Na Magesa Japhari
HABARI zenu ndugu wasomaji wangu popote pale mlipo nje na ndani ya Tanzania .
Mara nyingi nimekuwa nikifuatilia na kujiuliza; hivi ni kwa nini Soka letu hapa Tanzania linakuwa na hatua za mlevi, yaani mbele nne na kurudi nyuma nane na kisha viongozi wetu kuanza kujitapa eti wamefanya kazi kubwa.
Lakini kwangu mimi sioni hatua tuliyopiga zaidi ya kuona ujanja ujanja unaofanyika katika Soka letu. Ukiangalia kwa makini utaona ninachozungumzia kwani tukianza na vilabu vyetu vinavyoshiriki mashindano mbali mbali utaona jinsi gani vinavyoandaliwa.
Vilabu vinaandaliwa bila hata mechi za majaribio na katika mazingira magumu, lakini viongozi wa vilabu hivyo wakihojiwa utasikia timu iko vizuri na inaendelea na kambi vizuri lakini mwisho wa siku katika mashindano yenyewe wanaangukia pua na majibu yao hubadilika gafla; oh! timu haikuwa na maandalzi mazuri isitoshe hatukucheza mechi hata moja ya majaribio.
Sasa wakati unatwambia kambi ya timu ni nzuri na timu iko katika hali nzuri ulikuwa na maana gani. Nadhani wakati umefika tuambiane ukweli kama kocha wa riadha anavyoweka mambo hadharani na wala si kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa.
Tukirudi katika timu zetu za taifa ndio kichekesho kabisa; ulishaona timu inajiandaa kucheza mashindano ya kimataifa eti inajaribiwa na timu ya Vijana ya Azam. Mara inacheza na Vijana wa TSA, sasa tujiulize kama hawa vijana wa Azam wana uwezo wa kuipima Timu ya Taifa, kwa nini wasichukuliwe wao na wakaenda kuwakilisha taifa badala yao .
Kwa viongozi wetu wa vilabu, sasa naona imekuwa vurugu kwani wanafikiri kuonekana katika luninga wakisema jambo ndio wataonekana wanafanya kazi, matokeo yake wamesahau kuwa kila mmoja katika klabu ana mamlaka yake na kazi yake inabidi aifanye. Sasa wewe mwenyekiti, wewe msemaji wa klabu, wewe katibu wa klabu, sasa wenzio watafanya kazi gani au unataka wote waishie kujiuzulu au kuomba kuacha kazi?
Kiongozi badala ya kufanya mikakati ya kuendeleza klabu unaanza kuzunguka kutafuta vyombo vya habari ili tu uonekane. Mimi nina wasiwasi na viongozi kama hawa. Inawezekana kabisa hawapo kwa ajili ya kuongoza Soka letu bali kwa maslahi yao binafsi, maana haiwezekani ukataka kuonekana kila mara katika vyombo vya habari kama ndilo lengo. Viongozi kama hawa nadhani hawatufai katika Soka letu maana wanatufanya tuzidi kurudi nyuma katika soka.
Tukiangalia katika uongozi wa TFF ni madudu mengi yanayofanyika na wamekuwa wakiongoza pia kwa ujanja ujanja mwingi na kupelekea timu zetu za Taifa kuwa vichekesho katika mashindano ya kimataifa. Mfano mzuri ni pale timu ya Taifa iliposhinda Kombe la Tusker na baadaye kualikwa katika mashindano huko Misri. Matokeo yake naamini kila mtu anayajua na sina haja ya kusema. Je ni lini tumewahi kuzipeleka timu za vijana katika mashindano yoyote ambayo tumealikwa?
Na ni lini tumewahi kuandaa kikosi cha vijana kikadumu na hatimaye kuwa timu ya taifa ya wakubwa? Mimi naamini kama tungekuwa na utamaduni wa kuwatunza vijana wenye vipaji tulionao tungefika mbali. Mfano mzuri ni wale vijana walioshinda Kombe la Kopa CocaCola kule Brazil , je kuna mtu yeyote anajua walipo na wana hali gani?
Ukipata jibu basi ndio utajua nini nazungumzia kwani kwa jinsi ninavyoona ujanja ujanja unatawala sana Soka letu.
Je, wale wanaosema kwamba vilabu vya Simba na Yanga vinanunua mechi si wakweli? Maana kama wangekuwa mabinwa wa kweli basi tungekuwa tunaona ubora wao na si siasa za viongozi wao ambao wanazuga katika Soka; na lengo lao likiwa kupata umaarufu na kisha kukimbilia kugombea ubunge.
Nadhani, sasa wakati umefika wa kuweka siasa pembeni na kuamua kufanya kazi ya Soka na kuachana na ujanja ujanja unaofanyika kwa kuweka timu kambini kwa muda wa siku mbili bila hata ya majaribio na kisha kutaka ushindi; na eti tunasimama na kuwataka Watanzania wajitokeze kuwapa sapoti. Karne hii si ya ujanja ujanja kama tunavyofanya, kama kweli tuko tayari basi na tuwekeze katika vijana wadogo na si mbwembwe kama zile za TFF na kisha kufunga kituo cha TSA eti kisa magodoro na baadhi ya vifaa vimekwisha, sasa huo kama sio ubabaishaji ni nini?
Hebu tujipange na tuache huu ujanja ujanja wetu wa kuandaa timu zetu kama mapulizo ya kupamba kwenye harusi na badala yake tufuatilie program tunazopewa na walimu wa timu zetu na kuzifanyia kazi.
E- mail: magesajaph@yahoo.co.uk
Simu: 0784269812/0755826102/0714368843
No comments:
Post a Comment