Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeomba mechi ya marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga ya Dar es Salaam na Zamalek ya Misri iliyopangwa kufanyika jijini Cairo, Misri
Machi 1,2 au 3 isogezwe mbele kwa wiki moja.
Pia TFF imeomba mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba ya Dar es Salaam na Kiyovu ya Rwanda iliyokuwa ifanyike Dar es Salaam mwanzoni mwa Machi kama mechi ya Yanga nayo isogezwe mbele kwa wiki moja.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema Dar es Salaam jana kuwa wameandika barua Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuomba mabadiliko hayo kutokana na mechi hizo kukaribiana na ile ya timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Alisema Taifa Stars itacheza mechi na Ivory Coast kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia Februari 29, hivyo wachezaji kuweza kucheza mechi nyingine Machi mwanzoni itakuwa ni kutowapa nafasi ya kupumzika.
Alisema wachezaji wengi wanaounda Taifa Stars pia wapo kwenye timu za Simba na Yanga,
hivyo mazingira ya tarehe hizo yatawabana kuweza kutumikia majukumu ya pande zote mbili.
Yanga itacheza na Zamalek mchezo wa kwanza katika raundi ya awali jijini Dar es Salaam Februari 18 mwakani, kabla ya mchezo wa marudiano wiki mbili baadaye jijini Cairo nchini Misri.
Mshindi wa mechi hizo atakutana na kati ya Missile ya Gabon na Africa Sport ya Ivory Coast, katika raundi ya kwanza, itakayoanza Machi mwakani.
Wakati huohuo, Osiah alisema TFF haiwezi kushughulikia tuhuma zilizotolewa na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Miembeni United ya Zanzibar Salum Bausi kwamba alishinikizwa timu yake ifungwe na Simba katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi hatua ya makundi wiki iliyopita.
Akizungumza jana, Osiah alisema madai ya Bausi yanatakiwa yashughulikiwe na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ama mamlaka zinazopambana na rushwa Zanzibar.
Search This Blog
Wednesday, January 11, 2012
TFF: WAOMBA MECHI YA YANGA NA ZAMALEK ISOGEZWE MBELE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment