Search This Blog

Wednesday, May 23, 2012

SIMBA NA APR WAAMUA KUICHANGIA FAMILIA YA MAREHEMU PATRICK MAFISANGO


KLABU ya APR FC na Shirikisho la Soka la Rwanda(Ferwafa), wameandaa mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba kwa lengo la kupata fedha za kuchangia watoto na familia ya Marehemu Patrick Mafisango.

Mafisango aliyezikwa Jumapili eneo la Kinkole, nje ya Jiji la Kinshasa baada ya kufariki kwa ajali ya gari Dar es Salaam, ameacha watoto wadogo watatu, wanaume wawili Crespo na David pamoja na binti Patrina.

Hali ya familia mchezaji huyo ambae hana wazazi na alilelewa na shemeji yake Papaa Pierre tangu akiwa mdogo, si nzuri kiuchumi ingawa waligharamia sehemu kubwa ya mazishi ya ndugu yao.

Makamu Mwenyekiti wa Ferwafa, Raoul Gisanura na Katibu Mkuu wa APR, Adolphe Kalisa wameiambia Mwananchi msibani jijini Kinshasa kwamba wako tayari kucheza mechi hiyo muda wowote kabla ya kuanza kwa kombe la Kagame mwezi ujao.

Gisanura alisema; "Ni jambo zuri sana kuichangia hii familia ili hawa watoto wafaidi matunda ya baba yao na waende shule, kwavile hali halisi inaonyesha kwamba ni mzigo mkubwa kwa familia iliyoachwa pamoja na mama zao."

Kalisa alisema; "Simba na APR zimefaidika sana na Mafisango kuliko watu wa Kinshasa hivyo ni wajibu wetu kufanya kitu kama fadhila kusaidia hii familia, sisi tuko tayari kucheza na Simba lakini ingekuwa vizuri zaidi hiyo mechi ikaandaliwa na kampuni huyu ambayo si klabu hizo mbili wala Shirikisho."

Mwakilishi wa Simba aliyekuwa jijini hapa, Joseph Itang'are 'Mzee Kinesi'  alipoambiwa na Mwananchi kuhusiana na hilo alisema halina matatizo kwani ni kiasi cha kujadiliana tu na kuweka mambo kwenye mpango na akaahidi kufikisha kwa uongozi wa juu. 

source: www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment