Search This Blog

Friday, September 30, 2011

TIMBE: TEGETE NA KADO WANAKAA BENCHI KWA SABABU YA VIWANGO VIBOVU




Mapigo ya moyo ya kocha wa Yanga, Sam Timbe yameanza kurudi katika hali yake ya kawaida na sura furaha ikionekana tena baada ya ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Coastal Union.

Baada ya kumalizika kwa mchezo wa juzi Timbe ambaye alikuwa hapendi kuzungumza na vyombo vya habari kutokana na timu yake kuanza vibaya aliwasifia nyota wake kwa kuonyesha kiwango cha juu huku akiweka wazi kwamba kiwango kibovu cha Jerryson Tegete na kipa Shabaan Kado ndicho kinachowanyima namba.


Uwezo wa mkubwa ulionyeshwa na Shamte Ally na Idrisa Rashid katika michezo miwili iliyopita umekuwa ni faraja kubwa kwa Mganda huyo.Tangu Timbe alipoanza kuwatumia katika mchezo dhidi ya African Lyon, Villa Squad na Coastal Union wachezaji hao wameonyesha uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga zilizowawezesha mabingwa hao kufunga mabao kumi tofauti na ilivyokuwa mwanzo.

Akizungumzia uwezo wa wachezaji hao, Timbe alisema anafarijika sana kuona vijana hao wapo katika kiwango kizuri hivi sasa jambo linalompa matumaini makubwa ya kuendelea kufanya vizuri zaidi wakishirikiana na wachezaji wengine wa kikosi chake."Katika mechi tatu ambazo vijana hao wamecheza kwa hakika wameonyesha uwezo mkubwa na wamekuwa wakishirikiana vizuri na wenzao katika kuhakikisha tunapata ushindi," alisema Timbe.

Pamoja na kusifia nyota hao Timbe alisema sababu ya kutompanga Tegete na kipa Kado ni kutokana na kutoonyesha viwango vya kuridhisha wakati wa mazoezi na kusisitiza anapanga kikosi kutokana na uwezo wa mchezaji.Timbe ambaye anaondoka leo kuelekea nchini Uganda kwa mapumziko mafupi alisema haoni sababu ya kuwapanga wachezaji waliokuwa kwenye kiwango cha chini katika kipindi hiki ambacho timu yao bado ina deni kubwa kwa mashabiki.
Awali Kado alikuwa mgonjwa wa kidole, lakini tayari amerejea katika hali yake kiafya na kujiunga na wenzake mazoezini, kwa mujibu wa kocha huyo mchezaji huyo bado hajarudi katika kiwango chake cha awali.


"Napanga timu kwa kuangalia uwezo wa mchezaji, siwezi kumpanga Tegete au Kado wakati kuna wachezaji wanaofanya vizuri zaidi yao, ninapokuwa nao mazoezini ndio napata muda wa kufahamu yupi aanze na yupi abaki hiyo ndiyo sababu yangu ya msingi,"alisema kocha huyo.

Timbe alisema timu yake hivi sasa ipo katika kiwango kizuri isipokuwa kuna baadhi ya mapungufu hususani kwenye safu ya ulinzi ambayo imekuwa ikifanya makosa mara kwa mara.

Alisema jukumu la kuhakikisha safu hiyo inakuwa imara zaidi lipo mikononi mwake na ameahidi kulifanyia kazi mapema iwezekanavyo ili kuhakiksha timu hiyo inaendelea kufanya vizuri katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu

No comments:

Post a Comment