Tumepokea
barua kutoka Kitengo cha Sheria cha Shirikisho la Kimataifa la Vyama
vya Mpirawa Miguu (FIFA) likitutaka tuitaarifu Yanga kuhusu mashtaka
yaliyowasilishwa na kocha wazamani wa klabu ya Yanga, Kostadin Papic.
Katika malalamiko yake, Papic anadai kuwa hajalipwa malimbikizo ya
mshahara wake yanayofikia kiasi cha Dola 12,300 za Kimarekani. Katika
barua yake, kocha huyo anadai kuwa alikuwa akiwasiliana na maofisa na
viongozi wa Yanga, lakini hakupata ushirikiano na hivyo kuamua kwenda
FIFA. TFF ilifanya juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko hayo
ili kujaribu kumzuia kocha huyo asishtaki FIFA, lakini juhudi hizo
hazikuzaa matunda.
Kama
chombo kinachosimamia uendeshaji wa mpira wa miguu nchini, TFF
imesikitishwa na habari hizo na inaiomba klabu ya Yanga kufanya kila
jitihada kuhakikisha kuwa inawasilisha taarifa zote muhimu na nyaraka
zinazohusiana na stahiki za kocha huyo ili kama ilishamalizana naye,
sifa ya klabu ya Yanga isafishwe. Tayari barua imeshaandikwa kwa klabu
ya Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapema iwezekanavyo.
Tukio
hilo, si tu linachafua sifa ya klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania
kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la
malipo ya makocha nchini, ni dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu
zetu na hata timu za taifa kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa
watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya kazi nchini.
Hili
ni tukio la pili kwa Yanga baada ya mchezaji wake mwingine, John
Njoroge kuishtaki klabu hiyo FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa
mwezi Januari na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha FIFA (DRC).
Ushindi wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza
kumlipa mchezaji huyo kasi cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika
adhabu ambayo itatulazimisha tuishushe daraja; kuinyang’anya pointi kwa
kiwango kitakachotajwa na FIFA; kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa
pamoja. Tunaiomba Yanga itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa
kwenye barua ya FIFA ili kuepuka hatua hizo.
Suala
la Njoroge ni moja kati ya matukio mengi yanayohusu ukiukwaji wa
taratibu za kuvunja mikataba yanayofanywa na klabu zetu. Kuna malalamiko
ya wachezaji wengi dhidi ya klabu zao za zamani kuhusu kutolipwa
stahiki zao. Hivyo TFF inatoa wito kwa klabu kujiepusha na vitendo hivyo
kwa kuwa vinawanyima haki wachezaji, lakini pia vinachafua sifa ya nchi
iwapo wachezaji wanachukua hatua za kwenda kwenye vyombo vya juu.
Tumekuwa
tukisoma kwenye vyombo vya habari kuhusu kutimuliwa kwa sekretarieti
nzima ya Yanga kutokana na kuonekana kuwa ina udhaifu. Taarifa hizo
hazijaifikia rasmi TFF. Kiutaratibu, Yanga inatakiwa iwsasilishe majina
ya maofisa watakaofanya kazi na TFF kwa sasa na itakapoajiri
sekretarieti ya kudumu, basi itume barua nyingine ya kuwatambulisha
watendaji wake.
Kama
itakuwa imeitimua sekretarieti nzima, basi TFF inapokea taarifa hizo
kwa masikitiko makubwa. Si nia ya TFF kutetea watendaji wazembe, lakini
klabu hazina budi kufuatilia kwa karibu utendaji wa sekretarieti zao ili
isije ikafikia wakati sekretarieti nzima inaondolewa kwa makosa ambayo
yangeweza kusahihishwa kama kungekuwa na ufuatiliaji wa karibu. TFF
imekuwa ikitoa mafunzo kwa watendaji wa klabu ili waweze kufanya kazi
zao vizuri na kwa mintaarafu ya mpira wa miguu na hivyo kuondolewa kwa
timu nzima kama hiyo kunamaanisha kuwa ni upotevu wa rasilimali ambayo
imetumika kuwapa elimu ya kutenda kazi zao vizuri. TFF ilishafanya kozi
ya Event Management kwa ajili ya watendaji wa klabu; semina ya kuangalia
upya maazimio ya Bagamoyo kwa watendaji na viongozi na pia kozi ya
utawala hivyo haipendi juhudi hizi zipotee
kirahisi.
Angetile Osiah
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment