Uwanja wa soka unaomilikiwa na Jeshi la Misri, uliopo jijini Cairo, Misri ndiyo utakaochezwa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa kati ya Zamalek na Yanga ya Tanzania.
Maofisa wa uwanja huo, ambao pia ni chuo maalumu cha masuala ya kijeshi walisema juzi kuwa tayari wameshapata taarifa kuhusiana na suala la mechi hiyo.
Lakini maofisa hao ambao hawakutajwa majina, walikaririwa na mtandao wa Misri wa Ahram Online, wakisema wana asilimia kubwa kwamba mechi hiyo itachezwa jeshini.
Kulikuwa na hofu kama mchezo huo ungeweza kufanyika Cairo kutokana na sababu za kiusalama kufuatia maafa ya mashabiki 74 yalitokea kwenye Uwanja wa Port Said wakati wa Mechi ya Al Ahly na Al Masry.
Zamalek imepewa ruhusa ya kucheza kwenye uwanja huo wa kijeshi na itachezwa bila ya mashabiki kufuatia kufungiwa kwa timu hiyo kucheza mechi zake za Ligi ya Mabingwa bila ya mashabiki na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kufuatia vurugu za mashabiki wa timu hiyo kwenye mechi dhidi ya Club Africain ya Tunisia msimu uliopita.
Zamalek, ambayo ilichukua taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya mwisho mwaka 2002, ilitoka sare ya bao 1-1 na Yanga kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam Jumamosi iliyopita na sasa zitarudiana Jumamosi wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment