Bwana Leodger Chilla
Tenga
Rais wa TFF
Ndugu Tenga,
YAH: UKIUKWAJI WA KATIBA YA TFF
Sisi
wadau wa mpira wa miguu Tanzania tunakuandikia barua hii tukiwa na uchungu
mkubwa kuhusu mwenendo wa uongozi wako.
Ulipoingia madarakani kwa mara ya kwanza Golden Tulip tarehe 27 Desemba
2004 ulitoa matumaini makubwa kuhusu kuleta mabadiliko makubwa katika
uendeshaji wa mpira wetu. Pamoja na
mapungufu mengi yaliyojitokeza ndani ya miaka minane ya uongozi wako haya mawili
tutakayoyaeleza hapa chini hayawezi kufumbiwa macho na wanaoutakia mema mpira
wa Tanzania.
1. Kupitisha muda wa uongozi wako bila
kibali cha mkutano mkuu.
Mkutano
mkuu uliokuingiza madarakani ulifanyika siku ya Jumapili tarehe 14 Desemba
2008. Kifungu 33(1) cha Katiba ya TFF
kinatamka kuwa kipindi cha uongozi ni miaka minne tu. Hivyo ukomo wa uongozi wako na kamati yako ya
utendaji ni saa sita za usiku tarehe 13 Desemba 2012. Aidha kifungu cha 10(1) cha kanuni za
uchaguzi wa TFF kinatamka kuwa tangazo la uchaguzi litatolewa siku 40 kabla ya
uchaguzi. Kwa mantiki hii kamati yako ya
uchaguzi ilitakiwa itangaze tarehe ya uchaguzi siku ya Jumatatu tarehe 05
Novemba 2012 au kabla ya hapo. Leo ni
tarehe 13 Novemba 2012 na ofisi yako iko kimya!
Hii haikubaliki, haiwezekani ujiongezee muda wa uongozi bila kibali cha
Mkutano Mkuu. Tutawaomba wajumbe wa
Mkutano Mkuu wakuadhibu kwa kosa hili la ukiukwaji wa Katiba. Pamoja na mapungufu haya ni vyema
ukatufahamisha uchaguzi umepanga ufanyike lini au unasubiri wajumbe wa mkutano
mkuu wakulazimishe kwa maandishi?
2. Kufuta nafasi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa TFF
Yapo
maneno yanasemwa eti uongozi wako unataka kufuta nafasi ya pili ya Makamu wa
Rais wa TFF kinyemela. Kama tuhuma hizi
ni za kweli tunaoma tukukumbushe yafuatayo:
2.1.1
Nafasi
ya makamu wa pili wa Rais wa TFF iko ndani ya Katiba ya TFF kifungu 31(1)
2.1.2
Kifungu
cha katiba 30(1) kinatamka wazi kuwa ni mkutano mkuu pekee wenye mamlaka ya
kubadili Katiba ya TFF. Hivyo hakuna
njia mbadala ya kubadili Katiba ya TFF.
2.1.3
Kifungu
cha Katiba 30(2) kinatamka kuwa tangazo lolote la nia ya kubadili Katiba ya TFF
litatolewa siku 45 kabla ya mkutano mkuu.
Uongozi wako utawezaje kutoa tangazo hili ndani ya kipindi cha uongozi
wako kilichobakia?
2.1.4
Kifungu
cha Katiba 30(6) kinatamka kuwa ombi la kubadili katiba litapigiwa kura NDANI
YA MKUTANO MKUU na ili lipite theluthi mbili ya wajumbe sharti iridhie. Zingatia utashi huu wa Katiba.
Bwana Tenga kama kweli wazo hili lipo
basi achana nalo, usijidhalilishe kwa kukiuka Katiba iliyokuweka madarakani. Nafasi za uongozi katika uchaguzi ujao
zitangazwe kwa mujibu wa Katiba iliyokuweka madarakani. Kama kuna umuhimu wa kubadili Katia hakuna
uharaka wowote, subiri awamu ijayo ifanyie kazi wazo hilo, awamu ambayo huenda
wewe mwenyewe ukaingoza pia kama ukigombea tena.
Tunasubiri majibu ya hoja zetu za
majibu haya tunaomba uwajulishe watanzania wote.
Nakala ya barua hii tunawapelekea
wajumbe wote wa Mkutano Mkuu kwa taarifa.
Ni sisi kwa niaba ya wadau wa mpira
wa Tanzania.
Hakuna material hapa, hoja dhaifu kabisa hizi! na aliyeandika kwa kujipachika "jina la wadau wa soka" hebu na aende akafanye utafiti vizuri kisha aje na hoja za uhakika na siyo za kuhisi hisi. na una uhakika gani kwamba tangazo la kubadili katiba halijatolewa kwa mujibu wa taratibu za kisheria? au unasubiri litangazwe redioni clouds?
ReplyDelete