Search This Blog

Tuesday, December 27, 2011

KOSTADIN PAPIC AUFUNGA MWAKA 2011 KWA KISHINDO!


MICHAEL MOMBURI
KOCHA wa Yanga, Kostadin Papic, amekiri kwamba kikosi chake hakijaiva kimazoezi wala kisaikolojia kuikabili Zamalek ya Misri kwenye mechi ya kwanza ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini amewaomba mashabiki watulie.

Papic ambaye alijiunga na Yanga hivi karibuni akichukua nafasi ya Sam Timbe aliyetimuliwa, amewaomba mashabiki kuwa watulivu na kuelewa kwamba hali si nzuri klabuni, kutokana na ukosefu wa fedha unaowakabili.

Papic alisema kuwa akili yake ilikuwa kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanya vizuri zaidi kwa kuanza na Zamalek, lakini kwa mazingira yaliyopo timu hiyo haiko tayari kwa mchezo wowote.

HALI HALISI
Mserbia huyo aliyewahi kuzinoa Orlando Pirates na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini, alisema timu hiyo inakabiliwa na ukata mkubwa kuanzia kwa wachezaji, viongozi na yeye mwenyewe.

Katika hali ambayo iliwashitua waandishi wa habari kwenye mkutano wake wa jana Jumatatu jijini Dar es Salaam, Papic alitamka wazi kwamba hata mafuta ya gari ya klabu yaliyomtoa nyumbani kwake Upanga mpaka Ilala kwenye ofisi za Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) alipofanyia mkutano huo aligharimia mwenyewe kinyume cha utaratibu.

Sijakimbilia TFF kuja kuishtaki Yanga, nimekuja kukutana na waandishi wa habari hapa wote kwa pamoja ili kuepuka kutoa taarifa tofauti zinazoweza kutafsiriwa isivyo, alisema.

Hapa nilipokuja, tunazungumza wote hivyo mtaelewa kitu kimoja, tofauti na kuzungumza kwenye simu na mmoja mmoja, zitakuwa habari tofauti.

Lakini cha msingi zaidi ni kwamba pale klabuni Yanga kuna kambi ya waathirika wa mafuriko yaliyokea wiki iliyopita hapa Dar es Salaam, sioni kwamba ni busara kwenda kuweka mkutano kama huu pale, kwanza hakuna utulivu wa kutosha halafu watu wana matatizo si sehemu mwafaka ya kuzungumzia mambo kama haya, ndiyo maana nimekuja hapa.

Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba, alimzuia kocha huyo kutumia kumbi za mikutano za shirikisho hilo kwa maelezo kuwa hawana taarifa yoyote toka Yanga na kwamba mikutano kama hiyo hufanyiwa klabuni.

Kutokana na msimamo huo, kocha huyo alilazimika kusimama kwenye veranda za shirikisho hilo na kumwaga aliyonayo kwa mapaparazi.

MISHAHARA
Hali ni ngumu wachezaji hawana mishahara, mimi sina mshahara, sasa katika hali kama hiyo utafanyaje kazi? Ukiuliza viongozi wanakwambia kwamba klabu haina fedha.

Ni vigumu kufanya kazi katika matatizo makubwa kama haya, mbaya zaidi hata viongozi hawatoi ushirikiano si kwa simu wala kuwasiliana nao uso kwa uso. Hii inaleta picha mbaya hasa kwa klabu inayojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika, sisi tulikuwa tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri lakini kwa hali hii siwezi kuahidi chochote.

Tatizo hapa si mshahara wa kipindi gani kwa vile kila mmoja tatizo lake lina ukubwa wake, kilichopo ni kwamba tulipwe mishahara tufanye kazi.

Morali ya wachezaji imeshuka, hawa pia ni binadamu na wana majukumu yao ya kifamilia kama mimi kocha wao.

MAZOEZI
Timu haijafanya mazoezi tangu Jumanne iliyopita mafuriko yalipoanza, tatizo la mafuriko lilikuwa halikwepeki, viwanja kila sehemu vilijaa maji.

Lakini mpaka sasa timu inayojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika na ambayo inacheza mechi za ligi Januari mwakani haina mazoezi kwa siku saba. Hapa unategemea nini?

Nimewaambia viongozi kwa vile hatuwezi kufanya mazoezi uwanjani, basi twende gym hapo napo wanasema klabu haina fedha ya kupeleka timu huko, haya ni matatizo, Yanga ipo kwenye matatizo makubwa na hili kila mmoja anapaswa kulielewa vizuri.

Matatizo ni makubwa mno, hayafichiki. Tulikuwa tumeshashika kasi ya mazoezi sasa tumesimama siku saba bila kufanya chochote, hiyo kiufundi inamaanisha kwamba ninahitaji wiki tatu nyingine kuitengeneza timu vizuri.

Hiyo tayari ni Januari mwakani, kumbuka mwezi huohuo mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara unaanza, timu inahitajika kuwa fiti kwa ligi na hapo hapo una siku chache nyingine kucheza na Zamalek.

Timu haiko tayari kabisa kwa mchezo wowote ule, lazima tuambiane ukweli na wote wanaoipenda Yanga wajue hali halisi. Nimefuta mechi zote za kirafiki kwa sasa.

ZAMALEK NA MAPINDUZI
Timu haiko tayari hata kidogo kucheza na Zamalek kwa vile haijaandaliwa mpaka sasa, si Zamalek tu haiko tayari kucheza mechi yoyote ile kwa sasa, huwezi kuchezesha timu ambayo haijaandaliwa, utakuwa huwatendei haki mashabiki.

Angalia wenzetu Zamalek wanafanya maandalizi mazuri sana kwa taarifa nilizonazo ni kwamba wameshakuja Dar es Salaam wameandaa kila kitu kwa ajili ya mechi ya Februari, wameshaandaa hoteli, maji, chakula na usafiri wao.

Lakini Yanga ambayo inacheza nayo haina chochote inachofanya, hii ni hatari kubwa.
Hata hilo Kombe la Mapinduzi sina taarifa nalo na timu haitacheza kwa vile haina maandalizi, tutaangalia uwezekano wa kupeleka timu ya vijana ili hii nyingine ipate angalau muda wa maandalizi kama hizo fedha zitakuwa zimepatikana.

MASHABIKI
Lengo langu kubwa ni kuwaambia mashabiki kwamba hali si shwari na wajue kwamba Yanga yao ikoje kusudi tusije kulaumiana pasipo sababu, ndio maana nikaitisha mkutano huu, alisema Papic ambaye kuna uwezekano mkubwa akajiuzulu kuinoa Yanga.

Mashabiki wasije kumlaumu mchezaji yeyote au kocha kwa lolote lile, wanapaswa kujua kwamba uongozi haujaandaa timu kimazoezi kwa vile hauna fedha, ukweli ndiyo huo.

VIONGOZI
Papic aliwashutumu vikali viongozi, akisema wamekuwa wakimpa ushirikiano mdogo sana.

Mara nyingi hata simu zangu hawapokei na wala hawataki kuonana na mimi tuangalie cha kufanya, hii hali si nzuri kabisa, ninafanya kazi katika wakati mgumu.

Mambo mengi tuliyokubaliana kwenye mkataba hayatekelezwi ndiyo maana unakuta hata kwenye nyumba ninayoishi ni matatizo makubwa, hakuna maji wala umeme, sasa nitaishije?

Wala hakuna kiongozi yoyote aliyefanya juhudi ya kuondoa hali hiyo. Sasa tunawezaje kupata mafanikio katika mazingira ya utendaji kama huo?

MWENYEKITI
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alipoulizwa jana Jumatatu alisema yupo likizo na hawezi kuzungumzia chochote na akaelekeza atafutwe Katibu Mkuu, Selestine Mwesigwa.

Katibu huyo aliiambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kuwa Papic alisaini mkataba Oktoba 24 na tayari ameshalipwa mshahara wa miezi miwili hivyo wanashangaa anadai nini.

Suala la mishahara ya wachezaji kuchelewa si kitu cha ajabu kwani wanajua hulipwa tarehe 28 kila mwezi, Mwesigwa alisema.

Hilo suala la gym sisi tuna gym pale klabuni na yeye alituambia kwamba kwa sasa anafanya programu ya uwanjani tu.

MWAPE
Kutokana na ukata ulioelezewa na Papic, mshambuliaji Davies Mwape, amelazimika kuirudisha familia yake kwao Zambia baada ya maisha yao ya Dar es Salaam kuwa magumu.

Papic alisema: Amechukua familia yake ameirudisha kwao Zambia, hawezi kuishi nao hapa katika mazingira magumu kiasi hicho, hata hoteli ameshindwa kulipwa na mengine muulizeni mwenyewe.

5 comments:

  1. HILO NDIO SOKA LA BONGO,HALITOENDELEA KAMWE!!!! WADOGO ZETU NA WATOTO WETU NA HATA MAJUKUU ZETU WATAKUWA WAKISHABIKIA LIGI ZA ULAYA NA VIWANJA VITAENDELEA KUWA VITUPU. TATIZO KUBWA LA SOKA LA TANZANIA NI KUKOSA VIONGOZI WENYE UWEZO WA KUONGOZA KLABU ZA SOKO KIBIASHARA. VYANZO VYA MAPATO NI VINGI LAKINI MARA NYINGI KWA WAAFRIKA NI MASILAHI BINAFSI KWANZA!!!

    ReplyDelete
  2. hakuna haja ya kuwa na uongozi wala kamati kama hawajikiti kuendesha soka la kibiashara,kazi yao ni kumbembeleza manji kila siku wenyeewe mipango hawana?hapo hanuna uongozi

    ReplyDelete
  3. Kufikia hali hii ni kuonesha jinsi gani timu zetu hazina mipango endelevu. Sasa naamini kuwa mpira watu wanacheza kwa ajili ya kuonesha vipaji vyao na siyo kufanya sehemu ya kujiingizia kipato (kazi kama kazi nyingine) Ni aibu kwa Klabu kubwa kama Yanga kufikia hali hii. Napata wasiwasi kwa hizi klabu zetu ndogo japo sitozitaja zinajulikana. Ooooooooooooooooh mpira sasa basi kwa watanzania tufanye shughuli zingine.

    ReplyDelete
  4. Ujinga wa viongozi ( hasa wa Yanga) unatu-cost wabongo, sijui huwa wanagombea kwa nini wakati uwezo hawana. Na hao wafadhili ndo hamnazo kabisa. hapo atasubiri timu iwe choka mbaya then akarambwe miguu ndo ajitokeze wakati timu imeshapoteza mwelekeo. Ningekuwa rais ningewafunga jela wahuni hawa, kazi kututia machungu kila siku! Ni lini tz tutafurahia mpira wetu jamani?

    ReplyDelete
  5. kaka tatizo tanzania mtu akijua tu kuongea basi anpewa nafasi ya kuwa kiongozi na wenye kujua mpira wanabaki kujua washauri,mashabaki ilo ndiyo tatizo kubwa.pia hata kumtegemea mtu mmoja ambaye ni manji sasa umefika wakati timu kuendesha kama kampuni.kwa hiyo kaka shafii edo mayai mnamchango mkubwa katika ushauri.mfano mzuri mzee yusuph anayeimba taarabu ni mjumbe wa yanga wapi na wapi?mwisho nashauri uongozi wa yanga ujiuzuri kabla majungu yajaenda kwa wachezaji.

    ReplyDelete