Wakati beki Kelvin Yondani akiandika barua ya kutaka kurejea Simba, bado ameendelea kuwa kivutio kwa klabu ya Yanga, ambayo kupitia Kamati ya Usajili imepanga kuanza mikakati ya kumsajili katikati ya mwaka ujao.
Yondani bado ana mkataba na klabu ya Simba unaotarajia kumalizika katikati ya mwezi ujao, lakini hata hivyo ameshindwa kucheza muda mrefu kutokana na matatizo na uongozi wa klabu yake.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga Salim Rupia alisema, wameshindwa kumsajili Yondan katika kipindi hiki kwa sababu bado ana mkataba na klabu yake.
“Tulikuwa na nia hiyo ya kumsajili Yondan baada ya kupata taarifa kuwa hataki kuichezea timu ya Simba. Hata hivyo baada ya kufuatilia tuligundua ana mkataba na Simba na tukiamua kumsajili muda huu tutalazimika kulipa dau kubwa,” alisema Rupia.
Rupi alisema wanaheshimu mapendekezo ya kocha wao Mserbia Kostadin Papic, ambaye ndiye mwenye dhamana katika mambo yote ya usajili na wao watabaki kuwa washauri tu.
Aidha, Rupia alisema Papic amefanya mazungumzo na kiungo wa zamani wa timu hiyo, Athuman Idd ‘Chuji’ lengo likiwa ni kuangalia uwezekano wa kumrudisha kikosini kwa vile bado ana uwezo iwapo atafanya mazoezi vizuri.
“Kuna uwezekano mkubwa Chuji kurejea Yanga wakati wa duru la pili la Ligi Kuu. Kocha Papic ameshafanya mazungumzo na mchezaji huyo na kumpa masharti ili aweze kurejesha,” alisema Rupia.
Hata hivyo Rupia hakuwa tayari kusema aina ya masharti aliyopewa Chuji na Papic. “Waliyoongea na Chuji kama sehemu ya masharti yanabaki kuwa siri kati ya Chuji na kocha mwenyewe,” alisema zaidi.
No comments:
Post a Comment