Timu za Villa Squad na Yanga zinapambana kesho (Machi 17 mwaka huu) katika mechi namba 142 ya Ligi Kuu ya Vodacom itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Oden Mbaga mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B na sh. 15,000 kwa VIP A. Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni.
Mechi nyingine ya kesho namba 144 itachezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ambapo Coastal Union watakuwa wenyeji dhidi ya Oljoro JKT ya mkoani Arusha.
Ligi itaendelea tena Jumapili (Machi 18 mwaka huu) kwa mechi mbili. Mtibwa Sugar itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Azam watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Stars kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
WATANZANIA WATEULIWA KUCHEZESHA CONGO
Mwamuzi Waziri Sheha wa Tanzania ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha mechi namba 51 ya Kombe la Shirikisho kati ya AC Leopards ya Jamhuri ya Congo na Club Sportif Sfaxien ya Tunisia.
Katika mechi hiyo itakayochezwa jijini Brazzaville kati ya Machi 23, 24 na 25 mwaka huu, Sheha atasaidiwa na waamuzi John Kanyenye na Ferdinand Chacha wakati mezani atakuwa Ramadhan Ibada. Waamuzi wote hao wasaidizi pia wanatoka Tanzania. Kamishna atakuwa Zeli Sinko kutoka Ivory Coast.
Naye Hafidh Ally wa Tanzania ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi namba 53 ya Kombe la Shirikisho kati ya Lydia LB Academic ya Burundi na Enppi ya Misri itakayochezwa jijini Bujumbura kati ya Machi 23, 24 na 25 mwaka huu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment