Search This Blog

Monday, October 1, 2012

KWANINI NISIAMINI BAADHI YA VIONGOZI WA VILABU WAMEZISALITI TIMU ZAO KWENYE UDHAMINI WA LIGI

 
Na Somoe Ngitu, gazeti la NIPASHE

WAKATI Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ikiwa inaendelea na joto la wapenzi wa mchezo huo likiwa ni katika mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba utakaofanyika keshokutwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, bado najiuliza kwamba, kimeishia wapi kile kilio cha viongozi wa klabu kuhusiana na dau la udhamini wa ligi hiyo?


Je, ni kweli kimeisha hivi hivi kama machozi ya samaki baharini?
Katika mtima wangu, najiwa na hisia mbaya, tena mbaya sana. Nazo ni kwamba, huenda kuna viongozi wa klabu wameamua kusaliti maslahi ya waliyo wengi kwa sababu wanazozijua wenyewe.


Ndiyo. Na wala sihitaji kutumia nguvu nyingi ili kukidhi matakwa ya ile dhana maarufu katika misingi ya hukumu, nayo ni ile ya kuwa na ushahidi usio na shaka (beyond reasonable doubt).
Mtiririko wa yote yanayojiri katika sakata la udhamini wa Ligi Kuu ya Bara unatengeneza mazingira ya kuamini kwamba si bure. Wapo walioamua kusaliti klabu zao. Inawezekana si wote, lakini naamini kwamba wapo. Haki ya nani vile!


Kuna usaliti fl'ani umeingia kwenye suala hili nyeti ambalo ndio msingi wa ushindani wa ligi hiyo inayotoa wawakilishi wa nchi kwenye mashindano ya kimataifa na pia kuzalisha wachezaji wengi wa timu za taifa, hasa ile ya wakubwa ya Taifa Stars.


Najiuliza kwa mfano. Kwamba je; hata kama hakukuwa na kampuni au taasisi nyingine ya kibiashara ambayo ilikuwa tayari kudhamini Ligi Kuu ya Bara, ni kweli kwamba yale madai ya klabu yalipoteza umuhimu wake?


Mimi naamini madai ya klabu kuhusiana na utata wa udhamini yalikuwa ya msingi kutokana na hali halisi ya mazingira ya mchezo huo hapa nchini ambapo klabu hutumia gharama kubwa kuwatangaza wadhamini kuliko kile wanachopata kutoka kwa wadhamini hao.


Binafsi nakumgbuka vyema. Wakati mjadala kuhusiana na udhamini wa ligi na kiwango cha pesa ambacho klabu kitanufaika kutokana na 'dili' hiyo, klabu kadhaa kama za Simba, Yanga na Azam zilikuwa mstari wa mbele katika kupigania kile walichodai kuwa ni haki yao.


Hata hivyo, kadri siku zilivyokuwa zikisonga mbele, ndivyo viongozi wa baadhi ya klabu walivyopotea na kutosikika waziwazi wakilalamikia yale waliyokuwa wakiyasema hadharani kuhusiana na kiwango na aina ya  udhamini. Badala yake, walioonekana kuwa mstari wa mbele katika kupigania maslahi ya klabu katika udhamini ni African Lyon pekee, ambao walijitahidi na kupata mdhamini wao binafsi ambaye hata hivyo, amekataliwa kwa maeolezo kwamba ni mshindani kibiashara na mdhamini mkuu wa ligi. Sasa Lyon wanaonekana kwenda kinyume na sera za mdhamini mkuu na wametishiwa kuondolewa katika ligi kuu.


Binafsi naamini kwamba madai ya Lyon yalikuwa ya msingi kwa sababu klabu kama yao (Lyon) inayotumia zaidi ya Sh. milioni 300 kwa msimu kushiriki Ligi Kuu ya Bara inahitaji kuona kuwa inapata angalau nusu ya gharama hizo kutoka kwa mdhamini na tena kwa wakati muafaka.

Klabu hiyo ambayo mmoja wa wamiliki wake ni  Rahim Kangezi, licha ya kuonekana kuwa na ukorofi, lakini ni wazi kwamba kinachowaponza ni 'ungangari' wao katika kupigania kile wanachokiamini.


Kwa mfano, inakuwaje mdhamini wa Ligi Kuu yenye mechi 26 kwa kila klabu 14 zinazoshiriki ligi hiyo kutoa kiasi cha Sh. bilioni 1.6 kwa msimu wakati huwa kuna mechi zaidi ya 180, huku mdhamini wa sasa wa timu ya taifa (Taifa Stars) akitoa Sh. bilioni 3.5 kwa timu hiyo yenye mechi takriban 8 ndani ya mwaka mmoja, tena karibu nusu zikiwa ni za nyumbani?

 
Wakati viongozi wa Shirikisho la Soka (TFF) walipokuwa wakifanya mazungumzo na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa ajili ya kuidhamini Stars, walizingatia gharama za uendeshaji na mwishowe wakafanya uamuzi mgumu wa kuchana na udhamini wa awali wa  Sh. bilioni 1.2 kwa mwaka na kusaini haraka udhamini mnono wa Sh. 3.5.


Ingawa Stars inasafiri na inacheza mechi za kirafiki ndani na nje ya nchi, mdhamini wake hugharamia baadhi ya gharama kwa timu za mataifa mengine ambazo huzialika kuja hapa nchini pia, lakini tofauti ya udhamini huo na huu unaodaiwa kukubaliwa na viongozi wa klabu ni kubwa mno kulinganisha na mahitaji halisi ya uendeshaji wa timu inayoshiriki ligi kuu.


Klabu zinazunguka katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mbeya, Arusha, Tanga, Mwanza na Bukoba mkoani Kagera kucheza mechi za ligi na baadhi yao hujikuta wakienda kwenye kanda mojawapo mara mbili kutokana na ratiba ilivyo, hivyo kujikuta wakitumia kiasi kikubwa cha fedha kugharimia usafiri na malazi ya timu wawapo ugenini.


Ni jambo lililo wazi kwamba ni mechi chache sana ambazo walau timu hupata pesa za kupunguza makali ya gharama, na hasa zile zinazohusisha klabu za Simba na Yanga.
Kwa ufupi, mapato yatokanayo na viingilio vya mechi nyingine nyingi huwa hayatoshi hata kidogo katika kusaidia maandalizi ya timu.


Katika hali kama hii, mfuatiliaji mwingine wa maendeleo ya klabu zetu anaweza kuhoji kuwa je, ni klabu ngapi kati ya 14 zilizoridhia haki ya kipekee ambayo wadhamini wakuu wameipata?
Kwa mfano, hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia, alieleza kwamba klabu zimekuwa vigeugeu kwa kubadilisha mawazo yao kila mara wanapokutana. Alisema wazi kuwa jambo hilo limewafanya wafikie hapo walipo sasa ambapo hadi ligi ikianza, walikuwa bado hawajapokea fedha wala vifaa kutoka kwa mdhamini mkuu.


Aliwahi kueleza kwamba kuna kikao kimoja waliitisha na viongozi waliohudhuriwa walikuwa ni wa klabu tatu za Simba, Ruvu Shooting na Coastal Union. Lakini baada ya kikao hicho,  viongozi wa klabu nyingine waliodai kuwa hawako jijini, alikutana nao na walichomueleza ni kwamba walishindwa kuhudhuria kwavile walipewa taarifa ndani ya muda muda mfupi.


Inawezekana ni kweli viongozi hao walikuwa mbali na jijini Dar es Salaam ambapo vikao hivyo hufanyika. Lakini vile vile inawezekana kwamba kulikuwa na 'ujanja ujanja' wa kupitisha maamuzi kwa kuhusisha viongozi wachache.


Wakati wa maboresho ya mkataba mpya klabu zilisikika wazi zikisema kwamba zinahitaji kuona msimu huu wa ligi zawadi na fedha zinazotolewa na mdhamini zilingane na hadhi ya ligi husika,  huku wakieleza kwamba wadhamini hao hao ndio waliokuwa wakidhamini mashindano ya urembo ya Miss Tanzania na kutoa zawadi za gari na fedha taslimu (ukijumlisha thamani ya gari na fedha) jumla yake inakuwa kubwa kuliko zawadi ya bingwa wa ligi ya Bara.


Inakuaje TFF inakubali udhamini wa Sh. milioni 880 kwa mashindano ya wiki mbili ambayo bingwa wake anapata Sh. milioni 40 na shirikisho hilo hilo linaona ni sahihi kukubali Sh. bilioni 1.6 kwa ligi inayochezwa kwa kipindi kisichopungua miezi nane na kuhusisha mechi zaidi ya 180?


Kwa haya yaliyojiri wakati wa mjadala kuhusu udhamini wa ligi kuu, naamini kwamba hakuna wa kuzuia hisia zangu na pengine wafuatiliaji wengi wa soka kuwa kuna viongozi wa klabu wamesaliti klabu zao na kuweka mbele maslahi yao.


Inawezekana kwamba hivi sasa ikawa ngumu kuthibitisha ukweli wa hisia hizo. Lakini ni wazi kwamba ipo siku tutasikia undani wa kile kinachotokea sasa.


Haswa! Na tuipe subira nafasi yake. Tutasikia tu kwamba viongozi "X" na "Y" walifanya hivi na vile wakati wa mchakato wa kujadili udhamini wa ligi kuu ya Bara.
----

No comments:

Post a Comment