Search This Blog

Friday, September 7, 2012

TAIFA STARS YAPANGWA KUCHEZA NA UGANDA KUWANIA TIKETI YA CHAN 2012

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imepangiwa kucheza na Uganda (The Cranes) katika raundi ya kwanza ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika Afrika Kusini mwaka 2014.
 
Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa jana (Septemba 7 mwaka huu) makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) jijini Cairo, Tanzania imeingia moja kwa moja raundi ya kwanza ambapo itacheza na Uganda.
 
Mechi ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kati ya Juni 21,22 na 23, 2013 wakati ya marudiano itakuwa Uwanja wa Mandela ulioko Namboole jijini Kampala kati ya Julai 5,6 na 7, 2013.
 
Nchi 38 zinashiriki katika mechi hizo za mchujo ambapo nyingine zitaanzia raundi ya awali itakayochezwa kati ya Novemba 30 na Desemba 1 na 2 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Desemba 14,15 na 16 mwaka huu.
 
Ratiba imepangwa kwa makundi ya kanda ambapo jumla ya timu 16 ndizo zitakazocheza fainali hizo nchini Afrika Kusini. Kanda hizo ni Kaskazini itakayopeleka timu mbili katika fainali, Magharibi A (timu mbili), Magharibi B (timu tatu), Kati (timu tatu), Kati Mashariki (timu tatu), Kusini (timu tatu akiwemo mwenyeji Afrika Kusini).
 
Kwa upande wa kanda ya Tanzania (Kati Mashariki), timu zinazoanzia raundi ya awali ni Burundi, Eritrea, Ethiopia na Kenya.
 
Fainali za Kwanza za CHAN zilifanyika mwaka 2009 nchini Ivory Coast ambapo Tanzania ilishiriki huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ikiibuka bingwa. Fainali za Pili zilichezwa mwaka 2011 nchini Sudan ambapo Tunisia ilitwaa ubingwa. Fainali za Kwanza zilishirikisha timu nane kabla ya kuongezwa hadi 16 za sasa.

No comments:

Post a Comment