SIMBA ya Dar es Salaam leo ina nafasi kubwa ya kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakati itakapocheza na Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Azam Chamazi Mbagala.
Hadi sasa Simba inaongoza katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza mechi tisa na kushinda sita na kutoka sare tatu, ikifuatiwa na JKT Oljoro ya Arusha iliyocheza mechi 10 na kujikusanyia pointi 19 hadi sasa.
Pamoja na Simba kucheza na Ruvu Shooting iliyopo katika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14, isitarajie mteremko kwani wapinzani wao hao sio wa kubeza kwani nao wanaweza kusimama kidete na kuizuia Simba, iliyopania kumaliza duru la kwanza bila ya kufungwa hata mechi moja.
Simba katika mchezo wake wa mwisho iliibuka na ushindi wa bao 4-0 dhidi ya African Lyon na kuirejesha timu hiyo kileleni baada ya uongozi wa ligi hiyo kushikiliwa kwa siku kadhaa na JKT Oljoro yenye pointi 19 baada ya kucheza mechi 10 hadi sasa.
Timu hiyo yenye maskani yake Msimbazi jijini Dar es Salaam baada ya mchezo wa leo, itakuwa imebakiza mechi tatu kabla ya kukamilisha duru la kwanza la ligi hiyo.
Viingilio katika mechi hiyo namba 66 ni sh. 10,000 kwa VIP n ash. 5,000 kwa mzunguko.
Tiketi za mechi hiyo zitauzwa uwanjani Chamazi katika magari maalumu kwa ajili ya shughuli hiyo.
Wakati huo huo mahasimu wa Simba, Yanga watashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho kucheza na Toto Africa ya Mwanza katika mchezo mwingine wa ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment