Mjumbe Mwarami Kobe Ally ( kushoto ),mwenyekiti,Juma Simba (kati ) na Katibu wa kamati bwana Peter Hella (kulia ) .
Mgombea asiyeudhuria usaili apitishwa kugombea
WAKATI majina ya wagombea katika uchaguzi mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) yakiwekwa hadharani, majina ya wagombea Said Tully,Ally Mayay na Philemon Ntahilaja yamekatwa huku Isaac Mazwile akipitishwa bila hata ya kuwepo katika usaili.
Awali Tully ambaye ni wakala anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) aliwekewa pingamizi la kutokuwahi kufanya kazi katika klabu ya Ashanti United ya Ilala na hata alipowasilisha barua ya kuchaguliwa katika moja ya kamati za timu hizo, alitupwa nje.
Mbali ya Mazwile kupitishwa kuwania nafasi ya mwakilishi wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na makamu mwenyekiti, mtu mwingine aliyepitishwa ni Muhsin Balbhou anayewania nafasi ya mwakilishi wa mkutano mkuu huku akiwa amewekewa pingamizi.
Uteuzi wa Mwarami Ally Kobe kwa mara ya pili katika kamati ya uchaguzi
Kwa mujibu wa mmoja wa wagombea wa nafasi ya uwakilishi wa mkutano mkuu, Shaffih Dauda, mjumbe wa kamati hiyo Ally Kobe, hakustahili kuchaguliwa tena kuwamo ndani ya kamati hiyo kwani alishiriki madudu ya awali yaliyoifanya kamati iliyokuwa chini ya Mwenyekiti, Muhidin Ndolanga kuvunjwa na TFF.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deo Lyato alivunja kamati ya uchaguzi ya DRFA iliyokuwa chini ya Ndolanga kutokana kukiuka kanuni mbalimbali za uchaguzi huku kubwa likiwa kutia kasoro fomu za wagombea kadhaa.
Kobe anadaiwa kuhusika kwa kiasi kikubwa katika madudu hayo, lakini Mwenyekiti wa DRFA anayemaliza muda wake, Said Bakhressa ambaye ameenguliwa na kamati ya Lyato kutetea nafasi yake, alihakikisha Kobe anabaki katika kamati ili tu kuhakikisha mtandao wake wa viongozi unapitishwa kuwania uongozi DRFA.
Hivyo, Kobe aliachwa ili kuwalinda baadhi ya wagombea wanaodaiwa kuwa ama wafuasi au kupandikizwa na Bakhressa katika mchakato wa usaili hata mapingamizi wanayowekewa.
Ili haki itendeke, ilitakiwa Kobe asiwepo tena katika kamati mpya ili kufanya mambo yaendelee katika mstari mnyoofu kwani lengo la Lyato lilikuwa kuhakikisha haki inapatikana katika mchakato wa uchaguzi huo. Hii ina maana si Ndolanga peke yake aliyekuwa na matatizo katika kamati hiyo.
Inaweza hata mambo yaliyotokea wakati mwenyekiti akiwa Ndolanga, yalisababishwa na wajumbe kama kina Kobe. Kwa hali hii, hakuna jipya lililofanywa na Lyato, kwani madudu yameendelea.
Miongoni mwa mambo yaliyofanywa na kamati ya sasa ya uchaguzi ya DRFA iliyo chini ya Mwenyekiti, Juma Simba ‘Gaddafi’ ni kupitisha majina ya Mazwile na Balhabou huku wakiwa wamewekewa mapingamizi na wagombea wenzao.
Gaddafi kutokuwepo katika kamati kwaruhusu madudu
Katika kikao cha kupitia mapingamizi yaliyowekwa kwa baadhi ya wagombea wa uchaguzi wa DRFA, mwenyekiti, Juma Simba hakuwepo kutokana na udhuru aliotoa ili kuhudhuria mambo ya siasa katika Chama cha Mapinduzi (CCM) ambako ana majukumu.
Kwa kutumia mwanya huo, wajumbe Said Rubeya na Kobe walitumia kila njia kuhakikisha wanawabeba baadhi ya wagombea ambao ndani yake wapo Mazwile na Balhabou.
Hata katibu wa kamati, Peter Hella alizidiwa nguvu na Rubeya na Kobe katika kuhakikisha haki inapatikana jambo lililomfanya achukue uamuzi wa kujiuzulu kwa kutokubaliana na kilichokuwa kikifanywa na wajumbe hao.
Kuona hivyo, mwenyekiti Gaddafi alipopewa taarifa hizo na Hella, alimsihi katibu huyo asijiuzulu kwa ahadi ya kuzidi kuuchafua uchaguzi huo. Hella bado yupo mguu ndani mguu nje kuhusu nafasi yake kwenye kamati hiyo.
Pingamizi la Mazwile lilivyozimwa.
Mgombea Mazwile aliwekewa pingamizi na Shaffih Dauda linalohusu kitendo chake cha kutokuwa mwadilifu katika kazi zake akiwa mtendaji wa Chama cha Soka Kinondoni (KIFA) kwa kumruhusu mtu asiye kiongozi kusaini kazi za chama hicho.
Inadaiwa kuwa, Mazwile akiwa mtendaji wa KIFA alitakiwa kusaini fomu za wagombea mbalimbali waliokuwa wakitakiwa kuhalalishwa kugombea katika vyama mbalimbali vya soka ikiwemo DRFA ili kuthibitishwa uhalali wao.
Akijua ni kinyume na taratibu, Mazwile akiwa safarini mkoani Dodoma aliruhusu mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Seif Ally Mailo 'Saddam' alisaini fomu na karatasi nyingine zilizopita KIFA kwa niaba yake, ikimbukwe Saddam hana madaraka yoyote KIFA.
Katika pingamizi hilo, vithibitisho vilitolewa ikiwemo karatasi zilizosainiwa na Saddam kwa niaba ya Mazwile lakini kamati ya uchaguzi kupitia wajumbe wakina Rubeya na Kobe, walitupilia mbali pingamizi hilo. Hata katibu ambaye ni Hella alipowataka wajumbe wenzake kutazama kwa mara ya pili pingamizi hilo, alipingwa vikali. Hatimaye, pingamizi la Mazwile lilitupwa mbali.
Pingamizi la Balhabou nalo utata mtupu
Katika pingamizi lake kwa Balbhou, Shaffih Dauda alikuwa alipinga mgombea huyo kuwa na elimu ya kidato cha nne inayotakiwa kwa kila mgombea wa uongozi wa DRFA kwa sasa.
Kamati ilitoa jibu la kuhakika vyeti vya Balbhou lakini ikimruhusu kuendelea na mchakato wa uchaguzi jabo ambalo ni kinyume na taratibu za uchaguzi huo. Hivyo pingamizi hilo nalo lilitupwa na kamati huku nguvu kubwa ikitoka kwa Rubeya na Kobe.
Kwa kawaida taasisi inayotakiwa kuthibitisha elimu ya kidato cha nne nchini ni Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na mchakato huo unaweza kuchukua siku saba hadi 14 tu.
Mazwile hakuhudhuria usaili lakini kamati yampitisha
Madudu mengine yaliyofanywa na kamati ya uchaguzi ya DRFA ni kupitisha jina la Mazwile kuwania nafasi ya uwakilishi wa mkutano mkuu na makamu mwenyekiti bila ya kuhudhuria usaili wa wagombea wote uliofanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Uhuru.
Mmoja wa wagombea wa uchaguzi wa DRFA, Shaffih Dauda alikuwepo ukumbini tangu mwanzo hadi mwisho na hakumuona Mazwile kuhudhuria usaili huo, lakini jambo la ajabu jina la mgombea huyo limeorodheshwa katika majina ya wagombea waliopitishwa kuwania uongozi DRFA.
Hayo ni baadhi tu madudu yaliyofanywa na kamati ya uchaguzi ya DRFA ambayo inasimamia uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
ENDELEA KUWA NASI UPATE MADUDU MENGINE YA UCHAGUZI HUO
No comments:
Post a Comment