Search This Blog

Tuesday, September 11, 2012

TAARIFA RASMI DHIDI YA MAPINGAMIZI YA WACHEZAJI KUTOKA TFF

Kiggi Makassy mmoja ya wachezaji waliokuwa wamewekewa pingamizi
 
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 10 mwaka huu) ili kupitia na kutoa uamuzi/ushauri kwa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake.
Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
Suala la ugombea wa Michael Wambura katika FAM
Michael Wambura aliomba uongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM) katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliondoa jina lake kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo.
Wambura hakuridhika na uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya TFF. Kamati hiyo katika uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya kushughulikia shauri hilo. Baadaye Wambura alikata rufani katika Kamati ya Rufani ya TFF ambayo ilimpa haki ya kugombea.
Kutokana na mkanganyiko huo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa mwisho katika masuala ya uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa Kamati ya Rufani kuhusu uchaguzi wa mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya TFF iliomba mwongozo wa kisheria kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji.
Kwa vile Kamati hizo mbili (Uchaguzi na Rufani) haziko katika mtiririko wa moja kwa moja wa utoaji maamuzi, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliishauri Sekretarieti ya TFF kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ili kupata muongozo juu ya suala hilo.
Katika muongozo wake, FIFA ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF chombo cha mwisho cha rufani katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa TFF ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si vizuri chombo kimoja kikawa msimamizi wa uchaguzi, na chenyewe tena ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi kwenye uchaguzi husika.
Hivyo, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo mawili kwenda Kamati ya Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili kiwepo chombo kingine cha rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Mapendekezo hayo ni; Iundwe Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote zinazotokana na uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF isiwe chombo cha mwisho cha uamuzi kwa rufani zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF.
AU. Rufani zote zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF zisikilizwe na Kamati ya Rufani ya TFF. Kwa maana hiyo Kamati ya Rufani ya TFF ndiyo kiwe chombo cha mwisho kwa wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwasilisha malalamiko yao.
USAJILI/PINGAMIZI DHIDI YA WACHEZAJI
Musa Hassan Mgosi, Ayoub Hassan Isiko
Mchezaji Musa Hassan Mgosi ameombewa usajili Ruvu JKT kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na Ayoub Hassan Isiko ameombewa usajili Mtibwa Sugar kutoka Bull FC ya Uganda. Wachezaji hao hawaruhusiwi kuchezea timu hizo mpaka Hati zao za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) zitakapokuwa zimepatikana.
Toto dhidi ya Kagera Sugar kumsaini Enyinna Darlinton Ariwodo
Toto Africans ilipinga usajili wa Enyinna Darlinton kwa timu ya Kagera Sugar kwa vile bado ina mkataba wa mchezaji huyo ambao unamalizika mwakani.
Kwa upande wake Kagera Sugar ilisema imemsaini mchezaji huyo kwa vile Toto Africans imeshindwa kumlipa mshahara ambapo kuna makubaliano rasmi kati ya Ariwodo kuwa klabu hiyo ikishindwa kumlipa mshahara anaruhusiwa kuondoka.
Uamuzi wa Kamati ni kuwa Ariwodo ni mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile Toto Africans ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba.
Ramadhan Chombo ‘Redondo’
Redondo ameidhinishwa kuchezea Simba kwa kuzingatia mchezo wa haki na uungwana (Fair Play) baada ya klabu hiyo na ile ya Azam kufikia makubaliano kuhusu mchezaji huyo.
Mchezaji David Luhende kusajiliwa Yanga
Yanga ilikiri kutolipa ada ya uhamisho ya sh. milioni 5 kama walivyokubaliana na Kagera Sugar. Awali waliipa Kagera Sugar hundi iliyogonga mwamba benki (bounced cheque). Shauri hilo lilimalizwa kwa Yanga imetakiwa kulipa fedha hizo ndani ya siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu.
Super Falcon dhidi ya Edward Christopher kusaini Simba
Simba imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu iwe imeilipa Super Falcon fedha za matunzo (compensation) kwa vile ndiyo iliyomlea mchezaji Edward Christopher aliyesajiliwa katika klabu hiyo.
Toto Africans dhidi ya Mohamed Soud kusajiliwa Coastal Union
Toto Africans iliweka pingamizi kwa maelezo kuwa bado ina mkataba na mchezaji huyo. Hivyo kwa msingi wa Fair Play, mchezaji huyo ameidhinishwa Coastal Union baada ya makubaliono kati ya klabu.
Rollingstone dhidi ya Kigi Makassy kusajiliwa Simba
Simba imetakiwa kuilipa Rollingstone gharama za matunzo ilizoingia wakati ikiwa na mchezaji huyo kwa kuzingatia kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Super Falcon dhidi ya Sultan Juma Shija kusajiliwa Coastal Union
Uamuzi wa Kamati ni kuwa Shija atachezea Coastal Union, na kwa vile yuko chini ya umri wa miaka 23, Coastal Union itailipa Super Falcon fidia ya fedha ilizotumia kumhudumia mchezaji huyo.
African Lyon dhidi ya Razak Khalfan kusaini Coastal
Lyon imesema bado ina mkataba na mchezaji huyo. Kamati imebaini kuwa mkataba wa mchezaji huyo na Lyon umemalizika, hivyo ni mchezaji halali wa Coastal Union.
Flamingo dhidi ya Kelvin Friday kusajiliwa Azam
Friday ruksa kucheza Azam, lakini klabu hiyo imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu kuilipa Flamingo gharama za kuvunja mkataba.
Super Falcon dhidi ya Robert Joseph Mkhotya kusaini African Lyon
Lyon imeagizwa kuilipa Super Falcon sh. milioni moja ikiwa ni fidia ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo ambaye imemsajili. Fedha hizo zitalipwa kwa awamu nne kutokana na makato ya mlango yatakayofanywa na TFF. Falcon itapokea malipo hayo kupitia TFF.
Oljoro JKT dhidi ya Othman Hassan kusajiliwa Coastal
Kwa mujibu wa rekodi za TFF, mkataba wa mchezaji huyo na Oljoro JKT unamalizika mwakani. Hivyo, Othman Hassan ni mchezaji halali wa Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na klabu hiyo.
Yanga dhidi ya Simba kuacha wachezaji wanne
Kamati imetupa pingamizi hizo kwa vile hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji juu ya kuvunjiwa mikataba yao. Wachezaji hao walioachwa na Simba ni Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiavanga na Lino Masombo.
Ikiwa wachezaji hao watakuwa na malalamiko kuhusu kuvunjiwa mikataba suala hilo litafikishwa katika Kamati kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
Mbuyu Twite
Kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali. Hata hivyo, kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Kelvin Yondani
Kwa mujibu wa Ibara ya 44(3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kelvin Yondani, hivyo ni mchezaji wake halali.
Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji

No comments:

Post a Comment