Search This Blog

Thursday, April 26, 2012

MCHEZAJI AANGUKA NA KUFARIKI UWANJANI KIGOMA


Matukio ya wachezaji kuanguka na kufa uwanjani yameendelea kuuandama mchezo wa soka ambapo tukio la hivi karibuni wadau wa soka wamempoteza mchezaji aliyeanguka uwanjani na kufariki muda mfupi akiwa njiani kukimbizwa hospitali tukio ambalo limetokea huko kijiji cha Nyakitonto wilayani Kasulu mkoani Kigoma
Mchezaji Menanyamala Edison mwenye umri wa miaka 28 amekumbwa na umauti wakati akichezea timu ya kijiji chake cha Nyakitonto katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya kijiji cha Mugombe pia ya huko wilayani Kasulu mwishoni mwa wiki iliyopita
Akielezea tukio hilo kocha wa timu ya Nyakitonto Adam Charles maarufu kama “Nyoka wa Nyoka” amesema mchezaji huyo aliingia kama mchezaji wa akiba katika dakika ya sabini ya mchezo huo kuokoa timu yake ambayo ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 lakini ghafla akiwa peke yake bila kuguswa na akiwa hana mpira alidondoka chini
Amesema baada ya kuona kuwa mchezaji huyo hainuki walikwenda kumuangalia na kugundua kuwa alikuwa amezimia na ndipo walimpakiza kwenye pikipiki na kumkimbiza katika kituo cha afya cha Nyakitonto ili kujaribu kunusuru maisha ya mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo lakini walipofika hospitali wakaambiwa kuwa tayari alikuwa amekata roho
Nae kaka wa marehemu Matendo Edison akiongea kwa njia ya simu ambaye tukio hilo limetokea wakati yeye akiwa kanisani amesema alishitushwa na taarifa za kifo cha mdogo wake na kwamba kinatatanisha kwa kuwa mdogo hakuwa na tatizo lolote na aliondoka nyumbani salama akiaga kuwa anakwenda kwenye mechi
Bado haijafahamika ni nini chanzo cha mchezaji huyo kuanguka uwanjani na kufariki muda mfupi baadaye
Akizungumzia tukio hilo afisa michezo wilayani Kasulu bw.Dismas Kalegea amesema hilo ni pigo kubwa sio tu kwa club na familia yake bali hata kwenye halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwani mchango wake ulikuwa unahitajika katika harakati za kuendeleza michezo wilayani humo
Sambamba na hilo amezitaka timu mbali mbali zinapotaka kucheza kupeleka taarifa kwenye vyama au mamlaka za kusimamia  mchezo husika ili pindi linapotokea jambo lolote baya iwe rahisi kutoa msaada.
Sisi wanamichezo tunasema, “Mungu airehemu roho hiyo ya kimichezo na kuiweka mahali pema peponi, Amina”.

Taarifa na mwanamichezo Johnsona Matinde (Valeron), toka Kigoma.

No comments:

Post a Comment