Search This Blog

Sunday, October 28, 2012

AZAM FC INAHITAJI MBINU ZAIDI ILI IWEZE KUTWAA UBINGWA WA VPL.


Simba iliongeza 'gepu' la pointi baina yake na Azam FC, katika msimamo wa ligi kuu Bara, baada ya kuifunga timu hiyo iliyokuwa haijapoteza mchezo wowote katika ligi. John Bocco alifunga mapema tu, dakika ya nne ya mchezo huo, lakini, Felix Sunzu, aliisawazishia timu yake dakika tatu baadaye, kabla ya Emmanuel Okwi kufunga mara mbili na kutengeza pengo la pointi nne baina yao, huku, Azam ikilala kwa mara ya kwanza baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1.
       SIMBA SC
Iliingia katika mchezo huo ikiwa na presha ya kuhakikisha ni lazima washinde, baada ya sare tatu mfululizo, wapenzi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo waliingia katika presha ya kuushinikiza uongozi wao wa juu kuitisha mkutano wa dharura. Wachezaji kadhaa wakaondolewa kikosini kwa sababu mbalimbali, Haruna Moshi, akasimamishwa kwa siku 21, Juma Nyosso, akapelekwa kikosi B, akaimarishe kiwango chake. Wengi wakataka kuona itakuwaje katika mchezo wa jana, kocha, Milovan Curkovic, akawa na jibu.
Urejeo wa mchezaji, Shomari Kapombe katika safu ya ulinzi wa kati ilionekana ni nafuu zaidi kuliko kama angetumika mchezaji mwingine yoyote katika nafasi hiyo ndani ya Simba, aliweza kucheza vizuri na kuhakikisha njia zote ambazo viungo wa Azam FC, huwa huwatengenezea nafasi washambuliaji wao, John Bocco na Kipre Tcheche, hazionekani. Kapombe alicheza kama namba nne sahihi, na kuna wakati akawa akijibadilisha na kuwa namba sita 'kivuli', alimzima kabisa, Bocco hasa baada ya mshambuliaji huyo wa Azam, kufunga mwanzoni tu mwa mchezo. Wakati mzuri zaidi kwa, Simba jana ilikuwa ni pale walinzi hawa wawili wa kati ( Paschal Ochieng na Kapombe) walipokuwa wakibadilishana majukumu kwa namna washambuaji, Kipre na Bocco, walivyokuwa wakijaribu kujibadilisha zaidi kutoka washambuliaji hadi kuwa viungo washambuaji, lakini walizimwa na Simba ikaonesha uwezo wa juu kuanzia katika mikono ya Kipa, Juma Kaseja hadi safu ya ulinzi. Ushindi wa Simba ilikuwa ni walinzi hawa kwa kushirikiana na wale wa pembeni, Nassorro Chollo na Amir Maftah wakiwazima wafungaji bora wa Azam, Bocco mwenye mabao manne na Kipre mwenye mabao matano.
      AZAM FC
Waliiingia huku wakiamini matatizo makubwa yaliyopo ndani ya timu ya Simba yatawasaidia kuondoka na ushindi 'mnono' na mara baada ya kupata bao la kuongoza kabla ya hata dakika ya tano, Azam wakaamini, Simba inafungika. Wakajiamini zaidi, kuliko walivyokuwa wakijiamini awali. Lilikuwa kosa, wakasahau kuwa wanacheza na timu kubwa nchini, wakasahau kuwa wanacheza na Simba ambayo ndiyo bingwa mtetezi wa ligi kuu. Ili kuwa bingwa wa michuano yoyote ile ni lazima kwanza uzifunge timu ambazo unagombea nazo ubingwa wa michuano husika. Msimu uliopita kama, Azam ingeshinda walau mchezo mmoja tu dhidi ya Simba, bila shaka yoyote wangekuwa mabingwa wa ligi kuu. Wakati wakimaliza msimu wakiwa pointi tatu pungufu dhidi ya Simba, Azam wangenufaika sana kama wangepata pointi mbele ya Simba, lakini walishindwa.
Uwezo wao mdogo wa kiufundi katika michezo mikubwa umeendelea kuwasumbua. Katika mchezo wa jana, Azam ilikuwa katika ' shepu nzuri ya mchezo kuliko Simba' lakini Simba walitumia kila wanaloweza kuhakikisha hawapotezi mchezo huo, kwani walitambua wazi kuwa endapo watafungwa watawaacha wapinzani waende juu yao kwa tofauti ya pointi moja zaidi uku wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Lakini wakati, wenzao wakijiamini zaidi, Simba waliendelea kutafakari kwa kina matukio yote ambayo yametokea ndani ya klabu yao ndani ya wiki nzima, na wachezaji wakaingia huku wakijua fika wanakwenda kucheza mchezo mgumu, lakini ili kutuliza mambo ni lazima washinde. Azam ilikuwa na viungo wanne wazuri katikati ya uwanja. Abdulhalim Humud, Jabir Aziz, Himid Mao, na Salum Abubakary, lakini wachezaji hawa ambao wamekuwa ni silaha ya kujihami ya timu hiyo walijigeuka kutoka viungo wachezesha timu bora hadi kuwa viungo 'wachapa viatu' bora, walionekana kukosa ubunifu mbele ya Amri Kiemba, Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto, ambao wao waliamua kujiondoa katika utamadauni wa Simba wa mchezo wa pasi fupi fupi hasa wakianzia nyuma na kusogea na mpira, na Simba ikaamia katika mchezo wa mipira mirefu, Mwinyi akawa anapiga pasi ndefu, Kwa Mrisho Ngassa upande wa pembeni, au kwa Emmanuel Okwi, upande mwingine.
Viungo wa Azam, wakaanza kukimbia huku wakiitazama mipira ikipita kutoka upande mmoja wa uwanja hadi upande mwingine, wakashindwa hata kujikusanya wenyewe na kutafakari nini wanatakiwa kufanya, kila mmoja akaanza kucheza rafu pale alipoona anazidiwa, wakaanza kupata kadi za 'manjano' na matokeo yake wakakosa kujiamini, wakakosa mbinu mpya za kuituliza timu na mwisho wakaaanguka wao na timu yao hadi katika nafasi ya tatu, baada ya mchezo mmoja tu dhidi ya timu ambazo zinatawala ligi kuu ya Tanzania Bara kwa miaka mingi. Azam, walionekana kukosa njia mbadala na hata pale walipoamua kujaribu kujinasua katika hali hiyo, wakajikuta wakipigwa kitanzi na Okwi, Ngassa, akawa juu kiuwezo na kumsumbua mlinzi, Samih Nuhu.
          SAFU YA ULINZI YA AZAM NA MICHEZO MIKUBWA

Wakati wakifungwa na Yanga katika michuano ya Kagame Cup, Azam walionekana kutawala sana mchezo ule wa fainali, lakini wakakwamishwa na uwezo wao mdogo wa safu ya ulinzi katika kuzuia. Matokeo yake wakafungwa kirahisi mabao 2-0. Wakarejea katika mchezo muhimu wa Ngao ya Jamii, na wakawa mbele kwa mabao 2-0, lakini, Simba, ikasawazisha na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. Na baada ya kucheza michezo nane pasipo kufungwa, Azam, imepewa 'onyo' kali na washambuaji wa Kimataifa wa Simba, Felix Sunzu na Okwi kuwa ni timu dhaifu katika kucheza mipira ya juu, ile ya krosi na kona inawasumbua sana walinzi wao wote, kuanzia kwa Aggrey Morris, Said Mourad hata mzoefu, Ibrahimu Shikanda, wote hawajui nani ni mchezaji hatari wa mipira ya juu katika timu pinzani na anatakiwa kuwa chini ya nani. Ni mambo ambayo yamekuwa yakiigharimu timu hii hasa katika wakati ambao wanatakiwa kuzifunga timu kubwa au ngumu ili waweze kuwa juu yao. Ni vitu ambavyo vinatakiwa kufanyiwa kazi sana na maofisa wao habari, kuchunguza kila mbinu za wachezaji wa timu pinzani hasa katika michezo muhimu. Kama huwa wanafanya basi wanashindwa kutimiza wajibu wao. Safu hii ya ulinzi imekuwa ikiwaaangusha katika kipindi muhimu zaidi ambacho kablu inahitaji kufika tangu kuanzishwa kwake.
        CHA KUJIFUNZA NA CHA KUZINGATIA BAADA YA MCHEZO WA JANA
Timu zote zitaiwakilisha nchi katika michuano ya CAF, hapo mwakani, Simba watacheza michuano ya Klabu bingwa na Azam FC kwa mara ya kwanza wataingia katika soka la Afrika wakicheza michuano ya Shirikisho. Kwa mchezo wa jana ambao ni wa mwisho mkubwa kwa Simba mwaka huu, umeonesha kuwa Simba bado inahitaji nguvu zaidi katika idara ya kiungo mlinzi na ile ya beki namba tano. Anatakiwa kupatika mtu anayetambua majukumu yake hasa katika nafasi husika, tena wanatakiwa kuwa wachezaji wazoefu zaidi na si wanaokuja kujifunza soka.
Kwa upande wa Azam, wanatakiwa kuongeza ubunifu hasa wanapokuwa wamekamatwa. Azam, ni kama ilivyo kwa Barcelona, haina mbinu mbadala ya kujiepusha na 'kipigo mbele ya timu inayoingia uwanjani na kuwazima mapema kamna walivyofanya Simba hapo jana. Azam, wanakwenda katika michuano ya Kimataifa, lakini tayari wakiwa na mkusanyiko mzuri wa wachezaji, lakini bado haitoshi wanahitaji kuwa na mlinzi kama Joseph Owino katika ngome yao ili awesaidie katika kuondosha mipira ya juu. Ni lazima watafute mlinzi mmoja wa kuaminika wa kati kwa sababu hawana mlinzi yoyote ambaye anaweza kusimama na kuisogeza timu hiyo mbele kimataifa.

2 comments:

  1. Nimesoma makala yako ndefu na nzuri kiufundi lakini kilichowafunga azzam jana ni nje ya uwanja na sio uwezo.fatilia kaka,soka la bongo lina sifa zake mkuu,wenyewe wanaita bongo fitna

    ReplyDelete
  2. Mawazo ya nje ya uwanja hayana basis na yanatend kutupa majibu rahisi yasio tusaidia kwenda mbele.Lets work on principals. Nakubaliana na mwandishi wa makala hiyo juu ndefu lakini pia nakubali nadharia ya kuwa Azam inategemea zaidi striking force ya John Boko kufanya timu pinzani iwe katika tension muda wote. Ni kama Messi wao bila ya Boko timu inakosa punch na kufanya timu pinzani ijiamini na kushambulia bila wasiwasi kuwa wataadhibiwa. Naamin pia kuwa kwa kuumia Boko labda Mwaikimba angeweza kusumbua defence line ya Simba na kuwafanya wasiende mbele at will.

    ReplyDelete