Search This Blog

Saturday, November 17, 2012

Wash United kuungana na Taifa Stars kuweka mazingira na Usafi ‘salama’



Mpira wa miguu unaweza kufanya nini kuhusu mazingira na usafi?
Zaidi ya watu bilioni 2.6 duniani wanaishi bila ya kuwa na vyoo. Barani Afrika, magonjwa ya kuhara yanayosabishwa na ukosefu wa vyoo na usafi ni hatari zaidi na ndio yanayosababisha vifo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, hii ni zaidi ya magonjwa kama Ukimwi, Malaria na surua ikifuatia. Takwimu kutoka mashirika ya UNICEF na WHO zinaonyesha kuwa nchini Tanzania zaidi ya asilimia 90 ya watanzania wanaishi katika mazingira machafu, na asilimia 12 hawana vyoo wala maji. Matokeo yake zaidi ya watoto 24,000 nchini Tanzania hufariki dunia kila mwaka. Tabia ya kunawa mikono kwa kutumia sabuni ni njia rahisi na haina gharama kubwa katika kuzuia magonjwa ya kuhara ambayo haitumiki sana hapa nchini hasa kwa watoto. Tatizo kubwa ni kwamba usafi wa mazingira na afya haupewi kipaumbele katika mawazo ya watu wengi katika vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wash United inafanya kazi kuweka sawa mambo ya mazingira na usafi katika ngazi zote mahala popote na kuhamasisha watu kunawa mikono kwa sabuni kila mara. Wash United ni mpango mpya wa kwanza kutumia nguvu ya mpira wa miguu na mastaa wake katika kuhamasisha unywaji wa maji safi, mazingira safi na usafi kwa wote barani Afrika na duniani kote. Katika kukamilisha mpango wake huu Wash United imeungana na wadau mbalimbali duniani, kwa hapa Tanzania shughuli zinaendeshwa kwa msaada wa shirika la maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF)
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania limekubali kushirikiana na mpango wa Wash United katika kuhamasusha tabia ya kutunza mazingira na usafi kwenye timu za vijana kupitia mradi timu za vijana wa shirikisho hilo. Katibu mkuu wa TFF Ndugu Angetile Osiah, leo amesaini mkataba wa makubaliano kati ya TFF na Wash United. “Ushirikiano kati ya Taasisi ya Wash United na Shirikisho la mpira wa Miguu ni mpya na wa kujitolea katika sekta ya mpira wa miguu Tanzania. Akiongea kuhusu Wash United, mratibu wa Wash United nchini Tanzania Ndugu Femin Mabachi alisema “Kupitia mpira wa miguu na kwa kushirikiana na TFF, tunaweza kutunza mazingira na usafi ‘salama’ na kuongeza uwiano katika kushughulikia mambo haya katika jamii yetu.
Taifa Stars Kuongoza mpango wa Wash United
Kwa kuungana na Wash United, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakuwa limejiunga na zaidi ya mastaa 100 wa mpira wa miguu kama Didier Drogba, Michael Ballack, Arjen Robben, Bayern Munich, Taasisi za Real Madrid na ile ya Barcelona na pia zaidi ya wananchama 30,000 wa Wash United duniani kote. Nahodha wa Taifa Stars Juma Kaseja atawaongoza wachezaji wenzake kuwa washiriki kwenye mpango huu wa Wash United na kushiriki katika kampeni nchini Tanzania na duniani kote. Zaidi ya yote wachezaji wa timu ya Taifa watashiriki katika shughuli za mchezo wa mpira wa miguu mashuleni zitakazofanyika hapa nchini zitazokuwa zikiendeshwa na taasisi hizi.

No comments:

Post a Comment