Search This Blog

Wednesday, November 2, 2011

OKWI: SIJAPIGWA NA BOBAN


Siku chache baada ya kuripotiwa kupigwa baada ya mechi dhidi ya watani wa jadi, mshambuliaji Mganda wa Simba, Emmanuel Okwi, jana alikanusha taarifa za kupigwa na kiungo wa timu hiyo Haruna Moshi' Boban' kama ilivyoripotiwa juzi na jana huku uongozi wa klabu hiyo pia ukisema hapakuwa na tukio hilo lililodaiwa kutokea katika vyumba vya kuvalia wachezaji baada ya mechi waliyolala 1-0 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.

Hata hivyo, baadhi ya marafiki wa karibu wa Boban wameliambia gazeti hili kwamba kiungo huyo ambaye hakupatikana jana kwenye simu yake kuelezea tukio hilo, alimpiga Okwi.

Akizungumza jana jioni, Okwi alisema kwamba taarifa hizo si za kweli kama ilivyodaiwa kwani hata hakuonana na Boban baada ya kurejea katika vyumba vya kuvalia.

Okwi alisema kwamba ameshangazwa na uvumi huo na kusema kuwa yeye hakupata tatizo lolote baada ya kumalizika kwa mchezo huo ambao timu yake ilifungwa kwa goli moja ya Davies Mwape.

"Mimi mwenyewe nimeshangaa sana kusikia habari hizo, Boban hajanipiga na wala sikuonana nae wakati niliporudi kwenye vyumba vya kuvalia, hayo ni maneno ya watu ya kuzusha na mara nyingi hutokea timu inapofungwa, mimi sijapigwa nakuhakikishia," alisisitiza Okwi ambaye mara kadhaa amehusishwa na mipango ya kuhamia Yanga.

Mshambuliaji huyo aliongeza kwamba anasikitishwa na taarifa za aina hiyo kwa sababu hazijengi klabu na huwafanya wachezaji kutoaminiwa na wapenzi wao.

"Sio kwamba nimeambiwa nisiseme, ila hakuna kitu kama hicho, nilikuwa na wakati mgumu tangu jana (juzi) kwa kupigiwa simu na watu wengi na sikupokea simu zao," Okwi aliongeza.

Uongozi wa Simba jana ulisema kuwa taarifa za kiungo wao tegemeo Boban kumpiga Okwi katika vyumba vya kuvalia si za kweli na hakukuwa na tukio la aina hiyo juzi.

Afisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kuwa taarifa hizo zilizoripotiwa kwamba chanzo cha ugomvi kilikuwa ni madai ya hujuma na kutoaminiana ndani ya timu hazina ukweli wowote.

Aliongeza kuwa mara baada ya mechi, hali iliyotamalaki ilikuwa ni ya fadhaa na huzuni kwa wote wanaohusika na Simba, wakiwamo wachezaji na mashabiki na kusema kwamba habari hizo za ugomvi wa wachezaji ni uzushi unaoenezwa na watu wasioitakia mema klabu yao ambayo ilikuwa haijapoteza mechi hata moja tangu msimu huu wa ligi ulipoanza.

"Kuna mambo mawili yanayoweza kubainisha kuwa habari hizo hazikuwa za ukweli. Kwanza, kwamba vipo vyombo vilivyodai kuwa Okwi alipigwa hadi kuvimba uso. Ukweli ni kuwa Okwi yuko salama, buheri wa afya na hajavimba popote mwilini mwake, achilia mbali usoni, Pili, kuna magazeti yaliyoandika kuwa Okwi alipigwa vichwa vinne na Boban kabla hawajaamuliwa. Mengine yakaripoti kichwa kimoja. Kuna redio imeripoti kuwa vilikuwa vichwa vitatu. Tukio moja, taarifa tofauti lukuki," aliongeza afisa huyo.

Alisema kwamba hakuna mwandishi wa habari hata mmoja aliyeshuhudia tukio hilo na kulithibitisha pasi na shaka zaidi ya kusimuliwa na wale waeneza taarifa za uongo.

Aliwaomba wanachama na wapenzi wa timu hiyo kuendeleza ushirikiano na utulivu ili washinde katika mechi yao ya Jumatano dhidi ya Moro United.

2 comments:

  1. Hongera kwa kusema ukweli

    ReplyDelete
  2. Kama kweli Ema hakupingwa basi haya magazeti yetu hakika yamefikia mahali ambapo wadau lazima tupige kelele!Yawekana kweli mhariri achezeshwe ngoma asioijuwa?Kama mwandishi ana habari ya uzushi,halafu akampelekea mhariri wa habari ili aitoe gazeti hii ni sawa na yule mhariri kuicheza ngoma ya yule mwandishi bila kujuwa.Inatakiwa wahariri wachunguze mambo kabla ya kukurupuka na kuandika mambo ambayo mwisho wa siku yanazinunjia heshima taasisi zao,wao wenyewe na taaluma yao kwa jumla.

    ReplyDelete