini Khartoum, imepanga kwa gharama yoyote kuhakikisha inamsajili kiungo huyo ili aweze kuisaidia katika nafasi ya kiungo.

“Klabu yetu ina fedha za kutosha, tunachotaka ni kumsajili Niyonzima ili kuimarisha safu ya kiungo kwa sasa kwani tunadhani yeye ni miongoni mwa viungo wa Afrika Mashariki na Kati kwa wakati huu,” kilisema chanzo chetu makini cha habari kutoka El-Merreikh.

Katika barua pepe ya maombi ya kumsajili Niyonzima kutoka El-Merreikh, klabu hiyo imesisitiza kujibiwa haraka kuhusu dau la mchezaji ili mchakato wa usajili ufanyike haraka pindi makubaliano yakifikiwa. Dirisha dogo la usajili Tanzania Bara limeanza 15 Novemba hadi 15 Desemba mwaka huu.

Uongozi wa Yanga uliketi wikiendi hii na kukubaliana kumuuza Niyonzima kwa dau la dola 150,000 kwa El-Merreikh lakini ikisisitiza kuwepo kwa mazungumzo kati ya klabu hizo kwani kiungo huyo amebakisha si zaidi ya miezi sita kumaliza mkataba wake wa miaka miwili na Yanga.

“Tulipokea maombi ya El-Merreikh wikiendi iliyopita na ndani ya muda mfupi tulikaa na kujadili kisha tukapata jibu la kumuuza Niyonzima kwa dola 150,000 lakini tunaweza kuzungumza zaidi na timu hiyo.

“Lengo letu ni kumuona mchezaji ananufaika na uwezo wake wa uwanjani na siyo kumzibia njia ya kutoka hasa inapopatikana nafasi ya kufanya hivyo. Tumeshawajibu El-Merreikh na sasa tunasikiliza watasemaje,” alisema kiongozi mmoja wa Yanga aliye ndani ya kamati ya usajili ambaye hakutaka jina lake litajwe.



Hata hivyo viongozi wa El-Merreikh kutoka Sudan, wamesema bado hawajapata majibu ya Yanga, na walipoambiwa klabu hiyo inahitaji dola 150,000 ili imuachie Niyonzima, mmoja wa viongozi hao alisema; “Mbona nyingi mno?”



Kiongozi huyo alisema kiasi hicho ni kikubwa kulinganisha na thamani ya mchezaji uwanjani na umri wake, pia muda uliobaki katika mkataba wake.



“Hata hivyo, majibu ya Yanga yakitufikia tutajadiliana na kuamua nini cha kufanya japokuwa Niyonzima ni mchezaji mzuri kweli,” alisema kiongozi huyo.



Niyonzima ambaye Yanga ipo katika mchakato huo wa kumuuza, kwa sasa yupo Rwanda akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kinachojiandaa na michuano ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Chalenji itakayoanza wikiendi hii huko Kampala, Uganda.



Kiungo huyo alipomtafutwa kwa njia ya simu, hakuweza kupatikana kuzungumzia maombi hayo ya El-Merreikh.

SOURCE: GAZETI LA MSETO

No comments:

Post a Comment