Search This Blog

Friday, October 7, 2011

YANGA YASAJILI NEMBO, YATOA ONYO KWA WAFANYABIASHARA


Uongozi wa Yanga umewataka wafanyabiashara wote ambao wanamiliki bidhaa zenye nembo ya klabu hiyo kujisalimisha kabla ya Novemba.

Kauli hiyo ya Yanga imekuja kufuatia kuzagaa kwa vifaa vyenye nembo ya klabu hiyo ambavyo vinauzwa kiholela na wafanyabiashara na kuchapishwa au kutengenezwa bila idhini ya klabu hiyo.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Celestin Mwesigwa alisema kuwa ni bora wafanyabiashara hao wakajisalimisha wenyewe kwenye klabu ili kujua wafanye nini ili kuepuka usumbufu.

“Kuna wafanyabiashara ambao wana makontena ya bidhaa zenye nembo ya klabu yetu au wameagiza kutoka China na sehemu nyingine duniani, tunawaomba wavisalimishe klabuni ili kuepuka usumbufu wa kisheria,”alisema Mwesigwa.

Alisema wameshafuata taratibu za kisheria ikiwamo kwenda kusajili nembo ya klabu yao kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni za Biashara (Brela), zoezi ambalo limewagharimu zaidi ya shilingi milioni 10 ili iwe rahisi kwao kufanya wenyewe biashara ya vifaa vyenye nembo ya klabu hiyo.

Katibu huyo alisema kuwa mwanzoni kulikuwa na tatizo kwamba mahitaji ya vifaa hivyo vyenye nembo ya klabu yalikuwa makubwa kwa wanachama na wapenzi wa klabu hiyo na usambazi ulikuwa hakuna kwa klabu ndio maana wafanyabiashara wakajipa jukumu la kutengeneza na kusambaza bila makubaliano na wahusika, lakini klabu haikuwa na uwezo wa kudhibiti waagizaji wake.

Alieleza kuwa wameshafuata taratibu za kisheria na wanaye mshauri wa kisheria ambaye ni Kampuni ya AlexGlobes kwa ajili ya kuhakikisha analisimamia jambo hilo kwa umakini ingawa hakuwa tayari kueleza nani atasimamia zoezi la kukamata wafanyabiashara watakaokiuka ifikapo Novemba.

“Itakapofika Novemba tutajua nani atasimamia zoezi hilo bado kuna vitu tunakamilisha na huu ni wito kwa kila anayehusika hatutaki kuleta usumbufu kwa jamii kwa kuwa Yanga ni sehemu ya jamii pia,”alisema.

Aliongeza kuwa katika zoezi hilo la kuuza na kisambaza bidhaa zenye nembo yao, klabu hiyo inategemea kukusanya Shilingi 300 milioni hadi hadi 400 kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment