Na Arone Mpanduka(Radio Tumaini)
NDANI ya msimu wa mwaka 2011/2012 tumekuwa tukishuhudia matukio mbalimbali ya kimichezo hasa katika medani ya soka ambayo yamekuwa yakivutia na kusisimua.
Kutokana na kufuatilia kwa karibu zaidi matukio ya soka Barani Ulaya kupitia ligi mbalimbali nimeweza kubaini mambo kadhaa ambayo yamekuwa kinyume na matarajio ya wapenzi wengi wa mchezo wa soka duniani.
Kupitia matukio hayo wengi waliokuwa wanajaribu kutabiri ndivyo, matokeo yake yamekuwa sivyo.Fuatana nami ili tuweze kwenda pamoja hasa kwa kupitia tukio moja hadi lingine kwa kifupi.
BINGWA WA KOMBE LA FA
Hapa wengi walidondosha karata yao ya utabiri kwa timu ya Liverpool hasa kutokana na wachezaji wake kuwa na tabia ya kutokata tamaa katika dakika zote 90 hata kama wakiwa nyuma kwa goli moja ama mawili kitu ambacho wachezaji wa Chelsea wamekikosa.
Licha ya kwamba timu zote zilikuwa na mwenendo mbovu katika msimu wa 2011/2012 lakini Liverpool ilipewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa kombe hili lakini hatimaye mambo yalikuwa kinyume hasa pale ambapo Chelsea ilipofanya maajabu kwa kuinyuka Liver mabao 2-1.
Ramires na Didier Drogba ndiyo waliofanikisha kombe la FA kwenda darajani ambapo kwa mara ya mwisho Chelsea ilitwaa kombe hilo mwaka 2010.
BINGWA WA LIGI KUU YA HISPANIA
Katika ligi hii wengi walikuwa wakiiangalia zaidi Barcelona ambayo ilikuwa ikishiriki ligi kama bingwa mtetezi lakini pia bingwa wa dunia ngazi ya vilabu.
Watu walikuwa na imani na Barcelona hasa kwa uimara iliyonao wa kuweza kumiliki mpira na kupenyezeana pasi za uhakika na hata pia umakini wa washambuliaji wake kama Lionel Messi ambaye ni mgumu kumzuia pindi anaposogelea ‘sebule’ ya timu pinzani.
Hadi ngwe ya mechi za marudiano za ligi kuu ya Hispania inaanza Barcelona ilikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi ikifuatiwa na Real Madrid lakini mambo yalibadilika kuelekea mwishoni mwa ligi ambapo Madrid chini ya Jose Mourinho ikafanikiwa kuitangulia Barcelona kwa tofauti ya pointi 4.
Mambo yalizidi kwenda hivyo hasa kwa timu zote kuhakikisha kwamba hazifanyi makosa kwenye mechi zao na kufanya mashabiki wa soka ulimwenguni kusema kwamba bado Barcelona ana nafasi ya ubingwa hasa katika mechi ambayo wanacheza mwenyewe kwa wenyewe hasa ikizingatiwa kwamba mara zote Madrid ni kibonde wa Barcelona.
Lakini mambo hayakuwa mambo kwani hata walipokutana wenyewe kwa wenyewe Barcelona alikubali kichapo kutoka kwa Real Madrid mara baada ya kupigwa 2-1 na kutengeneza tofauti ya pointi 7 kutoka 4, tofauti ambayoi ilikwenda hadi siku ambayo Real Madrid inatangaza ubingwa.
Hapa ndugu msomaji hadi mwisho wa ligi ubingwa wa Real Madrid ulikuwa kinyume na matarajio ya wengi.
BINGWA WA LIGI KUU YA UINGEREZA
Katika ligi hii inayodhaminiwa na benki kubwa duniani ya Backlays tangu inaanza mwezi Agosti mwaka 2011 mashabiki wengi walikwishaipatia ubingwa timu ya Manchester United hasa baada ya kuanza vizuri msimu kwa kuinyuka Manchester City 3-2 katika mechi ya ngao ya jamii.
Kama hiyo haitoshi Manchester United ilionyesha kwamba ipo vizuri baada ya kutoa vipigo kwa timu kadhaa ikiwemo kipigo cha kihistoria ya mabao 8-1 ilichomnyuka Arsenal na kuweka rekodi ya ushindi wa mabao mengi zaidi katika msimu huo wa ligi kuu.
Kumbe wakati huohuo timu iitwayo Manchester City ilikuwa inakimbiza mwizi kimya kimya hasa baada ya kuonyesha ushindani wa hali ya juu kwa kutoa dozi kwa timu ilizokuwa inakutana nazo.
Hadi kufikia mwezi Januari mwaka 2012 Manchester City walikuwa wanaongoza ligi wakifuatiwa na Manchester United kitu ambacho kilihamisha mawazo ya wadau wa soka kutoka kwa United hadi City na kusema kwamba City ndiyo bingwa mtarajiwa.
Lakini mwishoni mwa ligi hiyo mambo yalibadilika ambapo wadau wakarejesha utabiri wao kwa Manchester United kuwa ndiye bingwa wa ligi hiyo hasa baada ya timu hizo kuwa na pointi sawa huku City ikiwa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa tu.
Utamu ulikuja katika siku ya mwisho ya kumaliza ligi ambapo bingwa alikuwa bado hafahamiki na watu wengi walitabiri kwamba Manchester United atamfunga Sunderland lakini wakiibeza City kwamba isingeweza kuifunga QPR ambayo nayo ilihitaji ushindi ili isishuke daraja.
Hali hiyo ilifanya siku hiyo hata helikopta iliyobeba kombe kuhangaishwa angani ambapo kila dakika ilikuwa inabadili njia zake, mara iende Sunderland mara ibadilike na kwenda Etihad.
Lakini mwisho wa yote Manchester City nayo iliibuka na ushindi wa mshangao wa mabao 3-2 ikitoka nyuma ya mabao 2-1 dhidi ya QPR huku Manchester United ambayo iliiombea City ifungwe ili yenyewe ichukue ubingwa ikajikuta ikipoteza ndoto hiyo licha ya yenyewe kushinda bao 1-0.
Mwisho wa yote Manchester City aliibuka bingwa kiyume na matarajio ya wengi ulimwenguni.
BINGWA WA KLABU BINGWA BARANI ULAYA
Hapa timu za Bayern Munich na Chelsea hazikupewa nafasi kabisa ya kufika hata nusu fainali lakini matokeo yake miamba hiyo ilitinga fainali na kuchuana pale Allianz Arena nchini Ujerumani.
Utabiri ulianza kushika kasi katika hatua ya 16 bora ambao kwa mtazamo wa haraka haraka mashabiki wengi duniani walihisi kwamba fainali itazikutanisha timu za Real Madrid na Barcelona na hapo yoyote kati ya hizo ndiye atakayekuwa bingwa.
Kinyume chake ni kwamba Real Madrid alibwagwa na Bayern Munich katika hatua ya nusu fainali huku Barcelona akibwagwa na kibonde Chelsea katika hatua ya nusu fainali, kitu ambacho kiliwashangaza wengi hasa kwa hali iliyonayo Chelsea kuweza kuiondosha miamba ya dunia Barcelona ambayo ilikuwa na kila sababu ya kufika fainali na kutwaa taji hilo.
Mechi ya fainali kati ya Bayern Munich na Chelsea nayo iliibua watabiri wengi walioegemea upande wa Bayern kwamba ndiyo wangekuwa mabingwa hasa kutokana na sababu nyingi ikiwemo tofauti ya uwezo wa kuuchezea mpira na kasi ya ushambulizi kwa timu hizo ambapo wajerumani waliizidi Chelsea.
Suala lingine ni kitendo cha Bayern kucheza nyumbani , mahali ambapo pana watu wengi wa kuiunga mkono pindi iwapo dimbani.
Matokeo ya mwisho yalikuwa ndivyo sivyo kwani Chelsea iliibuka na ushindi wa penati 4-3 hasa baada ya kutoka sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 za mchezo.
Barua Pepe:mpanduka@yahoo.com
mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.mpira ni dakika 90 na matokeo ya ushindi sio mpira kuchezea mdomoni.chelsea walistahili kwakua walifocus kwenye ushindi wa dakika 90 nasio possession kuwafurahisha watazamaji kwenye majukwaa na mbinu yao imefanikiwa. wakati timu nyingine zilifocus kwenye ball possession.chelsea walicheza michuano ya champions ligue kwa malengo.
ReplyDeleteH.sato
Chelsea wanajua mbinu
ReplyDelete