Mchezo ambao kila mmoja atakuwa anautazama hii leo bila ubishi utakuwa kati ya Man City na Chelsea kwenye uwanja wa Etihad.
Mchezo huu una umuhimu wa aina yake na unatazamwa kama moja ya michezo ambayo itakuwa na uamuzi wa timu itakayotwaa ubingwa wa England. Manchester City wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na presha kubwa sana ya kupata matokeo mazuri kwani tayari wako nyuma ya wapinzani wao kwa pointi nne na kitakachokuwa kinasakwa leo hii na vijana wa Sheikh Mansour ni pointi tatu muhimu kwani endapo watafungwa au watatoa sare watakuwa wamegawa ubingwa kwa wapinzani wao United.
Kwa upande wa Chelsea wanatafuta nafasi ya kumaliza kwenye zile sehemu za kufuzu kushiriki michuano ya ulaya msimu uliopita na kwa sasa wako kwenye nafasi ya tano hivyo wanatafuta matokeo mazuri kwenye michezo yao iliyobaki.
Malengo tofauti ya timu zote mbili kwenye mchezo huu ndio yanauongezea ladha na ugumu wa aina yake.
Moja ya mambo ambayo yametengeneza vichwa vya habari kwa upande wa Chelsea ni aina ya form ambayo wamekuwa nayo tangu walipomtimua kocha Andre Villas Boas . Imepita michezo mitano tangu aondoke na Chelsea imefanikiwa kushinda michezo yote hiyo chini ya Mtaliano Roberto Di Matteo. Kikubwa ambacho kinaonekana kuleta tofauti ni aina ya “attitude” waliyonayo wachezaji wa Chelsea chini ya Di Matteo.
Chelsea inaonekana kama imezaliwa upya vile na hakuna ushahidi tosha wa hili kama mchezo wao wa wiki iliyopita dhidi ya Napoli ambapo waliweza kupigana kufa na kupona hadi kuitoa timu hiyo kwa kuifunga mabao manne kwa moja.
Kilichowashangaza wengi ni jinsi wachezaji hawa hawa walivyoshindwa hata kunyanyua miguu yao wakati alipokuwa Andre Villas Boas.
Kingine ambacho kimekuja wakati sahihi kwa Chelsea ni ufungaji wa mabao wa mshambuliaji mwenye thamani ya paundi milioni 50 Fernando Torres. Jumapili alifunga mabao mawili dhidi ya Leicester City huku akisaidia kutengeneza mengine mawili kwa wenzie.
Kila mmoja kwenye timu ya Chelsea atakuwa na hamu ya kuona mabao haya mawili yakifungua mengine mengi kwa mshambuliaji huyu ambaye amekwenda zaidi ya masaa 24 bila kufunga. Hata hivyo hofu itakuja pale unapofikiria kuwa Torres aliwahi kuonyesha ishara za kurudi kwenye kiwango chake baada ya kufunga kwenye mechi dhidi ya Genk alipofunga mabao mawili na hata mechi dhidi ya Man United ambayo alifunga bao moja lakini baada ya hapo alirejea kwenye ukame wake kama kawaida.
Hali ni tofauti kidogo kwa upande wa City . Kitakacholeta tofauti kwa timu yao kwenye mchezo huu ni jinsi wachezaji watakavyopambana uwanjani lakini wakiwa na ujasiri wa kisaikolojia pia kwani presha itakuwa kubwa sana kwa upande wao hasa baada kujikuta wako nyuma ya United katika kipindi kigumu kwenye ligi kama hiki.
Kuelekea mchezo huu moja ya mambo ambayo yamekuwa yakizungumziwa ni urejeo wa Carlos Tevez ambaye taarifa zinasema kuwa atakuwa benchi. Mancini amejaribu kuwapa moyo wachezaji wake kwa kusema kuwa ana uhakika City watatwaa ubingwa lakini anajua kuwa haitakuwa rahisi kama asemavyo na amezungumzia umuhimu wa Carlos Tevez kama mtu anayeweza kuisaidia City katika hilo.
Wachezaji wa City wakiongozwa na Joe Hart na Kolo Toure wamezungumzia pia umuhimu wa Tevez ambapo Hart anasema kuwa Tevez atakuwa kama mchezaji mpya na Kolo akisema kuwa angependa kumuona Tevez akifunga bao litakaloipa City ubingwa .
Kauli hizi zinaweza kuonekana kama zinajenga umoja kwenye timu lakini zinaweza kuwa mbinu ya kupunguza presha kwa wachezaji wengine jambo ambalo kwenye kipindi kama hiki linaonekana kuwa muhimu sana kwenye safari ya ubingwa wa City ambayo inaweza kuisha kwneye mchezo huu.
City hata hivyo wana matatizo makubwa sana kwenye defence . Nahodha Vincent Kompany na patner wake kwenye defence Joleone Lescott wataukosa mchezo dhidi ya Chelsea kutokana na majeraha.
Kuwakosa wachezaji hawa kunamaanisha kuwa City inabakia na mabeki wawili wa kati ambao ni Kolo Toure na Stefan Savic. Ni vigumu kuamini kuwa Mancini atashawishika kuwachezesha mabeki hawa sababu kuu ikiwa ukweli kuwa hawajacheza pamoja kwa muda mrefu na hivyo ukosefu wa chemistry kati yao unaweza kuidhuru City na kuwapa wepesi kina Drogba na wengineo. Pia Savic amekuwa kimeo kwa City mara zote ambazo amepangwa kucheza kwenye defence.
Mancini anaweza kuwapanga Micah Richards na Kolo Toure kati ya defence au hata kumtumia Yaya Toure ambaye anao uwezo mkubwa wa kucheza kama beki wa kati .
Hata hivyo hakuna matatizo kama haya kwenye idara nyingine za uwanja.
Kwenye Midfield Yaya Toure atakuwepo endapo hatachezeshwa kama mbadala kwenye nafasi ya beki , Gareth Barry na Nigel De Jong wapo pia , James Milner na Adam Johnson. Mancini anaweza kushawishika kuwatumia Barry na De Jong kama viungo wa ziada kuwapa Ulinzi mabeki ambao leo huenda wakawa na wakati mgumu.
David Silva na Adam Johnson pamoja na Sergio Aguerro wanatarajiwa kuwa fit na watatumiwa na kocha Mancini. Edin Dzeko amekuwa kwenye wakati mgumu baada ya kuingia kwenye ukame wa mabao nah ii inamaanisha kuwa huenda akawekwa benchi kama ambavyo imekuwa kwa muda mrefu na Mario Balotelli kwa hakika ana nafasi yake kwenye safu ya ushambuliaji . Carlos Tevez atakuwepo benchi na nafasi yake kuonekana leo sio kubwa sana ukizingatia kuwa City hawana baadhi ya wachezaji muhimu na hii inamaanisha kuwa mabadiliko ya nafasi kujaribu kujaza mapengo yaliyopo yatamnyima tevez nafasi .
Kwa upande wa Chelsea nahodha John Terry atakuwa nje kutokana na jeraha la goti . Fernando Torres pamoja na mabao yake mawili ataanzia benchi . Wengi wanaweza kutafsiri kinyume uamuzi wa kumuanzisha Torres benchi lakini kwa mchezo kama huu ni muhimu kuwa na Plan B na Torres anafit kuwa plan B kama “impact player” na anaweza kuleta madhara pale anapoingia akitokea bench.
Kumkosa Terry kunamaanisha kuwa Gary Cahil atacheza kati kati ya defense na David Luiz huku Ashley Cole na Branislav Ivanovic wakicheza pembeni . Michael Essien , Ramirez, Frank Lampard na Juan Matta watakuwepo kwenye defense huku Didier Drogba na Daniel Sturidge wakicheza mbele.
Manchester City wameifunga City mara nne katika michezo yao mitano iliyopita na Chelsea walijikwamua kutoka kwenye uteja huo mapema msimu huu kwa ushindi wa 2-1 walioupata. Hata hivyo mchezo wa leo una umuhimu wa aina yake kwa kila timu.
City wakiwa na presha ya kuwa nyuma ya United wakitafuta ubingwa watakuwa wanatafuta pointi tatu na hawajapoteza nyumbani katika mechi zao zote za ligi kuu ya England je leo itakuwa mara ya kwanza kwa mwiko huo kuvunjwa, Chelsea nao watakuwa wanataka kuendeleza maisha mapya chini ya Roberto Di Matteo huku wakitaka kumaliza msimu kwenye nafasi ya heshima kwao .
Sijaona alichocheza Ramires kwa kweli usiku wa leo...
ReplyDeleteAmefanya Torres asifunge pia.. Yeye ndiye chanzo cha Chelsea kupoteza mchezo!