zimesalia siku chache kabla ya Mabingwa wa soka kwa mujibu wa Ligi kuu ya Tanzania Bara Dar Es Salaam Young Africans hawajatupa karata yao ya kwanza kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika safari hii wakivaana na Zamalek Sc ya nchini Misri.
Hadi kufikia tarehe 18 ambapo mchezo huu utakuwa unachezwa Yanga watakuwa wamepata michezo kadhaa ambayo kwa upande wake itakuwa majaribio muhimu ama sehemu ya maandalizi .
Rekodi haionyeshi matumaini kama Yanga wanaweza kweli kuitoa Zamalek lakini rekodi hizi hizi kwa kawaida huwa zinawekwa ili zivunjwe na mwamuzi wa mchezo ni dakika 90 na kwa hatua kama hii ni dakika 180 za michezo miwili yaani ule wa nyumbani na wa ugenini.
Bahati mbaya zaidi ni ukweli usiopingika ambao wote tunaufahamu juu ya maandalizi mabovu ya timu za Tanzania kuelekea michezo mikubwa kama hii. Zamalek ni moja ya timu 3 bora barani Afrika kwa kipindi cha karne iliyopita na wana historia ambayo inatosha kuzifanya timu nyingi ziogope hata kuwakaribia.
Lakini kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita rekodi hazizungumzi vizuri kuhusu Zamalek na hapa ndio watanzania wanaweza kutazama na kuona matumaini yalipo. Zamalek haijaonja mafanikio kwenye michuano ya kimataifa kwa zaidi ya miaka mitano na mara ya mwisho walitolewa kwenye raundi ya pili na Club Africain ya Tunisia.
Ukirudi kwenye ligi kuu nchini Misri Zamalek mwenendo wake umekuwa wa kusuasua kwa muda sasa na imepita miaka takribani saba Klabu hii haijaonja ladha ya mafanikio ya ubingwa wa ligi kuu na ahueni yake ya kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa imekuwa nafasiiliyo nayo nchi ya Misri kwenye viwango vya ubora vya CAF ambavyo vinaipa nchi hii fursa ya kutoa washiriki wawili kwenye michuano ya Klabu bingwa barani afrika.
Hata hivyo hayo hayatoshi kuwafanya Yanga waone wepesi wa kuitoa Zamalek kwani bila shaka kila mmoja anatambua kuwa Yanga ndio vibonde kwenye mchezo huu nab ado Zamalek wanabaki kuwa tishio kwa Yanga hivyo lazima kazi ifanyike ili Yanga ifanikiwe kuitoa klabu hii toka Misri.
Katika msimu huu wa ligi ya Misri , Zamalek hadi sasa wanashika nafasi ya Tatu nyuma ya Klabu za Al Ahly wanaoshika usukani wa Ligi hiyo na Haras El Hadoud wanaoshika nafasi ya pili . Cha ajabu ni kwamba Klabu hizi zilizoko mbele ya Zamalek zote zimeshawahi kucheza na klabu za Tanzania Yanga wakiwemo pamoja na Simba kwa nyakati tofauti . Zamalek hadi sasa zikiwa zimechezwa raundi 14 za michezo ya ligi kuu wamefaikiwa kushinda jumla ya michezo 10 huku wakipoteza miwili na kutoka sare miwili . Katika michezo hiyo Zamalek wamejikusanyia jumla ya pointi 32 ambapo wamefanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani wake mbalimbali mara 27 na kwa upande wao wenyewe wameruhusu wavu wao kuguswa mara zisizopungua 11 . Katika kikosi hi jukumu la ufungaji limemwangukia kiungo Ahmed Hassan ambaye hadi sasa amefunga mabao 7 . Ahmed Hassan hayuko peke yake , Zamalek ina nyota wa kutosha ambao wana uwezo wa kuifanya timu yoyote ‘kitu mbaya ‘ pale itakapokutana nayo . Kuna watu kama Amr Zaki na Ahmed Hossam Mido ambao wamerudi nyumbani baada ya kuhangaika ulimwenguni kote wakicheza soka la kulipwa . Uwezo wa watu hawa unafahamika kwa watu wote na hakuna jipya ambalo halijawahi kuzungumzwa kuwahusu . Mido amekuwa akifunga mabao katika ngazi ya juu ya mchezo wa soka kwenye ligi mbalimbali barani ulaya hususani kwenye ligi kama za England ambako amewahi kuzichezea Tottenham Hotspurs na Middlesborough, Ligi ya Serie A , Ufaransa na sehemu nyingi tu . Zaki amewahi kuichezea Wigan Athletic ambako mabao yake 9 kwenye michezo kadhaa misimu miwili iliyopita yaliwafanya hata Liverpool wamzungumzie mchezaji huyu. Nyuma ya washambuliaji hawa yuko kiungo mahiri pengine kuliko wote kwenye soka la Misri kwa miaka ya hivi karibuni Mahmoud Abd El Razak maarufu kwa jina la Shikabala na wote hawa wako chini ya kocha mwenye historia ya kipekee barani Afrika Hassan Shehata ambaye amerejeshwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Hossam Hassan aliyeachia ngazi miezi michache iliyopita.
Rekodi za Yanga kwa msimu huu hazitofautiani sana na Zamalek hadi kufikia hatua hii . Juzi tu Yanga wamecheza mchezo wake wa 15 ambapo walifanikiwa kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya JKT RUVU . Yanga imekusanya jumla ya pointi 31 huku wakiwa wameshinda michezo 9 , wametoka sare michezo minne na wamepoteza michezo miwili. Kwenye ufungaji bado Yanga haitofautiani sana na Zamalek wakiwa wamekusanya jumla ya mabao 25 huku wakiruhusu wavu wao kuguswa mara 12. Mshambuliaji toka Ghana Kenetth Asamoah amekuwa kinara ambapo amefunga mabao 9 .
Takwimu zinafanana kwa kiasi Fulani lakini ukiangalia ligi za nyumbani ambazo timu hizi mbili zinashiriki hapo ndio unapoweza kuona tofauti kubwa baina ya timu hizi mbili ilipo.Wanadamu huamini kuwa hakuna jambo linaloshindikana chini ya jua na mashabiki , wapenzi , viongozi na wachezaji wa Yanga wataamini vivyo hivyo lakini kwa yale yanayowezekana baada ya dhana hii ya hakuna kinachoshindikana huwa wanafanya vitu Fulani ambavyo vinawafanya wawe na hali ya kustahili kufanya yale wanayotaka . Maana yake ni kwmaba Yanga wanapaswa kufanya maandalizi yatakayowafanya wastahili kupata ushindi na sio kuishia kutegemea bahati .
Endapo maandalizi ya ukweli na ya dhati yatafanyika kweli hakuna kinachoshindikana chini ya jua na hata kwenye uwanja wa mita mia moja kwa sitini za uwanja wa mpira ambao Yanga watacheza na Zamalek hiyo tarehe 18 na wiki mbili baada ya hapo kwenye mchezo wa marudiano.
shaffi usiwape moyo wenzio kaka,tembo aliokonda hata siku moja huwezi kumuita ng'ombe,huko unakokuita kusuasua kwa zamaleki swa na yanga utaona mziki,yanga atachezea za kutosha tu aggregate kama 6 ivi we utaniambia
ReplyDeletechela wa Dom