Search This Blog

Friday, September 9, 2011

Liverpool wanatafuta ushindi wa kwanza kwenye uwanja wa Brittania .


Moja ya timu ambazo zimekuwa zikiipa Liverpool tabu ni Stoke City, tangu mwaka 2008 , Liverpool wametoka sare na Stoke mara mbili na wamefungwa na vijana hao wa Tony Pulis mara moja.
Wenyeji wa mchezo huu Stoke City wanatarajiwa kumpa mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Peter Crouch mechi yake ya kwanza tangu asajiliwe toka Tottenham siku ya mwisho ya usajili na kama bahati ikiwa kwake huenda akawadhuru mabosi wake wa zamani.
Crouch anakuja kwenye nafasi ya mmojawapo kati ya Kenwyne Jones na Jonathan Walters huku Wilson Palacios naye akitarajiwa kuonekana kwa mara yake ya kwanza kwenye timu yake mpya ya Stoke City, Palcios anaweza kucheza katikati na Rory Delap kama mrusha mipra huyu toka Ireland atakuwa amepona jeraha lake la misuli ya mguu.
Ujio wa Crouch , Cameron Jerome na Palcios kwa vyovyote utainufaisha Stoke kwa kuwa mitindo ya uchezaji wa watu hawa watau inaendana sana na falsafa ya soka linalochezwa kwenye klabu hii.

Mara nyingi vijana wa Tony Pulis huwa hawana vitu vingi kwenye mchezo wao, mfumo wao ni rahisi , mipira mirefu kwa mshambuliaji mmoja mwenye umbo kubwa na si vinginevyo huku viungo wa kati na mabeki wakicheza soka la shoka ambalo nguvu ndio hazina kubwa na ndio maana Liverpool wanateseka dhidi ya hawa jamaa hasa wanapolazimika kusafiri hadi Brittania ambako takwimu zinaonyesha kuwa kuna mashabiki wanaopiga kelele kuliko uwanja wowote kwenye ligi kuu ya England.
Kocha wa Stoke anaweza kuamua kumtumia beki Robert Huth kama beki wa pembeni ili kumpa nafasi Jonathan Woodgate kucheza katikati na Ryan Shawcross kama ilivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya Chelsea ulioisha kwa sare ya bila kufungana siku ya kwanza ya msimu.

Kwa upande wa Mfalme wa Anfield, Charlie Adam ataanza baada ya kurejea haraka toka kwenye jeraha alilopata akiwa na timu yake ya taifa Scotland wiki iliyopita, beki wa pembeni Martin Kelly hataonekana na kwenye nafasi yake atarejea John Flanagan japo Glen Johnson ameanza mazoezi baada ya kurudi toka kwenye jeraha lililomuweka nje.

Bado Liverpool itaendelea kumkosa Captain Fantastic Steven Gerard ambaye anaendelea kupoba taratibu kutoka kwenye maumivu ya sehemu ya juu ya mguu wake yanayomsumbua kwa muda mrefu . Liverpool wanaweza kumtumia Craig Bellamy pamoja na beki mpya Sebastian Coates huku ‘cha ulevi’ Andy Carroll akiwa benchi ambapo Dalglish anatarajiwa kuchezesha ‘maforward’ wale wale Kuyt na Suarez walioiua Bolton mara ya mwisho Liverpool ilipocheza kwenye ligi kuu ya England.
Dalglish anapaswa kuhakikisha kuwa anaipa ‘balance’ ya kutosha timu yake na hapa pengine ingeweza kuwa busara kumuacha Charlie Adam kwenye benchi na kumpa nafasi ya Lucas Leiva ambaye kwenye mchezo wa msimu uliopita alipata kadi nyekundu.


Mechi kama hizi za Stoke ndio haswa zinazomfaa kwa kuwa anapenda soka la vurugu ambalo Stoke ndio nyumbani kwake na Luis Suarez atakuwa chaguo bora kwa ushambuliaji kwa kuwa ujanja wake hakika utawapa tabu mabeki wa Stoke kina Huth,Shawcross na wengineo ambao uchezaji wao wa nguvu na ujanja wa Suarez vinaweza kusababisha hatari kwa Stoke, hasa ukizingatia tabia ya Suarez ya kupenda kuwaibia waamuzi kwa kujiangusha na kutafuta penati.

Auheni kwa Stoke inakuja kutokana na uwepo wa Jonathan Woodgate mtu ambaye ni kaka mkuu kwa mabeki wenzie na pia ana ‘dimensio’ tofauti kwenye mchezo wake ambapo yeye si kama wenzie ambao hutumia nguvu sana yeye hutumia zaidi akili na ni mtulivu kuliko wenzie.

Stoke hawajawahi kufungwa na Liverpool kwenye uwanja wa Brittania tangu wapande daraja, Mara ya kwanza Liverpool kusafiri kuelekea huko walitoka sare ya bila kufungana wakati huo wababe wa Anfield wakiwa chini ya Rafa Benitez , na kwenye mchezo wa marudiano msimu huo huo Robert Huth alifunga bao la kusawazisha na kwenye msimu uliofuata wakati Liverpool wakiwa chini ya Roy Hodgson waliondoka mikono mitupu baada ya kufungwa mabao mawili bila .
Hadi hivi tunavyozungumza Stoke haijapoteza mchezo wowote kati ya michezo 7 ya kiushindani waliyocheza na wamefungwa bao moja tu ugenini kwenye mchezo dhidi ya Norwich, mechi nyingine walizocheza ni dhidi ya Chelsea na West brom kwenye ligi na dhidi ya Hadjuk Split na Fc Thun kwenye michezo ya kufuzu Ligi ya Europa .
Msimu uliopita Stoke walishinda mchezo huu kwa matokeo ya 2-0 kupitia kwa mabao ya Ricardo Fuller na Kenywyne Jones.
Kocha wa Stoke Tony Pulis amelitumia vizuri dirisha la usajili baada ya kuwanunua wachezaji watano na cha kushangaza kwa kocha wa Stoke ni ukweli hakutumia fedha yoyote hadi siku ya mwisho ya dirisha la usajili ,Matthew Upson na Jonathan Woodgate walisajiliwa bure huku Peter Crouch , Cameron Jerome na Wilson Palacios wakijumuisha matumizi ya paundi milioni 20 zilizotumika dakika za mwisho kabisa za dirisha la usajili.
Kwa upande wake Kenny Dalglish ametumia takribani Paundi milioni 50 kwa wachezaji sita wa kikosi cha kwanza walionunuliwa msimu huu, Jordan Henderson, Stewart Downing, Charlie Adam, Alexander Doni, Jose Enrique na Craig Bellamywote wamejumuisha paundi milioni 50 kuja Anfield msimu huu.
Mara ya mwisho kwa Liverpool kupata ushindi wa aina yoyote ile kwenye uwanja wa Brittania ilikuwa mwezi Novemba mwaka 2000 ambapo Liverpool walishinda 8-0 kwenye kombe la ligi.Stoke wamewahi kuifunga Liverpool mara 27 huku Liverpool wao wakishinda mara 55 katika michezo 112 ambayo timu hizi zimekutana ambapo mara ya mwisho ilikuwa msimu uliopita huko Anfield ambapo Luis Suarez alifunga kwenye mchezo wake wa kwanza .

No comments:

Post a Comment