WADAU WASAIDIE TWIGA STARS
Timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) inaendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam chini ya Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwasa kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Namibia baadaye mwezi ujao. Mechi hiyo ya kwanza itachezwa ugenini Januari 14 mwakani jijini Windhoek. Timu hiyo ambayo sasa inafanya mazoezi kwa wachezaji kutokea majumbani (off camp) inatarajia kuingia kambini Januari Mosi mwakani. Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linahitaji zaidi ya sh. milioni 50 ikiwa ni gharama za safari, kambi na posho kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa ajili ya mechi hiyo moja tu. Mechi ya marudiano itachezwa Januari 29 mwakani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Tunatoa mwito kwa wadau mbalimbali zikiwemo taasisi, kampuni na watu binafsi kusaidia ushiriki wa Twiga Stars kwenye mechi hiyo na michuano hiyo kwa ujumla. Twiga Stars kama ilivyo kwa timu nyingine za Taifa ukiondoa Taifa Stars bado haina mdhamini.
WAAMUZI 14 WAPATA BEJI ZA FIFA
Waamuzi 14 wakiwemo wawili wapya wamefanikiwa kupata beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa mwaka 2012 baada ya kufaulu mtihani wa waamuzi uliofanyika mwaka huu na kusimamiwa na shirikisho hilo. Ferdinand Chacha na Ali Kinduli ambao ni waamuzi wasaidizi ndiyo wapya katika jopo hilo la waamuzi wa FIFA kwa Tanzania. Waamuzi wa kati waliopata tena beji hizo ni Ramadhan Ibada, Orden Mbaga, Israel Mujuni na Sheha Waziri. Mbali ya Chacha na Kinduli, waamuzi wengine wasaidizi kwa upande wa wanaume ni Josephat Bulali, Hamis Changwalu, Erasmo Clemence, Khamis Maswa na Samuel Mpenzu. Kwa upande wa wanawake, mwamuzi wa kati ni Judith Gamba wakati wasaidizi ni Mwanahija Makame na Saada Tibabimale. Mwamuzi pekee wa FIFA 2011 ambaye jina lake halikurudi ni John Kanyenye ambaye alikuwa mwamuzi msaidizi.
TAIFA STARS, DRC KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI
Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imeomba kucheza mechi moja ya kirafiki na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars). Mechi hiyo itafanyika Februari 23 mwakani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. DRC inatarajia kuwasili nchini Februari 18 mwaka huu ambapo itaweka kambi yake ya mazoezi hadi Februari 25 mwaka huu kujiandaa kwa mechi yao ya mchujo ya Kombe la Afrika (CAN) dhidi ya Mauritius. Mechi ya DRC na Mauritius itachezwa Februari 29 mwakani nchini Mauritius. Stars yenyewe itacheza mechi ya kwanza ya mchujo kwa ajili ya fainali hizo za 2012 zitakazofanyika Afrika Kusini dhidi ya Msumbiji. Mechi hiyo itachezwa Februari 29 mwakani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
13 WASHIRIKI KOZI YA UKAMISHNA
Kozi ya siku mbili ya ukamishna iliyomalizika Desemba 29 mwaka huu imeshirikisha washiriki 13 chini ya ukufunzi wa Stanley Lugenge, Leslie Liunda na Sunday Kayuni. Walioshiriki kozi hiyo ni Abdallah Zungo, Ally Mkomwa, Ally Mozi, Army Sentimea, Awadi Nchimbi, Beatus Manga, Christopher Mpangala, Hakim Byemba, Josephat Magazi, Juma Mgunda, Juma Mpuya, Mugisha Galibona, Ramadhan Mahano, Robert Kalyahe na Said Nassoro. Wakufunzi wanaendelea kusahihisha mitihani ya washiriki na baada ya kazi hiyo kwa ambao watakuwa wamefanya vizuri majina yao yataingizwa katika orodha ya makamishna kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na mashindano mengine yanayosimamiwa moja kwa moja na TFF.
No comments:
Post a Comment