Search This Blog

Saturday, August 25, 2012

MBWANA SAMATTA ANAVYOTISHIA UTAWALA WA TRESOR MPUTU TP MAZEMBE


Na Edo Kumwembe

Huu ni mfululizo wa makala za Mbwana Samatta ambaye anachezea TP Mazembe ya Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Jumanne iliyopita tuliona Samatta akisema anafikiria kuoa mwanamke wa Kizungu iwapo atafanikiwa kucheza soka Ulaya.
Sasa endelea

Napata hamu ya kumwuliza Mbwana Samatta kuhusu Tresor Mputu, mtu ambaye inaonekana ufalme wake kwa TP Mazembe unakwisha na badala yake kila mtu anamzungumzia Samatta kwa sasa.

Inasemekana kwamba hata tajiri wa timu, Moise Katumbi ana mapenzi makubwa zaidi kwa Samatta akimpigia simu mara kwa mara. Inasemekana kitu hiki kimekuwa kikifanya Mputu awe na wivu kwa sababu mtu pekee aliyekuwa karibu zaidi na Katumbi ni yeye Mputu na si mtu mwingine kama sasa.

Katika pambano kati ya Mazembe dhidi ya Chelsea Berekum lililopigwa Lubumbashi, Samatta alipika bao la kwanza kwa Mputu baada ya kuwalamba chenga walinzi wawili wa Berekum na kutoa pasi maridadi kwa Mputu aliyefunga.

Hata hivyo, tofauti na ilivyo kwa wanasoka wengi wa kulipwa, Mputu hakumfuata Samatta kwenda kushangilia na badala yake alikimbilia kwingine kwenda kushangilia, kitu ambacho kiliwachukiza mashabiki wengi wa soka.

Lakini katika pambano dhidi ya Zamalek lililochezwa Lubumbashi namshuhudia Samatta akifunga bao kufuatia mpira wa adhabu wa Mputu na Samatta anakimbilia kwenda kumkumbatia Mputu.

Namwuliza Samatta kuhusu hili, pia kuhusu uhusiano wake na Mputu. Samatta anakuwa makini na mwanadiplomasia zaidi kuhusu jambo hilo.

�Sina tatizo lolote na Tresor yeye ndiye mfalme hapa. Tresor ndivyo alivyo tu. Inabidi umkubali kama alivyo kwamba yeye ni mfalme hapa. Ukishakubali hilo wala hutapata shida ya kuishi naye. Mimi sina tatizo naye, ni mtu wangu, anasema Samatta.

Achilia mbali Samatta, mashabiki wa Mazembe kuhisi kwamba Mputu anawaonea wivu mastaa. wengine wawili wa Zambia Rainford Kalaba na Given Sunguluma.

�Mimi kaka sijaona kitu kama hicho. Mashabiki ndio wanatutazama kwa nje labda wao wanaweza kuhisi kitu tofauti, lakini sisi tunaocheza uwanjani hatuhisi kitu tofauti. Kuna wakati wanasema Mputu anaweza kukunyima pasi sehemu ya kufunga, sidhani kama ni kweli kwa sababu huwa anatengeneza mabao, sema uwezo wake umepungua kidogo baada ya kutoka kifungoni, anasema Samatta.

Edo Kumwembe katikati akiwa na Mbwana Samatta na Patrick Ochan kwenye hostel ya TP Mazembe

Namwuliza shabiki mmoja anayeitwa Phillipo Kabongo anayeishi jirani na Samatta na anaonekana kulielewa suala hili kwa undani. Lakini analalamika kwamba Tresor ni mtu mwenye maringo mengi tofauti na Samatta.

�Tresor siku zake zinaelekea mwisho, mfalme hapa ni Samatta tu. Tatizo la Tresor ni kujisikia. Ana majivuno sana. Lakini ni jambo la kawaida kwa mchezaji wa nyumbani kujisikia vibaya pindi mgeni anapofanya vizuri zaidi, anasema Kabongo.

Wakati tunatoka katika mazoezi ya Mazembe, kila siku Mputu huwa analiziba kwa makusudi gari la Samatta lisitoke kwa madai kuwa Mfalme huwa anaondoka kwanza kisha wanakuja wafanyakazi wake. Tunalazimika kumsubiri Tresor.

�Nimekwambia Tresor ni mfalme hapa. Si unaona, kila siku anapaki hilo Range Rover lake mbele ya gari langu halafu utamsikia anasema Samatta mimi ndiye mfalme wako hapa lazima niondoke kwanza ndipo uondoke, anasimulia Samatta.

Baada ya muda Mputu anakuja, anamtania Samatta, anajiita mfalme na kisha anaondoka zake. Mputu ananukia fedha. Ana kila dalili ya kujiamini kuwa ni mtu tajiri. Leo atakuja na Range Rover, kesho atakuwa na Nissan Morano na keshokutwa anakuja na Lamborghini.

�Tresor ni tajiri sana, anasema Samatta bila ya kuficha. Huyu jamaa ana pesa sana, anamiliki vitu vingi sana. Ameingia hadi katika biashara za Moise Katumbi. Ana magari yake makubwa, ana majumba yake hapa na ana kila kitu, ndiyo maana hakutaka kucheza Ulaya.

Hili suala la Mputu kutotamani kucheza Ulaya ndilo ambalo linanifanya nigutuke kumwuliza Samatta, vipi na yeye katika hali kama hii kama amebakiwa na ndoto za kucheza Ulaya kitu ambacho mashabiki wengi wa Tanzania wanakisubiri kwa hamu.

Anapendwa na watu wengi Lubumbashi, anapendwa na tajiri wa timu Moise Katumbi. anaendesha magari ya kifahari, anamiliki nyumba mbili. Inaonekana kama ndoto zake zimetimia. Namwuliza Samatta kama ndoto zake za kucheza Ulaya katika timu kubwa kama zipo. Samatta anajibu bila ya kusita.

Je Samatta anasema nini kuhusu ndoto zake za kucheza Ulaya? Bado zipo? Tajiri Katumbi amesema nini kuhusu ndoto za Samatta kucheza Ulaya? Fuatilia simulizi hii ya maisha ya Samatta TP Mazembe katika sehemu ya mwisho toleo la Jumanne.


Source:Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment