Chairman wa Yanga anayeandamwa na shinikizo la kutakiwa kujiuzulu,
Lloyd Nchunga amewaponda baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji
waliojiondoa na kusema uamuzi wao siyo dawa ya suluhu ya mgogoro uliopo,
na kwamba katiba ya klabu hiyo inampa mamlaka ya kuteua wengine kuziba
nafasi hizo.
Nchunga ambaye amekuwa gumzo kwenye vyombo vya
habari kutokana kung'ang'ania kwenye mstari wa kukataa kuachia ngazi,
amesema katiba ya Yanga inatoa mamlaka ya kuchagua watu wengine kuziba
nafasi za wajumbe wa kuchaguliwa waliojiuzulu, na tayari amefanya hivyo.
"Kipengele
cha 29, ibara ya (3) ya Katiba ya Yanga, kinaruhusu kuteuliwa kwa watu
wa kuziba nafasi za wajumbe wa kuchaguliwa wa Kamati ya Utendaji
waliojiuzulu," alisema kwa kujiamini Nchunga.
Aliongeza:
"Kutokana na uteuzi huo wa watu wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na
wajumbe wa kuchaguliwa waliojiuzulu, hakutafanyika uchaguzi mdogo.
Wateule wapya tumeshawaandikia barua za kuwafahamisha.
Nchunga
alisema kamati ya utendaji itawatangaza wajumbe wapya mwishoni mwa wiki
hii na kuongeza: "Waliodhani kwamba kujiuzulu kwao kamati ya utendaji
kungeweza kuwa kiini cha mimi pia kujiuzulu, watakuwa wameingia mlango
siyo sahihi."
Alisema amegundua baadhi ya wajumbe kwenye kamati
hiyo hawana msimamo na ndiyo hao ambao wamekuwa wakimshinikiza yeye
kujiuzulu bila kufahamu kwamba uamuzi huo hauwezi kuwa suluhu ya
mgogoro.
Amemtaja mjumbe aliyejiuzulu hivi karibuni, Mohamed
Bhinda kuwa ni mmoja ya watu vigeugeu na waliokosa msimamo kutokana na
kutoa kauli zisizo sahihi na zenye lengo la kupotosha ukweli.
Juzi,
Bhinda alikaririwa na chombo kimoja cha habari akisema kikao cha kamati ya
utendaji cha Yanga kilichokutana hoteli ya Protea ilimtaka Nchunga
ajiuzulu kwa faida ya Yanga kwa vile mzani unaonyesha ndiye chanzo cha
mgogoro wa Yanga.
Bhina alikwenda mbali zaidi na kusema,
mwenyekiti wake baada ya kubanwa alikubali kujiuzulu muda wowote, lakini
Nchunga alipinga kauli hiyo na kusema hakuna kikao kilichoitiswa
akakubali kuachia ngazi.
"Bhinda ni dhaifu, kwanza aliyoyasema
siyo tuliyoyazungumza, anatumika tu lakini ajue kutumika kwake
anajidhalilisha, kamati ya utendaji tunakaa tena hivi karibuni
tutamjadili na kumchukulia hatua kali za kinidhamu," alisema Nchunga.
Bosi
Nchunga alitumia fursa ya kuzungumzia hali ilivyo Yanga kwa kuwaonya
wazee wa klabu hiyo kwa kusema, angependa kuona mgogoro wa uliopo
unaisha katika njia ya amani tofauti na hali inavyoonekana sasa.
"Hao
wazee kama wameshindwa kunipindua kikatiba watulie, wasinione nimekaa
kimya wakaniona mjinga, nawaheshimu ndiyo maana nimekaa kimya. Kama
wanataka tuchafuane, mimi pia naweza kufanya hivyo.
"Ninawaheshimu
wazee hawa, nisingependa kuingia nao kwenye matatizo, nawafahamu wote
na kila mmoja anavyoishi. Nawaomba wapokee heshima yangu,
wasinilazimishe kuivunja," alisema.
Kuhusu kuimarika shinikizo la
kutakiwa kujiuzulu, Nchunga alisema: "Msimamo wangu uko wazi,
nilishasema na narudia tena, haipo sababu ya kujiuzulu kwa shinikizo la
wachache, lakini kama binadamu nitaeleza kila kitu Ijumaa."
No comments:
Post a Comment