TIMU ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17, Ngorongoro Heroes, jana kwa mara ya pili ilishindwa kutamba mbele ya vijana wenzao wa Rwanda baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo wao kwanza Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji, Heroes pia ilichapwa mabao 2-0.
Timu ya Rwanda |
Vijana hao wa Tanzania wanajiandaa kwa mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika kwa Vijana mwaka 2013 dhidi ya Nigeria baadaye mwezi huu.
Vijana wa Rwanda walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Ngorongoro na kujipatia bao la kuongoza dakika ya pili kupitia kwa Nsimiyiman Imran aliyeunganisha wavuni pasi ya Kabanda Boifil.
Heroes ikiwa na Frank Domayo, Omega Same, Saimon Msuva na Ramadhan Singano walitawala kwa kiasi kikubwa sehemu ya kiungo.
Ikicheza mbele ya mashabiki wachache waliojitokeza uwanjani, Heroes ilisawazisha bao hilo dakika ya 30 kwa mkwaju wa penalti uliosababishwa na Umwengeri Patrick kumchezea vibaya Singano.
Kiki hiyo ya penalti ilikwamishwa vizuri kwenye kamba na mchezaji Atepele Green na kuzifanya timu hizo kumaliza nusu ya kwanza zikitoshana nguvu ya bao 1-1.
Vijana wa Rwanda, kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza kufunga bao la haraka, ndivyo walivyofanya kipindi cha pili ambapo iliwachukua dakika nane kufunga bao la pili.
Bao hilo lilifungwa na Nsimiyimana Imran aliyetumia vizuri fursa kuchelewa kujipanga kwa mabeki wa Heroes na kuujaza mpira wavuni akimalizia pasi ya Tibingana Charles.
Baada ya bao hilo, Rwanda walichukuwa utawala wa mchezo na kufanya mashambulizi jinsi walivyotaka kwenye lango la Heroes.
Wenyeji walizinduka katika dakika ya 71 baada ya kufanya shambulizi kubwa langoni mwa Rwanda lililoishia kwa shuti kali la Domayo kupanguliwa na mlinda mlango Rafael Stevin.
Kocha Msaidizi wa Heroes, Adolph Richard alikiri kipigo hico, lakini akasema kimewapa mazoezi ya kutosha na kufanya marekebisho kabla ya mcehzo dhidi ya Nigeria.
News courtesy of Mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment