Siku mbili baada ya kupeleka msiba mtaa wa msimbazi, wachezaji wa maafisa wa benchi la ufundi la timu ya Yanga, kila mmoja amelamba kitita cha shilingi mil 1.5 kama zawadi ya kuwafunga Simba katika mechi ya Ligi Kuu ya bara iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga, hizo ni fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali wa timu hiyo akiwemo mfadhili wao, Yusuf Manji, ambao kwa ujumla, wametoa sh mil 54.
Alisema huo ni utamaduni wa wadau wa klabu hiyo kutambua juhudi kubwa ya wachezaji katika mechi ya juzi ambayo Yanga ilishinda bao 1-0, likifungwa na Davis Mwape katika dakika ya 72.
Nchunga aliyeingia madarakani Julai 18, 2010, alisema ushindi huo umekuwa ni faraja kwa kila mwana Yanga kwani mbali ya kulipa kisasi cha Agosti 17, pia kumewapa nguvu na ari ya kupigania ubingwa wao.
Aidha ushindi huo umeiwezesha Yanga kufikisha pointi 24 huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 27 baada ya kila moja kucheza mechi 12 tangu kuanza kwa ligi hiyo Agosti 20.
No comments:
Post a Comment