Search This Blog

Wednesday, December 28, 2011

Tuzigeuze shule za msingi kuwa ‘soccer academies’


Fred Mwakalebela
PAMOJA na kuwapa pole Watanzania wenzetu waliokumbwa na mafuriko jijini Dar es Salaam na sehemu nyingine za nchi, ni vyema pia nikawapa heri ya Sikukuu ya Noeli wale wote waliopata bahati ya kuisherehekea siku hiyo.

Naam, ni bahati kwa kusema ukweli kwani kuna mashabiki wengi tu wa soka waliokuwa wakiishi maeneo ya mabondeni jijini hapa kwa sasa wamesahau hata neno ‘soka’ kutokana na maswahibu yaliyowakuta.

Lakini wiki moja kabla ya majanga haya, Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa kushirikiana na mabosi wao FIFA, waliandaa kitu kama tamasha lililojumuisha waalimu wa michezo kutoka shule mbalimbali za msingi jijini hapa.

Tamasha hilo lililopewa jina la ‘Grassroots Football’, ni jambo kubwa sana linalopaswa kupongezwa na kisha kuendelezwa ili ndoto za mashabiki wa soka za kuona soka la Tanzania linasonga mbele ziweze kutimia.

Sina uhakika sana kama walimu wa michezo nchini kwenye shule za msingi wana utaalamu kama waliokuwa nao walimu wetu enzi zile tukiwa shuleni.

Serikali ya Nyerere, ingawa wengi humchukulia mzee yule kama mmoja wa viongozi waliokuwa mbali na michezo, bado serikali yake ilitoa kipaumbele kwenye michezo.

Wakati ule walimu wa michezo walikuwa wakipata mafunzo ya kitaalamu kwenye Chuo cha Walimu Butimba, na hata wanapokuwa kazini, walikuwa wakipewa nafasi ya kwenda kujiendeleza kwenye Chuo cha Michezo cha Malya.

Kwa hiyo, mkusanyiko wa walimu wa michezo kutoka shule za msingi uliofanyika jijini wiki iliyopita, ulipaswa kuwa mkusanyiko wa wataalamu kabisa wa soka la vijana, na unapaswa kufanyika kila kona ya nchi, kila mwaka.

Je, hilo litafanyika? Na je, TFF na wadau wengine wa soka wamejiandaaje na changamoto ya uhaba wa viwanja? Wakati wenzetu wa Zanzibar wameendelea kuvitunza viwanja vyao vya Mnazi Mmoja na Maisela, sisi viwanja vya Jangwani vinauzwa! Tufanyeje?

Tumebaki tunategemea viwanja vya shule za msingi na sekondari zile za enzi za Mwalimu tu. Kwa sasa kila shule ya msingi ina pacha wake, lakini kiwanja kimabaki kimoja tu huku idadi ya wanafunzi ikiongezeka zaidi ya mara 10 ikifananishwa na idadi ya mwaka 1990.

Shule za kisasa, ambazo ni lazima zitanguliwe na jina la ‘Saint’ au ziwe na neno ‘Academy’, ziko kibiashara zaidi na suala la kiwanja wala haliwaingii akilini. Hapa ninadhani ni vyema Serikali ikaingilia kati na kuweka sheria kuwa shule isiyo na uwanja wa michezo haitasajiliwa.

Soka ni lazima lianzie kwa watoto au vijana. Kwa kuwa Tanzania tunaonekana kushindwa kuwa na academy za soka za ukweli, basi ni vyema ukasukwa mkakati endelevu chini ya TFF na Kamati ya Olimpiki ili vijana hawa walio shuleni leo wakapatiwa mafunzo huko huko, yaani tuzifanye shule ziwe academy za soka kwa kuwaendeleza watoto wenye vipaji.

Ukiwekwa mkakati wa ukweli, miaka kadhaa ijayo shule zetu zinaweza kuanza kupata matunda ya programu hiyo kwani iwapo itatoa mwanasoka atakayenunuliwa na timu kubwa, kwa mujibu wa sheria ya FIFA ya training compensation, zitakuwa zikipokea asilimia fulani ya malipo ya mchezaji huyo.

Mfano akienda Simba au Yanga na baadaye akachukuliwa na TP Mazembe kisha akaenda Chelsea, mlolongo wote huo utatakiwa kuwa ukitoa asilimia ya fedha kwenye academy iliyokuza au kufufua kipaji husika.

Ni hapo ndipo ninajiuliza kwanini TFF imeamua kuivunja Tanzania Soccer Academy (TSA) wakati fedha ya Vodacom ilikuwapo? Huu ni mfano mbaya sana kwa wengine waliokuwa na ndoto za kuanzisha academy kwani watajiuliza iwapo TFF yenyewe imeshindwa, sisi tutawezaje?

Nirejee kwenye tamasha la walimu. TFF na FIFA wanapaswa kulipeleka kwenye mikoa kama Tabora au Mwanza ambako walau viwanja vya soka bado vipo na watu wanapenda mchezo wenyewe.

Walimu wa mikoa hiyo wahamasishwe na ikiwezekana wapelekwa Malya kusomea soka la vijana! Tena nadhani walimu hawa ndio wangepaswa kupewa nafasi ya kushiriki ile kozi ya Nishani za Miaka 50 ya Uhuru.

Niwasilishe hoja kwa kumwomba bosi wa Kamati ya Olimpiki kuangalia uwezekano wa kuisaidia TFF kuzifanya shule za msingi kuwa academy za soka.

Si lazima ziwe shule zote, wanaweza kuteua shule moja katika kila wilaya au mkoa na kuisheheni walimu wataalamu wa soka la vijana, walimu hao wakawa wakiwakusanya vijana wenye vipaji na kuwaweka pamoja.

Niwatakie heri kwenye kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

No comments:

Post a Comment