UDHAMINI mnono unaopatikana Tanzania umelifanya Baraza la vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuamua kurudisha Kombe la Kagame jijini Dar es Salaam tena mwaka huu.
Michuano hiyo ya Kagame iliyofanyika mwaka jana na kushuhudia Yanga ikitwaa ubingwa baada ya kuifunga Simba katika fainali huku umeme ukikatika Uwanja wa Taifa, mwaka huu yalipangwa kufanyika Rwanda.
Akizungumza na gazeti la The New Times la Rwanda, Katibu mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, alisema wameamua kurudisha mashindano hayo Tanzania kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka jana.
Pamoja na mafanikio ya mashindano hayo, Cecafa pia kuna jambo moja la muhimu la kupatikana kwa wadhamini Tanzania ambao wameshapata siku moja iliyopita.
Taarifa hiyo inalifanya jiji la Dar es Salaam kuwa mwenyeji kwa mara ya pili mfululizo kwa Kombe la Kagame kama ilivyokuwa kwa Kombe la Chalenji lililofanyika mwaka jana na kushudia Uganda 'Cranes' wakitwaa ubingwa huo kwa kuichapa Rwanda.
Zanzibar na Sudan pia walikuwa wakipewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa kwa klabu Afrika Mashariki na Kati, lakini tatizo la fedha limewakosesha nafasi hiyo.
Fainali ya mwaka jana ya Kombe la Kagame, ilizikutanisha timu zote za Tanzania, Simba na Yanga na kushuhudia kocha Sam Timbe akipata taji lake la nne la Kombe la Kagame baada ya kufanya hivyo akiwa na SC Villa (2005), Polisi (2006), Atraco (2009) na Yanga (2011).
No comments:
Post a Comment