Search This Blog

Thursday, September 27, 2012

WAZIRI MKUU WA CAMEROON AINGILIA KATI ISHU YA ETO'O KWENYE TIMU YA TAIFA - AMSHAWISHI ARUDI KIKOSINI


Takribani mwezi mmoja baada ya kuandika barua ya kugoma kuichezea timu ya taifa ya Cameroon, mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani kwa upande wa soka, Samuel Eto'o sasa anaonekana yupo tayari kwenda kinyume na msimamo wake wa mwanzo na kurudi kuitumikia timu ya taifa lake baada ya kuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo.

Mshambuliaji huyo wa klabu ya Anzhi Makhachkala alifungiwa kwa miezi nane baada ya kuongoza mgomo wa wachezaji dhidi ya Chama cha Soka cha Cameroon kuhusiana na posho zao.

Hata alipomaliza kutumikia adhabu hiyo na kuitwa kikosini, Eto'o alikataa na kusema kwamba hataichezea tena timu ya taifa hadi hapo viongozi wa chama cha soka nchini mwake watakapobadilika na kufanya kazi kwa weledi mkubwa na unaostahili.

Jambo hilo sasa linaelekea kupata ufumbuzi baada ya Waziri Mkuu Philemon Yang kuzungumza yeye mwenyewe na mtupia mabao huyo wa zamani wa Barcelona na kumuomba arudi kikosini ili aisaidie nchi yake inayohaha kupata nafasi ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2013).

“Mkuu wa Nchi ameamua kulishughuilikia suala hilo yeye mwenyewe na ametupa maelekezo,” amesema kocha wa Cameroon, Jean-Paul Akono.

“Baadaye tulikutana kuweka mambo sawa na sasa kila kitu kiko vizuri. Hivi sasa yuko tayari, lakini anaweza kukosekana kwa sababu ya majeraha. Tutaendelea kuomba na kusubiri siku za mwisho kabla ya mechi."

Cameroon walichapwa 2-0 katika mechi yao ya ugenini dhidi ya Cape Verde, ambayo ni ya kwanza katika raundi ya mwisho ya kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON 2013, na kurejea kwa Eto’o kunatarajiwa kuwaongezea nguvu katika mechi yao ya marudiano mjini Yaounde Oktoba 13.

No comments:

Post a Comment