USHINDI wa mabao 2-0 iliyoupata jana timu ya soka ya Azam dhidi JKT Ruvu, umewashusha nafasi moja mabingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Yanga kutoka nafasi ya tatu hadi ya nne.
Mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa ilipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo iliwachukua sekunde 36 Azam kujiandikia bao la kwanza lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake, Mrisho Ngasa, baada ya kumlamba chenga kipa wa JKT Ruvu, Shaaban Dihile.
Bao hilo liliwachanganya zaidi JTK ambao walianza kucheza kwa tahadhari sana, huku wachezaji wa timu hizo wakikosa mabao ya wazi baada ya kucheza fyongo.
Timu hizo zilikwenda mapumziko kwa Azam kuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa JKT kucheza bora liende, kwani hawakuonyesha jitihada yoyote ya kutaka kusawazisha.
Hata hivyo, mshambuliaji wa Azam, John Bocco ‘Adebayor’ aliifungia timu yake bao la pili katika dakika za nyongeza za mchezo huo.
Kwa ushindi huo, Azam iliyokuwa ikishika nafasi ya nne kwenye ligi hiyo imepanda hadi nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 18, wakati nafasi ya kwanza inashikililiwa na JKT Oljoro yenye pointi 19, Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 18 huku Yanga yenye pointi 15 ikishika nafasi ya nne na JKT Ruvu inashika nafasi ya tano kutokana na pointi 15 ilizonazo.
No comments:
Post a Comment