Search This Blog

Tuesday, April 10, 2012

Tumejifunza nini kutokana na mafanikio ya Simba dhidi ya Setif.

Katika hali ya kawaida kabisa Simba walipoteza mchezo wao wa marudiano dhidi ya Es Setif , tena kwa matokeo mabaya sana ya kuruhusu mabao matatu ambayo hayawezi kumfurahisha kocha au mchezaji au hata shabiki yoyote yule ambaye anahusika na klabu yake .
Hata hivyo lazima tukiri ukweli kuwa katika michezo miwili Simba ilipata matokeo mazuri na ndio maana wamefanikiwa kufuzu kuingia raundi inayofuata ya michuano hii. Kwa sababu hii hatuna budi kutoa sifa pale sifa inapostahili na kiukweli kabisa Simba wanastaili pongezi kwa kuwatoa Setif.
Pamoja na sifa hizo lazima turudi nyuma na kujiuliza nini siri ya mafanikio ya Simba  na baada ya kujiuliza huko lazima tujifunze kutokana na mafanikio ya Simba hasa kwenye mchezo wao mwisho dhidi ya Setif.
Kikubwa kilichowasaidia Simba ni matokeo mazuri kwenye mchezo wa kwanza ambao kwa Simba ulikuwa mchezo wa nyumbani. Kwenye mchezo wa kwanza Simba walishinda kwa mabao mawili bila na ndio maana pamoja na kupoteza mchezo wa marudiano , bao moja la ugenini lilitosha kuwapa matokeo ya kuwatoa Setif pamoja na ukweli kuwa matokeo ya jumla yalikuwa sare .
Moja ya vitu ambavyo vimekuwa vikizitatiza timu za Tanzania ni kutofanya vizuri hasa kwenye mchezo wa nyumbani. Ukirudi nyuma na kutazama mchezo wa Yanga dhidi ya Zamalek wiki chache zilizopita utagundua ukweli wa hoja hii . Hebu jiulize kama Yanga wangeshinda mchezo ule ambao uliisha kwa sare ya 1-1 labda kwa matokeo kama ya 2-0 au 3-0 au 3-1 ? Jibu ni moja tu kuwa hunda yanga wangekuwemo kwenye mashindano hii leo kwa kuwa Nyumbani Zamalek walishinda kwa bao moja  pekee. Hata timu ya taifa imekuwa na tatizo hilo hilo la kufanya vibaya nyumbani . Mfano angalia mara ya mwisho kwenye mchezo wa hatua za awali kufuzu kwa kombe la mataifaya afrika dhidi ya Msumbiji , sina lengo la kusema kuwa Taifa Stars itatolewa lakini siku zote unapotoka sare ya 1-1 au unaporuhusu bao la ugenini unajiweka kwenye mazingira magumu sana ya kusonga kwenye raundi inayofuata .
Kikubwa kilichowapa simba faida ni mchezo wa nyumbani ambao endapo time za kitanzania zitajifunza kuuchukuliakwa umakini matokeo kama ya Simba yataendelea kuwepo , hata kwenye mchezo unaofuata ambao Simba  watacheza na Al Aly Shandy wanapaswa kurudia kile walichokifanya kwenye mchezo dhidi ya Setif ambao siri ya ushindi ilikuwa mchezo wa nyumbani.
Zaidi ya hapo lazima usifu moyo wa kishujaa ulioonyeshwa na wachezaji wa Simba . Tunaweza kuzungumzia ushindi wa nyumbani tunavyotaka lakini bado bao moja la ugenini lililofungwa na Emmanuel Okwi limechangia asilimia hamsini ya ushindi wa Simba . Bao hili limekuja kutokana na juhudi binafsi za Okwi ambaye mara nyingi hufunga mabao ya aina ile , lakini zaidi ya hapo bao lile lilikuja kutokana na moyo wa kuendelea kupambana waliokuwa nao wachezaji wa simba . Mazingira yalikuwa magumu sana hasa ukizingatia hali ya hewa , na jins ambavyo mchezo ulikuwa unaelekea . Kwa mtu mwingine angeweza kukata tamaa na kuomba tu mechi iishe haraka apunguziwe mateso lakini Simba walipambana kiume na ndio maana wakapata matokeo kama yale. Hili ni fundisho muhimu kuwa mchezo ni dakika tisini na kabla ya filimbi ya mwisho kama mchezaji unapaswa kupambana kufa na kupona .

4 comments:

  1. Mimi niungane mkono na makala yako bwana Shaffih na kweli wachezaji wa Simba wanahitaji pongezi kwa kupigana kiume kabisa kwani haikuwa kazi rahisi binafsi mimi kama mshabiki tu sikuwa naipa tena simba nafasi hasa baada ya wao kuwa nyuma kwa goli 3 mpaka dakika ya 90 na ukizingatia walikuwa pungufu na spidi ya waalgeria, ila spirit ya kutokata tamaa ilipelekea wao kupata matokeo waliyokuw wanayahitaji lakini pia Pongezi za dhati kabisa kwa Okwi kwa goli alilolifunga ni goli ambalo huchoki kulitazama kwa kweli na lilikuwa la uwezo binafsi najua timu nzima inahitaji pongezi kwa team work waliyoionyesha ila Okwi na Kaseja walionyesha tofauti kwa kweli.
    Naamini hilini funzo kwa klabuna hata timu yetu ya Taifa kila suala la kuutumia uwanja wa nyumbani kwa kadiri ya uwezo wako wote ni muhimu sana sitaki kurudia mfano ulizoitoa ila ukishindwa kutumia vema uwanja wa nyumbani kwa kweli unajiweka katika mazingira magumu sana kisoka na hasa soka letu la Afrika ambalo lina fitina nyingi sana tena nyingine za wazi kabisa na bado CAF watapeta kwa hiyo naamini timu zetu zichukulie jambo hilo kama funzo kuruhusu bao unapocheza nyumbani ni hatari kubwa, wale Settif walipoenda kwao nadhani Simba walishangaa jamaa walivyobadilika jamaa walikuwa wanakimbiza hatari tofauti na walipocheza hapo dar.Sina historia sana ya Shandy ya Sudan ila natumai si timu ya kuidharau na Simba bado wana kazi kubwa ya kufanya ili kuitoa timu hiyo naamini hawatabweteka ila watajipanga zaidi.
    Huu ugonjwa wa timu zetu kila mara kuwa uchochoro uishe sasa wenzetu wanaingiza klabu karibu 4 kwenye mashindano ya CAF kwanini isiwe sisi na ndio maana tunasema mafanikio ya simba ni mafanikio ya timu zote za Tanzania kwa ujumla kwani wakifanya vema naamini hata nafasi ya timu za uwakilishi zitaongezeka nimeliona hilo Zimbabwe wana timu 2 kwenye champions league na 2 kwenye confederation.
    Mdau
    Mike.

    ReplyDelete
  2. Maka Patrick MwasomolaApril 10, 2012 at 11:49 PM

    Umesema Shafii!

    ReplyDelete
  3. Shafiih, umetoa somo zuri sana. maana katika mchezo ule hakukuwa na hata dalili ya kuonekana kuwa simba wangepata bao, hasa ukizingatia kuwa Setif walipata mabao ma2 ya haraka haraka katika kipindi cha pili hivyo watu tulikuwa tukitegemea labda simba ingepata matokeo mabaya zaidi. nakumbuka nilikuwa nafuatilia maelezo yenu kupitia kipindi cha michezo, nilimsikia Mbwiga akitoa vijembe vyenye mwelekeo wa kuidharau simba kwamba walizidiwa kwa kiasi kikubwa sana na hivyo Setif hawakupata upinzani wowote kutoka kwa simba, nikiwa mwenye huzuni kubwa usiku ule nilikusikia ukitangaza game na mara nikakusikia ukisema heeey naona okwi anapachika bao hapa,amini usiamnini niliruka kwa shangwe kubwa na kuanza kushangiria kama vile nilipagawa,zikiwa zimebakia dakika 2 mpila kwisha nilikuwa naona kama dakika 20 vile maana wenzetu walikuwa wepesi mno kulikaribia lango la simba mara kwa mara.

    ReplyDelete
  4. Watangazaji watangaze mpira kama inavyotakiwa siyo kuleta ushabiki maana mnaweza kuuwa watu,utaletaje dharua kwa timu nyingine wakati mpira ni dk 90.

    ReplyDelete