SIKU zote taifa linapokwenda vitani kanuni ya kwanza ni kukusanya silaha zote muhimu kwa ajili ya vita hiyo. Hata shule ambazo wote tumesoma siku zote hujitahidi kuwaweka karibu wanafunzi wote wenye uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kwenye mitihani kwa kuwa wanatambua mchango wao na ili kupata mafanikio lazima wanafunzi hawa wawe kwenye hali nzuri ili walete mafanikio.
Suala hili linaonekana hata kwenye michezo mbalimbali, ukiachilia mbali mchezo wa soka ambao ndiyo dhima kuu hapa. Mathalani mchezo kama mpira wa kikapu, kwenye ligi ya NBA kuna timu mbalimbali kama vile Los Angeles Lakers. Nani asiyejua kuwa timu hii imejengwa kwa kumzunguka mtu mmoja anayeitwa Kobe Bryant.
Zamani alikuwepo nyota mwingine Shaquile O’neal lakini hata Shaq mwenyewe alikuwa anachezeshwa vizuri na umahiri wa Kobe na ndiyo maana Shaq aliondoka na Lakers haikutetereka kwani Kobe aliendelea kufanya vitu vyake .
Takwimu zinaonyesha kuwa Kobe anapokosekana kwenye hii timu hali huwa mbaya na ushindi kwa Lakers unakuwa mgumu sana. Hali hii hutokea hata kwenye timu nyingine, mfano Dallas Mavericks na Dirk Nowtzki, Miami Heat na Dwayne Wade na nyinginezo.Kwa muda mrefu Tanzania kwenye upande wa soka imekosa nyota ambaye anaweza kuibeba timu hii mgongoni mwake kutokana na kipaji halisi alicho nacho miguuni mwaka mathalani kama ilivyokuwa enzi zile za kina Edibily Lunyamila, Zamoyoni Mogella, Mohamed Mwameja na wengine ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwa timu ya taifa.
Katika kipindi cha miezi 18 iliyopita Taifa Stars imetokea kuwa na Mbwana Samatta ambaye uwezo wake ni kama pumzi mpya kwenye mwili wa Stars. Samatta ana uwezo mkubwa sana ambao ulianza kuonekana tangu akiwa na klabu ya Simba ambako katika kipindi cha nusu msimu ambacho alicheza kwa ukamilifu alidhihirisha umuhimu wake.
Samatta amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu ya Taifa pia. Katika michezo yake mitano ya kwanza akiwa na timu hii Samatta aliweza kufunga si chini ya mabao tatu. Bahati nzuri kwa kijana huyu imekuwa jinsi alivyofanikiwa kutoka mapema nje ya mazingira ya soka la Tanzania ambalo kwa kiasi kikubwa huwadumaza wachezaji wanaocheza hapa nyumbani.Umuhimu wa Samatta umeonekana hata kwenye klabu yake mpya ya TP Mazembe ambako amekuwa akifunga mabao muhimu pamoja na kuwatengenezea wachezaji wenzie, hali ambayo imemfanya awe kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo ya nchini DR Congo ambako mara nyingi hata mashabiki wenye huchanganyikiwa pale anapokosekana .
Jambo la ajabu ambalo lilitokea wiki iliyopita ni kwa mchezaji huyu ambaye ana umuhimu wa kipekee kwenye timu ya taifa, Taifa Stars kuachwa kwenye kikosi cha kocha Mdenishi, Jan Poulsen kwa ajili ya mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya timu ya taifa ya DRC na ule wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya timu ya taifa ya Msumbiji.
Sababu kuu aliyoitoa Poulsen ni kwamba Samatta hayuko fiti au hajitumi, hakika unaposikia sababu hii moja kwa moja unapata picha ya kwamba labda Samatta ameumia au amekuwa amepoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza kwenye klabu yake lakini hakuna chochote kati ya haya mawili ambacho kimetokea. Samatta hajaumia na amekuwa akicheza kwenye kikosi cha kwanza cha klabu yake na hata kwenye mchezo wa mwisho wa ligi kuu alicheza na aliweza kufunga bao wakati timu yake ikipata ushindi wa mabao 5-0.
Hapa ndio tunaporudi kwenye dhana ya Jeshi linalokwenda vitani pasipo kuchukua wanajeshi wake bora pamoja na hazina ya kutosha ya silaha kwa ajili ya kumkabili adui aliyeko mbele yenu. Haina maana ya kwamba akikosekana Samatta mambo hayaendi wala timu haitacheza kwa sababu lazima kuwepo na mpango mbadala au ‘Plan B’ ,lakini pale anapokuwa fiti halafu haitwi lazima wadau tutahoji.
Kwa heshima yote aliyo nayo Mwalimu wa timu ya taifa, Poulsen kutokana na uzoefu wake, hakuna anayediriki kumuingilia katika kazi yake kama kocha wa timu ya taifa lakini pale anapochukua uamuzi unaoonekana kuwa una walakini, lazima tuhoji.
Mwishoni mwa miaka ya 90 timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars walikuwa na kocha Mjerumani Marehemu Reinhardt Fabisch(mungu amlaze mahali pema peponi). Fabisch alikuwa na kawaida au unaweza kusema alikuwa na tabia fulani ya kuwaacha wachezaji nyota, aliwahi kumuacha mchezaji pekee wa Harambee ambaye kipindi kile alikuwa akicheza soka la kulipwa Mike Origi Okoth.
Baadaye Fabisch alimrudisha okoth na kumpa sharti la kufunga mabao matatu kwenye mchezo dhidi ya Burkina Faso. Okoth akafunga mabao manne na kumvua nguo kocha wake aliyedai kuwa hana kiwango. Fabisch aliwahi kufanya kosa hilo pale alipomfungia vioo mshambuliaji Christian Chukwu kwenye kikosi cha kwanza cha klabu ya Mamelodi Sundowns . Lakini akalazimishwa kumpanga na wakurugenzi wa timu hiyo, Chukwu alifunga mabao manne kwenye mechi yake ya kwanza.Hii yote ni mifano inayoonyesha kuwa kila timu ina wachezaji muhimu na siku zote wanapoachwa timu lazima igharimike . Pengo la Mbwana Samatta lilionekana kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na hakuna anayejua kitakachotokea kwenye mchezo muhimu dhidi ya Msumbiji.Kinachosumbua vichwa vya watu ni kwamba Samatta yuko fit na amekuwa akicheza kwenye klabu yake na kiwango chake kiko juu na jana tu ameifungia timu yake kwa mara nyingine kwneye mchezo wa ligi ambao TP Mzembe imeshinda mabao manne , mabao mawili katika michezo miwili ni rekodi nzuri na ‘Consistency aliyo nayo kwenye klabu yake imekuwepo hata kwenye timu ya taifa. ‘Fitness’ anayoizungumzia Mwalimu Poulsen kukosekana kwa Samatta ni ipi?Mwalimu Jan Poulsen ana uhuru wa kufanya atakavyo kwenye benchi la ufundi la Taifa Stars , lakini linapokuja suala la Samatta, akubali au akatae, kijana huyu anabaki kuwa mchezaji muhimu kwenye timu ya taifa na kukosekana kwake ni jambo ambalo lazima lipatiwe maelezo ya kina. Tanzania ni nchi changa linapokuja suala la soka la kimataifa na safari ya taofa hili imekuwa ikipunguzwa kasi kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kuwatengeneza kina Samatta wengine ili huy akiyepo asilemewe na mzigo wa kutegemewa peke yake. Endapo Taifa Stars itafanya vibaya kwenye mchezo dhidi ya Msumbiji hakika Poulsen atakuwa na maswali mengi ya kujibu.
Ninaamini nimeeleweka, lakini mimi bado sijaelewa na ndiyo maana ninataka jibu la swali langu kuwa, kwa nini Samatta hayupo kwenye kikosi cha Taifa Stars?
Shaffih .
ReplyDeleteKwanza kabisa heshima kwako mkuu, na nipongeze mabadiliko uliyoyafanya katika blog yako.
Kuhusu suala la Mbwana Samatta labda niseme tu kwamba mimi pia nilishangazwa sana niliposikia kikosi hicho bila kuwepo jina la Samata na lawama zangu za kwanza nilizipeleka kwenu waandishi wa habari ambao mlikuwepo ukumbini pindi kikosi hichi kilipokuwa kinatangazwa kwani mlipaswa kutusaidia kumbana kocha atoe sababu za kueleweka na sio kutuletea maneno yake ya ajabu ajabu.
Sina maana kwamba Samatta ni suluhisho la matatizo yetu kwenye timu ya Taifa ila hakuna asiyeujua mchango wa Samatta uwanjani hata kama hafungi goli ila timu inakuwa na uhai.Mimi binafsi sababu alizozitoa huyo mzee kuhusu kumuacha Samatta haziniingii akilini hata kidogo. Nina muheshimu sana huyo Mzee kwani ni kocha mwenye CV nzito na pia ni mkufunzi lakini hayo yote hayaaaminishi kwamba kwenye soka yeye anajua kila kitu, tumeona mifano mingi ya machocha bora kabisa wanakalishwa kitimoto pamoja na ubora wao itakuwa huyu Babu.
Angalia tukio lililotokea majuzi wakati Chelsea wanacheza na Napoli,AVB aliwaweka benchi Lampard,Essien na Cole ambaye alikuja kuingia baadae ya Bosingwa kuumia na timu ilipofanya vibaya Mmiliki wa Timu alimwambia AVB atoe maelezo ni kwanini aliwaweka benchi.
Suala la kuwa na viongozi wasiojiamini huleta matatizo kama haya ambapo wanaogopa kumuuliza kocha na kumbana mimi sina imani kabisa na watendaji wa TFF:
Huu sio muda wa kuleta mzaha na timu ya Taifa wakae wakijua tumechoka kuwa wasindikizaji wakati wao wanashibisha matumbo yao na huyo mzee akae akijua hatutaki utani hata kidogo tunataka matokeo sasa, masuala ya undumulakuwili hatuyataki tena.
Samatta bado ni mdogo sana na mchango wake unahitajika sana kwenye National team yeyekama anaona kijana hana uzalendo amuite kwenye National team kisha wakae wazungumze, mchezaji kutofunga kwenye mechi 2 za National team hakumaanishi hana uzalendo ndio maana Timu huwa zinakuwa na wataalamu wa Saikolojia ili kuwaweka wachezaji sawa.
Babu aache utani muda wa kutaniana umekwisha sasa ni matokeo.
Na hii TFF hii yaani basi tu