Ngorongoro Heroes, timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20
imewasili asubuhi hii (Agosti 10 mwaka huu) kwa ndege ya Overland
Airways kwenye mji wa Ilorin, Jimbo la Kwara lililo Kusini mwa Nigeria
tayari kwa mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji Flying Eagles
itakayochezwa Jumapili.
Mechi hiyo ya raundi ya pili ya michuano
ya U20 ya Afrika itachezwa kwenye Uwanja wa Township kuanzia saa 10
kamili jioni kwa saa hapa ambapo Tanzania itakuwa ni saa 12 kamili
jioni. Ngorongoro Heroes ilitua jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Lagos
ambapo ililala kabla ya kuja hapa.
Msafara wa Ngorongoro Heroes
wenye watu 27 ukiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) ulipokea na Ofisa Ubalozi wa
Tanzania nchini
Nigeria, Jones Mndeme na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Nigeria (NFF) umefikia hoteli ya Kingstone Grand Suites.
Kwa
mujibu wa Kocha wa Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen, timu itafanya
mazoezi leo jioni (Agosti 10 mwaka huu) wakati mazoezi ya mwisho
yatakuwa kesho jioni (Agosti 11 mwaka huu) kwenye uwanja ambao utatumika
kwa mechi ya Jumapili.
Wachezaji wote wako katika hali nzuri
isipokuwa Issa Rashid na Aishi Manula ambao walikuwa wakisumbuliwa na
tumbo baada ya timu kufika jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Nairobi,
Kenya ambapo ilibadili ndege kuja Nigeria. Hata hivyo, hali zao
zinaendelea vizuri na huenda wakawa sehemu ya kikosi cha kwanza
kitakachoivaa Flying Eagles.
Mbali ya Rashid na Manula, wachezaji
wengine walioko hapa kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Barwany
Khomeiny, Samir Ruhava, Dizana Yarouk, Leonard Muyinga, Hassan Ramadhan,
Jamal Mroki, Omari Kheri, Frank Domayo, nahodha Omega Seme, Abdallah
Kilala,
Hassan Dilunga, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Said Zege, Atupele Gren
na Ramadhan Salum.
Mbali ya Michelsen, Benchi la Ufundi linaundwa
na Mohamed Rishad 'Adolf' (Kocha Msaidizi), Peter Manyika (Kocha wa
makipa), Nassoro Matuzya (Daktari), Joakim Mshanga (Physio), Juma
Kizwezwe (Mtunza vifaa) na Meneja wa timu John Lyimo.
Flying
Eagles ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 2-1 nayo tayari
imeshaingia hapa Ilorin ikitokea Lagos kwa mechi hiyo ambayo matokeo
yake yataamua timu ipi itaingia raundi ya tatu ambayo ni ya mwisho kabla
ya fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20
zitakazofanyika mwakani nchini Algeria. Timu itakayovuka itacheza raundi
hiyo na mshindi kati ya Congo Brazzavile na Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment