Search This Blog

Wednesday, July 4, 2012

Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’-EPISODE 8

jjjjjj

*Yanga yaanza michuano kwa kichapo, kocha alia kama mtoto
*Gulamali, Francis Kifukwe watua Kampala, wamwaga fedha

Na Saleh Ally

WIKI ILIYOPITA, Malima wakiwa na Yanga walitua Kampala, Uganda kwa ajili ya kushiriki michuano ya Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati. Lakini walikwenda kwa kuungaunga, hawakuwa na posho na maisha yalikuwa magumu sana. Je, mambo yataendaje? Endelea.
TULIPOWASILI tukakuta ratiba imeshatoka, tulikuwa tumepangwa kundi moja na Rayon Sports ya Rwanda na Red Sea ya Djibouti. Ilionyesha tunatakiwa kuanza na Rayon.
Nikakumbuka siku chache zilizopita, tuliwatoa Rayon kwenye michuano ya Afrika. Tukasonga mbele kwa sare ya mabao 1-1, CCM Kirumba, Mwanza. Kwa hiyo tukajua mechi itakuwa ngumu lakini tukajipanga tayari kwa vita.
Tukaingia uwanjani na kucheza kwa kujituma sana, wakati huo ilikuwa ni siku chache baada ya kumpata kocha mpya, huyo ni Raoul Shungu raia wa DRC. Alikuwa kocha wa Rayon kabla ya kuja Yanga kuchukua mikoba ya Tito Mwaluvanda.
Mechi iliishika tukiwa tumepigwa mabao 3-0, hali ilikuwa mbaya na hatukuamini. Wote tulikuwa katika hali ya majonzi lakini Shungu ndiye alionekana kuchanganyikiwa zaidi baada ya kufungwa na timu yake ya zamani.
Baada ya kufika hotelini, kila mmoja akionekana kuwa hoi, Shungu aliingia chumbani na kujifungia. Alilia sana, alilia tena kwa sauti na tukawa tunaelezana kuwa kocha alikuwa akilia.
 Hali hiyo ilitufanya tuone tuna kazi mbele na tunaiweza, kwa kuwa mechi yetu iliisha saa kumi kasoro jioni, na tukawahi kufika hoteli. Wakati huo huo tukaamua kwenda mazoezini.
Tuliona haikuwa sahihi kufungwa, tulijua tulikuwa na njaa lakini tuliamini tunaweza kufanya vizuri. Wachezaji wachache nikiwemo mimi ndiyo hatukwenda mazoezini kwa kuwa ulikuwa ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Wenzetu walipotoka mazoezini, walitukuta tunamaliza kikao chetu ambacho tulikifanya baada ya kufuturu. Tukawambia nasi tuliamua kuacha kufunga kwa kuwa dini inaruhusu, kama kuna kitu muhimu unaweza ukalipa baadaye.
Waliungana nasi na kwa pamoja tukasema tumepania kushinda mechi inayofuatia. Lakini siku iliyofuata tukaambiwa ile timu ya Djibouti ilikuwa imejitoa kwenye michuano.
Maana yake tulibaki sisi na Rayon na pamoja na kufungwa ilikuwa lazima tucheze tena ili kupata timu itakayokuwa ya kwanza na ya pili kwa ajili ya robo fainali ya michuano hiyo.
Rayon walionyesha kufurahia, waliona ingekuwa lahisi tu. Mechi kweli ilikuwa ngumu sana na tulicheza kwa kujituma sana. Mwisho tukaibuka na ushindi wa mabao 3-0. Nakumbuka wafungaji walikuwa Kally Ongala aliyefunga mawili na Iddi Moshi ‘Mywamwezi’.
Rayon hawakuamini kama sisi ndiyo walitufunga tatu mechi ya kwanza. Baada ya hapo, tukawa tumelingana kila kitu, maana yake ikabidi irushwe shilingi ili kupata kiongozi wa kundi na wenzetu Rayon wakashinda na wao wakawa viongozi wa kundi.
Kwa nafasi yetu ya pili ya kundi, mechi ya robo fainali tukapangiwa kucheza na timu ngumu ya Al Hilal ya Sudan. Huku nyumbani kila mmoja akajua safari imetukuta kutokana na hali halisi.

Al Hilal ni moja ya timu kubwa barani Afrika na wanaishi maisha mazuri na yenye mpangilio ukilinganisha nasi. Lakini kambini sisi hatukuwa hata na hofu. Tulikuwa tayari kwa vita kwa ajili ya kuipigania Yanga.
Binafsi niliona tulishapata moto, hivyo hakuna timu ambayo ingeweza kututisha na kawaida tulipokuwa tunaingia uwanjani tulisahau kila kitu. Tulimhakikishia kocha kuwa Wasudani watakiona cha mtema kuni.

Mechi ya robo fainali ilikuwa ngumu, jamaa walikuwa wako sawa, walipiga pasi na kumiliki mpira za uhakika na ikaonekana wana mashabiki wengi pale Kampala, labda kutokana na kwamba Wasudani wengi wanaishi pale.
Pamoja na mapenzi yetu kwa Yanga na kazi yetu, wachezaji wote tulijua kama tutafanikiwa kushinda mechi za michuano ile, huduma itakuwa nzuri na kuepukana na maisha ya shida tulikuwa tukiishi. Hivyo tuliendelea kupambana kwa nguvu.
Sisi hatukujali hata kidogo uzuri wa Wasudani na jamaa walipata bao. Lakini Salvatory Edward alisawazisha na ngoma ikawa droo. Bado tuliendelea kupamba na kitu kizuri kwetu tulikuwa na pumzi ya kutosha.
Kadiri muda unavyozidi kuyoyoma, kasi yetu ilizi kupanda na kuzidi kuwapa jamaa wakati mgumu. Dakika ya 90 tukapata penalti. Ilikuwa ni wazi na jamaa wala hawakulalamika, tukampa mtu ambaye tunajua hawezi kufanya mzaha, alikuwa ni Edibily Jonas Lunyamila na hakufanya ajizi. Akaikwamisha wavuni. Tukasonga nusu fainali.
Ushindi dhidi ya Al Hilal, ulifanya baadhi ya viongozi wafunge safari kuja Kampala. Nakumbuka Francis Kifukwe akiongozana na Abbas Gulamali walitua hotelini kwetu. Ilikuwa furaha maana walimwaga fedha, kila mchezaji alipewa dola 200, kwetu ilikuwa ni kama milioni tano kutokana na ukata tuliokuwa nao.

TAYARI wachezaji wa Yanga, akiwemo Malima wamelamba fedha kutoka kwa Gulamali na Kifukwe. Je, nusu fainali watakutana na nani na itakuwaje” USIKOSE MUENDELEZO WA HEKAHEKA ZA MAISHA YA SOKA YA MALIMA

4 comments:

  1. Kaka Shaffih, this is very interesting story....please usiiweke kimya xanaaaa... baada ya siku tatu au nne..weka mzigo tupate raha zetu bhanaa.....Lovely
    Bocco wa Tanga.

    ReplyDelete
  2. Kwa kweli YANGA hawana busara hata kidogo walicho kifanya cjakifurahia

    ReplyDelete
  3. Mheshimiwa Shaffih Dauda....tafadhali sana sana endeleza huu mzigo wa stori tamu sana ya Malima(Jembe Ulaya) lini itaendelea maana ni utamu usiokuwa na mwisho...

    ReplyDelete
  4. Very very interesting. Inanikumbusha mbali sana.Nakumbuka ilikuwa ni kipindi cha mfungo na matokeo yetu ya form four yalikuwa yamefutwa nchi nzima.

    ReplyDelete