UONGOZI wa Simba
SC unapenda kuzungumza yafuatayo
kuhusiana na matukio ya karibuni kuhusiana na klabu ya Simba.
- Uongozi umesononeshwa na matokeo ya siku za karibuni ya timu ya Simba hususani yale ya kufungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar ya Morogoro. Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Utendaji ya Simba imeliagiza benchi la ufundi la Simba kutoa ripoti kuhusiana na mwenendo wa timu katika mechi za karibuni.
Ikumbukwe kwamba Simba ilianza
ligi kwa vishindo na hadi kufikia mechi ya 12, ilikuwa ikiongoza ligi na
ilikuwa timu pekee ambayo haikuwa imepoteza mechi.
Mara baada ya ripoti ya benchi la
ufundi kukamilika, Kamati ya Utendaji ya Simba itakutana na kutoa maamuzi
kuhusiana na yaliyomo kwenye ripoti. Kutokana na hali hiyo, uongozi unaomba
wapenzi na wanachama wake kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo uongozi na
benchi la ufundi linatafuta suluhisho la kudumu kuwezesha timu kuendelea
kushinda.
Hata hivyo, uongozi wa Simba
unasisitiza kwamba hakuna kiongozi yeyote wa Simba –kuanzia wa juu zaidi hadi
wa chini zaidi, ambaye amejiuzulu au kuachia ngazi ndani ya klabu.
Ifahamike kwamba uongozi huu
ulipewa dhamana na wanachama miaka minne iliyopita ya kuiongoza klabu kisasa na
kuipa maendeleo endelevu kwa kipindi hicho.
Chini ya uongozi huu, Simba
ilikuwa mshindi wa pili misimu miwili iliyopita (ikiwa pointi sawa na mabingwa
ila ikizidiwa kwa pointi, ilikuwa mabingwa msimu uliopita, iliingia hatua ya 16
bora michuano ya CAF, imesajili wachezaji msimu huu kwa fedha zake yenyewe
(miradi mbalimbali) na inaendesha timu tatu za vijana.
Bado kuna kazi za kufanya na
uongozi unatambua hilo.
Ndiyo maana uongozi hauamini kwamba maneno mabaya yanayosambazwa dhidi ya
viongozi yanatoka kwa wanachama wake. Kazi nzuri ya uongozi huu inaonekana na
iko dhahiri.
Uongozi wa Simba unaomba wapenzi
na wanachama wake kuwa wamoja katika kipindi hiki ili kuwezesha ushindi
kupatikana dhidi ya Toto African ya Mwanza Jumamosi ijayo.
2. Kuhusu mchezaji Juma Kaseja
Uongozi umesikitishwa na vitendo ambavyo baadhi ya washabiki
walivifanya dhidi ya nahodha wa Simba, Juma Kaseja. Washabiki hao walimtukana,
kumkashifu, kumdhihaki na kumtishia maisha mchezaji huyo mara baada ya mechi
dhidi ya Mtibwa.
Kaseja ni miongoni mwa wachezaji wanaoheshimika sana ndani na nje ya
nchi. Vitendo vya kumkashifu si vya kiungwana na uanamichezo. Nahodha huyu
ameitumikia Simba kwa moyo mmoja na ni mmoja wa wachezaji wenye kuheshimika sana miongoni mwa
wachezaji.
Hatua ya kumtukana inaharibu heshima ya klabu. Ni mchezaji
mgani mzuri atataka kujiunga na Simba iwapo ataona Kaseja anafanyiwa hivyo?
Benchi la ufundi la Simba ni makini na iwapo kutakuwa na tatizo lolote la
kiuchezaji, litafanya mabadiliko.
Kama Kaseja angekuwa anapendelewa Simba, asingechaguliwa
kuwa kipa namba moja wa Taifa Stars na nahodha pia.
Tunachukua fursa hii kutangaza kwamba uongozi wa Simba,
kuanzia sasa, hautavumilia matusi kwa wachezaji au viongozi wake. Wote
watakaobainika kufanya matendo haya, sheria itachukua mkondo wake.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
Nasikitishwa sana na Radio iliyoaminika kama radio ya michezo na burudani inapogeuzwa chama cha siasa,hii habari imetoka jana lakini kwa sababu inamgusa ibrahim masoud ambaye ni kiongozi jana hajazungumzia kabisa habari za simba,vurugu hizi zingekuwa upande wa pili ungemsikia.Aibu kwenu Clouds kwa unazi
ReplyDelete