Search This Blog

Sunday, September 2, 2012

HARUNA MOSHI BOBAN ALIVYOTOKA KWENYE MSHAHARA WA DOLA 5,000 MPAKA $700




 Miaka 3 iliyopita Haruna Moshi Boban alikuwa nchini Sweden akicheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Gefle inayoshiriki ligi ya daraja la kwanza nchini humo. Muda mfupi baada ya kukaa nchini Sweden huku akiwa mmoja ya wachezaji wa kutegemewa na klabu hiyo kwenye michuano mbalimbali iliyokuwa ikishiriki, Haruna ghafla akaamua kurudi nyumbani Tanzania huku akiwa bado na mkataba na klabu hiyo.

Alivyorudi nyumbani akakaa kwa muda bila timu na hatimaye akasajiliwa na timu yake ya Simba iliyomuuza kwenda huko ughaibuni.
Boban na Alexander Gerndt dimbani wakiwa wote Gefle IF

Wakati Haruna akiwa nchini Sweden alikuwa akilipwa kiasi cha dola 5,000 kwa mwezi, huku akipewa huduma zote muhimu, na baada ya kufanya vizuri katika kipindi kifupi alichokaa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuongezewa maslahi kama angeongeza bidii kidogo kwa bahati mbaya au kutokuwa na maamuzi mazuri akaamua kundoka kwa sababu zisizoeleweka na zisizo na maana.

Ndani ya kikosi cha Gefle, Haruna alikuwa ameiingia kwa pamoja na wachezaji ambao baadae wakawa marafiki wakubwa kwenye timu hiyo Alexander Gerndt raia wa Sweden na Mghana Yussif Chibsah, na wote walikuwa wanaringana kwa kiwango cha mshahara, kwa bahati nzuri zaidi kati yao Haruna ndio alikuwa akionekana kuwa na nafasi kubwa ya kuboreshewa mshahara.

Yussif Chibsah rafiki mkubwa Boban wakati wakiwa wote pale Gefle IF
Lakini Haruna akaamua kurudi Bongo, wenzie Gerndt na Chibsah wakaendelea kujituma na kucheza kwa bidii. 

Kutokana na malengo, management nzuri na uvumilivu waliokuwa nao matokeo yake wakaanza kuvuna walichopanda. 

 Yussif Chibsah, aliyetoka nchi kwao Ghana mwaka 2006 na kuanza kusota kwenye timu za madaraja ya chini nchini Sweden huku akilipwa fedha za kawaida, lakini kutokana na kujua nini anataka akaendelea kucheza bila kukata tamaa na hatimaye kusajiliwa na klabu kubwa ya Gefle. Akiwa Gefle pia alikuwa akilipwa mshahara wa chini ya $5,000 kwa mwezi lakini aliongeza bidii na hatimaye akaonekana na klabu kubwa zaidi ya Sweden iliyopo mji mkuu wa nchi hiyo Stockholm ya Djurgåden IF, ambao walilipa kiasi cha $1,000,000 kwa Gefle kumpata Mghana,  na kwa sasa analipwa mshahara wa $18,000 baada ya kodi huku akipewa mhitaji mengine yote muhimu na posho kubwa kila baada ya mchezo.

Alexander Gerndt akiwa na jezi ya klabu yake mpya ya Ultretch ya Uholanzi
 Kwa upande wa Alexander Gerndt ambaye akiwa Gefle IF msimu wa kwanza na akina Haruna hakuwa kwenye kiwango kizuri na hivyo pamoja na kuwa mzawa bado hakuweza kupewa nafasi ya kufanya vizuri mbeleni kama Mnyamwezi wa Tabora Haruna Moshi - Gerndt hakukata tamaa aliendelea kuituma na msimu uliofuata kacheza vizuri sana na kufunga mabao mengi muhimu kiasi cha kuanza kuzivutia klabu nyingine kupata saini yake.

Mabingwa sasa wa Sweden Helsingborg IF timu ambayo alikuwa akiichezea Henrik Larsson  ndio wakaibuka na ushindi kwenye mbio za saini yake, akiwa analipwa $20,000 baada ya kodi. Akiwa na Helsinborg akacheza vizuri sana na kiasi cha kuwa mchezaji bora wa ligi kwa msimu wa 2010/11. Hatimaye muda kuondoka Sweden ukafika, klabu ya Ultretch ikamsainisha mkataba wa miaka minne wenye thamani ya millioni 27 za kisweden, akiwa analipwa dola 35,000 kwa mwezi.  

Baada ya kuangalia maisha yalivyowabadilikia wachezaji hawa Yussif Chibsah na Alexander Gerndt ambao walikuwa wakicheza na Boban kwenye timu moja, tena Haruna akiwa kwenye mazingira mazuri ya kufanikiwa kuliko ilivyokuwa kwa wenzake. Unadhani ni wapi Boban angekuwa anacheza sasa hivi kama angeongeza bidii na kujituma na kuwa mvumilivu? Bahati mbaya sio wote tulibarikiwa kuwa na akili ya kufanya maamuzi mazuri lakini hivi ndivyo Haruna Moshi Boban alivyotoka kulipwa $5,000 kwa mwezi mpaka $700 kwa mwezi.

KWELI NG'OMBE WA MASKINI HAZAI


2 comments:

  1. hahahahahahahahahahahaha aliwazalo mjinga ndio litakalo mtokea,aliwaza home kula kaalmati sasa alekaalimati waache wakina yusuf wapete next time utasikia yussuf kasajiliwa nottinghamforest

    ReplyDelete
  2. Mimi binafsi simlaumu ila namuonea huruma kwa kutokuwa na washauri wazuri.Ndio maana wenzetu ulaya wachezaji wanakuwa na mawakala wao ambao ndio wanakuwa na jukumu la kuwashauri na kuwatafutia timu nzuri zenye maslahi zaidi. Kwa jinsi Boban alivyo sidhani hata kama anajutia kurudi bongo.

    ReplyDelete