SIKU moja baada ya kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutupilia mbali rufaa ya timu ya Yanga kupinga kupokwa pointi tatu na mabao matatu, uongozi wa klabu hiyo umesema bado unatafakari cha kufanya.
Kamati ya nidhamu chini Mwenyekiti wake kamishna mstaafu wa Polisi Alfred Tibaigana iliyokutana juzi ilitupilia mbali rufani hiyo ya Yanga iliyowasilishwa na Yanga ikilalamikia kamati ya kamati ya Ligi kuipoka pointi hizo na mabao matatu baada ya kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alikuwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi tatu.
Ofisa habari wa Yanga Louis Sendeu alisema jana kwamba wamezipata taarifa za rufaa yao kutupiliwa mbali lakini kwa sasa wanaendelea na mambo mengine kwanza ambayo yana manufaa na klabu hiyo huku wakiliweka kiporo suala hilo.
Alisema kwa sasa viongozi wengi wa klabu hiyo wapo nje ya jiji la Dar es Salaam kwa majukumu tofauti lakini bado kuna nafasi ya kukata rufaa kwa kamati ya Rufaa kama itabidi kuwa hivyo kwa kuwa muda bado upo.
“Tumepata taarifa za rufaa yetu kushindwa, hivyo ni mapema mno kutoa uamuzi tutkaochukua baada ya hatua hiyo, kwa sasa tunaendelea kuchapa kazi kwanza,”alisema Sendeu.
Aprili 2 mwaka huu Kamati ya Ligi ya TFF iliipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha Cannavaro kwenye mechi ya Ligi Kuu bara kati ya timu hizo iliyofanyika Machi 31 mwaka huu wakati akiwa na adhabu ya kukosa mechi tatu.
No comments:
Post a Comment