Search This Blog

Tuesday, July 10, 2012

TAARIFA KUTOKA TFF!

TEMEKE YAINGIA NUSU FAINALI COPA COCA-COLA 2012
Temeke imekuwa timu ya kwanza kupata tiketi ya kucheza nusu fainali kwenye michuano ya mwaka huu ya Copa Coca-Cola baada ya kuing’oa Mjini Magharibi kwa mikwaju ya penalti.

Mechi hiyo ya kwanza ya robo fainali imechezwa leo asubuhi (Julai 10 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ambapo hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.

Mjini Magharibi ndiyo walioanza kupata bao dakika ya 79 lililofungwa na Salum Maulid wakati Abdul Hassan aliisawazishia Temeke dakika ya 90.

Waliofunga penalti kwa upande wa Temeke ni Baraka Ntalukundo, Khalid Mwendakamo, Mohamed Dikougwa na Abdul Hassan wakati aliyekosa ni Anwar Kilemile. Waliokosa kwa Mjini Magharibi ni Abdulrahman Mohamed na Salum Maulid wakati waliofunga ni Alawi Kombo na Salum Shukuru.

Katika nusu fainali, Temeke itacheza na mshindi wa mechi ya robo fainali kati ya Kinondoni na Mwanza itakayochezwa kesho asubuhi (Julai 11 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Robo fainali ya pili ya michuano hiyo kati ya Mara na Morogoro ilitarajiwa kuchezwa leo jioni kwenye uwanja huo huo. Mechi nyingine ya robo fainali itakayowakutanisha Dodoma na Tanga itachezwa kesho jioni.

EL SALAM WAU, ATLETICO ZAWASILI KUWANIA KOMBE LA KAGAME
El Salam Wau ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi zinatarajiwa kuwa timu za kwanza kuwasili nchini kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

Michuano hiyo inaanza kutimua vumbi Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikishirikisha timu kumi na moja akiwemo bingwa mtetezi Yanga na makamu bingwa Simba.

Kikosi cha El Salam Wau ambacho kitawasili kesho alfajiri (Julai 11 mwaka huu) kwa ndege ya Ethiopia Airlines kikitokea Juba kupitia Addis Ababa, Ethiopia kikiwa na wachezaji 18 na viongozi saba.

Wachezaji wanaounda kikosi hicho ni Khamis Leone Uso Wani (nahodha), Adheil Bugwic Jongkor Bugwic, Edward Joram Simon Julio, Fidel Andrea Fides Fas, Ismael Musa Juma Ismael, James Anei Matheli Anei, Jervas Ayo Abdalla Ayak, Khamis Doshama Ulama Andel na Meki Sultan Berema Kuku.

Wengine ni Moga Emmanuel Androga, Mubarak Mohammed Saleh Omer, Ndili Rabeh Nasir Hozi, Nizir Rihan Taban Talib, Oliver Paul Kangi Akok, Rabie Mohammed Abubakar Hassan, Rufino Joseph Uras Ambros, Santino Makuei Uyu Upio, Thomas Rufino Thomas Diakon.

Nayo Atletico inatarajiwa kuwasili kesho (Julai 11 mwaka huu) kwa usafiri wa barabara. Timu hiyo inakuja kwa usafiri wa basi lake ambalo pia italitumia kwa muda wote itakapokuwa kwenye mashindano.

Wakati El Salam Wau itafikia kwenye hoteli ya Rungwe iliyoko maeneo ya Kariakoo, Atletico itakuwa Lunch Time Hotel iliyoko Mabibo.

Timu zinazotarajiwa kuwasili keshokutwa (Julai 12 mwaka huu) ni Mafunzo ya Zanzibar kwa boti saa 9 alasiri, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) itatua saa 1.20 usiku kwa Kenya Airways. Timu nyingine itakayowasili siku hiyo jioni ni URA ya Uganda.

WATANGAZAJI KWA ‘SCREEN’ KUBWA KOMBE LA KAGAME
Wakati wa michuano ya Kombe la Kagame itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Julai 14-28 mwaka huu, screen kubwa iliyoko uwanjani itatumika kwa matangazo ya biashara na ujumbe mbalimbali kwa washabiki watakaoshuhudia mechi hizo.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linakaribisha kampuni na wadau mbalimbali wanaotaka kuweka matangazo yao wakati wa michuano hiyo itakayoshirikisha klabu kumi na moja kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Muda wa kurushwa matangazo hayo yanayotakiwa kuwa kwenye mfumo wa DVD ni kabla ya mechi kuanza, wakati wa mapumziko na baada ya mechi. Matangazo hayo yanatakiwa kuwa ya sekunde 60 (dakika moja) au sekunde 30 (nusu dakika).

RAMBIRAMBI MSIBA WA MWENYEKITI FAM
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Fabian Samo kilichotokea leo asubuhi (Julai 10 mwaka huu).

Samo ambaye Novemba 13 mwaka jana alichaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa FAM katika uchaguzi uliofanyika wilayani Rorya alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam akisumbuliwa na maradhi ya figo.

Taratibu za mazishi ya Samo ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu (Internal Audit Committee) ya TFF ikiwemo siku atakayozikwa bado zinafanywa na familia yake.

Samo alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla, vitu ambavyo vilichangia kuchaguliwa kwake tena kuiongoza FAM.

Msiba huo ni pigo kwa familia ya Samo, FAM, TFF na mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango na mawazo aliyotoa kwa kipindi chote alichokuwa kiongozi.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Samo, FAM, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Mungu aiweke roho ya marehemu Samo mahali pema peponi. Amina

KOZI YA MAKOCHA WA GRASSROOTS
Kozi ya makocha wa mpango wa grassroots unaolenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12 imeanza leo (Julai 10 mwaka huu) kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam.

Wakufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ndiyo wanaoendesha kozi hiyo iliyofunguliwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah.

Kozi hiyo itakayomalizika Julai 15 mwaka huu inashirikisha washiriki 35, na mwendelezo wa ile ya awali iliyofanyika Desemba 14-17 mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Gouinden Thandoo kutoka Mauritius ni mmoja wa wakufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wanaoendesha kozi hiyo.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 

No comments:

Post a Comment