Search This Blog
Monday, September 12, 2011
Ramadhani Chombo,Said Morad na Victor Costa walicheza Vizuri...
Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kucheza mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Msimu huu jijini Dar es salaam baada ya kufungwa kwa muda kwa uwanja wa Taifa ili kupisha marekebisho madogo na timu waliyocheza nayo ni Azam Fc .
Ulikuwa mchezo ambao kabla timu zote zilikuwa zimekamiana kwa sababu ya rekodi tofauti ambazo timu zote mbili imekuwa nazo tangu ligi ianze. Azam wakiwa wamepata ushindi mara moja, wamefungwa na wametoa sare mara moja moja huku Simba wakiwa wameshinda michezo yote mitatu tangu ligi ianze.
Kwa vyovyote Azam walikuwa kwenye presha ya kupata matokeo mazuri kwa kuwa wachezaji wanajihisi kuwa na deni la kuwalipa wamiliki wa timu ambao kiukweli wamejitahidi kuipatia timu kila kitu,
Simba waliingia wakiwa na lengo la kuwaonyesha mashabiki wao wa hapa jijini DSM vitu ambavyo wamekuwa wakivifanya mikoani.
Kukosekana ubunifu kwenye kiungo cha Simba hasa pembeni…
Simba hawakucheza kama walivyostahili kucheza wakiwa kwenye hali ya ku-relax kuliko wenzao ambao walikuwa hawajaanza msimu vizuri. Tatizo kubwa kwa Simba lilikuwa jinsi ya kumtengenezea nafasi mshambuliaji Gervais Arnold Kago ambaye kwa mchezo dhidi ya Azam alikuwa anacheza kama mshambuliaji pekee huku Haruna Moshi akicheza nyuma yake. Haruna alikuwa anakaa mbali sana na kago kiasi kwamba mshambuliaji huyu toka Jamhuri ya Afrika ya kati alionekana kuhangaika mwenyewe pasipo msaada.
Mipira toka pembeni haikuwa mingi sana na mawinga wa Simba Amri Kiemba na Ulimboka Mwakingwe japo walionekana kucheza sana lakini hawakuwa na madhara kwa wapinzani wao na mara nyingi walikuwa wanachezea mpira miguuni kwao na si kutuma mipira hatari kwenye lango japo zipo nyakati ambazo walionyesha kuwa hatari .
Viungo wa Simba Jerry Santo na Patrick Mafisango hawakuwa na mchezo mbaya japo mengi yalitegemewa toka kwa Mafisango ambaye anaijua vyema Azam kwa kuwa alicheza huko msimu mzima na kuna wakati mawasiliano kati yake na wachezaji wa upande wa mbele wa Simba hayakuwa mazuri.
Muda wote mchezo ulikuwa wa piga nikupige huku kila timu ikionyesha umahiri wa kuchezea mpira na kupiga pasi za moja moja.
Azam na Simba ni timu ambazo soka lao linafanana kidogo kifalsafa, ni timu ambazo hupenda kucheza soka ambalo linatawaliwa na viungo ambao ni wachezea mpira huku wakitoa burudani kwa mashabiki.Viungo wa Simba Patrick Mafisango na Jerry Santo walikuwa na mchezo wa wastani.
Azam kutokucheza kwa kumzunguka Bocco
Kilichokuwa kinaigharimu Simba kwa washambuliaji wake ndicho kilichokuwa kinaiua Azam pia ambayo ilikuwa na Mshambuliaji mmoja akicheza katikati huku akisaidiwa na Tchetche Kipre kwenye upande wa kushoto na Mrisho Ngasa upande wa kulia huku nyuma yake wakiwa viungo wawili Ramadhan Chombo na Jabir Aziz. Bocco kama ilivyokuwa kwa Kago alionekana kutengwa akihangaika peke yake muda wote huku Ngasa na Kipre wakiwa kama wanacheza na majukwaa na hawakuwa wakimpa huduma inayostahili mshambuliaji wao.
Kwa mawazo ya kocha Stewart Hall kina Ngassa na Kipre wanapaswa kucheza kwa kumtazama Bocco yaani kwa maana nyingine Azam icheze kwa kumzunguka Boco lakini haikuwa hivyo kwani kina Kipre walikuwa wanaonekana zaidi kwenye mpira na sio Boko.
Lakini pia kama Bocco angeitumia vizuri nafasi aliyoipoteza kipindi cha kwanza tungeweza kuzungumza mengine sasa.
Nyoso na Costa ‘Nyumba’ Vs Aggrey na Morad ‘Mweda ‘
Mchezo huu ulikuwa kivutio kwa safu mbili za mabeki wa kati ambazo zilikuwa shupavu kwa asilimia mia moja. Simba wakiwa chini ya ‘baba mwenye nyumba’ Victor Costa na mdogo wake Juma Said Nyoso.
Kama kuna vitu vya msingi ambavyo Simba imevifanya ni kumrejesha beki huyu ambaye aliwahi kucheza miaka ya nyuma . Costa bado ni beki bora na adimu kwa Soka la Tanzania , ni mtulivu asiye na papara , anajua la kufanya muda wote na safu ya ulinzi ya Simba iko salama salmini chini yake . Kama kuna vitu vilivyoigharimu Simba msimu uliopita ilikuwa ni kutokuwa na safu ya ulinzi ambayo ‘imebalance’.
Wakati Simba inatwaa ubingwa bila kufungwa msimu wa kabla ya huu uliopita ambao Yanga walitwaa ubingwa walikuwa na safu bora ya ulinzi ambayo ilikuwa chini ya beki ambaye amefanana kwa vitu vingi sana na Victor Costa, Joseph Owino . Kumkosa Owino msimu uliopita kuliwalazimu Simba kuwatumia mabeki watatu ambao wamefanana kwa vitu vingi, Juma Nyoso , Kevin Yondani na Meshack Abel na hakuna mfano mzuri wa jinsi beki ya Simba ilivyokuwa hovyo zaidi ya mchezo kati ya Simba na Azam ambao Azam walishinda 3-2 kwenye uwanja huu huu wa Taifa.
Hayo hayakuonekana kwenye mchezo huu kwani uwepo wa Costa umemsaidia hata Nyoso ambaye anaonekana kuwa amejifunza vitu vingi toka kwa kaka yake. Ni jinsi ilivyokuwa wakati akiwepo Owino ambapo Nyoso alionekana kubadilishwa kwa vingi na Mganda huyu lakini alirudi kuwa Nyoso wa zamani alipoumia Owino .
Mabeki wa pembeni hawakucheza vibaya hasa kwa Amir Maftah ambaye alionekana ku-link vizuri kwa kiasi na Ulimboka , na kwa mchezo huu Amir ameonekana ku-improve kwenye tatizo lake la kupanda sana na kusahau majukumu yake na tatizo lake sugu la kukosa umakini na kupenda kucheza na majukwaa.
Tatizo lilikuwa upande wa kulia ambako anacheza Nassoro Said ‘Cholo’. Huyu jamaa ana shida moja kubwa nayo ni kushindwa kutimiza majukumu yake yote kama beki wa pembeni . Cholo anapenda sana kutumia nguvu kuliko maarifa na anajisahau sana hasa kwenye kupandisha timu . Kuna wakati mpira ulipokuwa unaelekea ukingoni nahodha wake Juma Kaseja alionyesha kukerwa na Cholo ambaye kaseja alihitaji kumuanzia mpira lakini Cholo alikuwa tayari keshapanda yuko mbele akisubiri Juma apige .
Kwa upande wa pili mchezaji ambaye wengi walimuona kama mchezaji bora wa mchezo huu , naye si mwingine ni beki Said Morad. Alikuwa anacheza vizuri kupita matarajio ya wengi ambao wanamkumbuka kwa jinsi alivyoachwa na Simba misimu kadhaa iliyopita na ni kama alisahaulika . Hakuna anayejua kwanini viongozi wa Azam walivuka misitu , nyika na milima kwenda kusajili beki toka Ghana wakati tayari Patnership ya Said Morad na Aggrey Morris inaonekana ku-click vizuri .
Morad alikuwa mwepesi sana katika maamuzi yake akiwapanga na kuwaelekeza mabeki wenzake juu ya wapi pa kucheza, alikuwepo kila mahali ambako mpira ulienda na hakuwa na kigugumizi, alikuwa anafanya clearance pale ilipohitajika, alikuwa akitoa mpira nje pale ilipomlazimu na megine mengi aliyafanya kwa usahihi pasipo kukosea.
Aggrey Morris naye alikuwa Yule Yule ambaye amezoeleka akicheza kwa utulivu wa hali ya juu huku akiusoma mchezo na kutumia maarifa mengi, Aggrey hana Tofauti kubwa na Costa na hawa ndio mabeki pekee walioko Tanzania kwa sasa ambao wanacheza kwa kutumia maarifa kuliko nguvu na kiukweli partnership ya Aggrey na Morad itawafikisha Azam mbali sasa kwa kuwa wameonekana kujenga uelewano wa haraka sana . Mabeki wa pembeni wa Azam nao walicheza vyema wakipandisha timu kwa umahiri mkubwa kwa na hali ilikuwa hivyo kwa sababu mchezo ulikuwa wazi sana huku kukiwa na nafasi nyingi za kupitisha mipira .
Chombo,Jabir na Morad ( wachezaji wa Zamani wa Simba )..
Viungo wa Azam Chombo na Jabir Azizi walicheza kwa umahiri mkubwa na kama isingekuwa performance super ya Morad basi mtu mwingine aliyestahili kuwa ‘man of the match’ machoni kwa wengi alikuwa Chombo.
Alikuwa akianzisha mashambulizi mengi ya Azam na hata pale ambapo wenzie walionekana kukwama kimawazo baada ya njia za kupitisha mipira kuwa zimebanwa walikuwa wakimtafuta na kumpa mipira yeye. Pengine Chombo, Morad na JABIR Azizi walicheza vizuri kwa kuwa walikuwa na kitu cha kuwadhidhirishia mabosi wao wa zamani Simba ambako waliwahi kucheza na kuachwa baada ya kuonekana viwango vyao vimeshuka.
Kiungo mwingine wa Azam Ibrahim Mwaipopo alionekana kucheza vizuri kwa kiasi chake ambako aliwakaba vyema viungo wa Simba na pia likuwa akiwaondoa mchezoni wachezaji wa mbele wa Simba akiua mashambulizi mengi.
Shija Mkina na ubinafsi wa Uhuru…
Wachezaji walioingia kwa upande wa Simba walionekana kushindwa kuendana na kasi ya mchezo. Shija Mkina aliingia kuchukua nafasi ya Amri Kiemba hakuonyesha makeke yoyote ambayo yalitarajiwa na kocha wake ambaye alimuingiza huku akimtazama kama mtu ambaye anakuja kubadili mchezo lakini haikuwa hivyo kwani alionekana kutokuwa mchezoni na alifanya kosa ambalo kocha wake alillitazama kama jambo ambalo linaweza kuidhuru timu yake pale alipomcheza rafu Mrisho Ngassa na kujikuta akionyeshwa kadi ya njano . Kocha Moses Basena aliamua kumtoa tena na kumuingiza Uhuru Suleiman ambaye hakuwa na faida kwa timu yake na alicheza akiwa hana uchangamfu ambao umezoeleka toka kwake.
Labda ilikuwa kwa sababu hajacheza muda mrefu na hana ‘match fitness’ lakini wakati mchezo unaelekea ukingoni aliikosesha timu yake bao la wazi pale alipokuwa na nafasi ya kufanya hivyo . Angeweza kutoa pasi kwa washambuliaji ambao walikuwa na nafasi ya kufunga kwa kuwa mpira ulikuwa kwenye nafasi ambayo yeye hakuwa anaweza kufunga na alichopaswa kufanya ni kutoa pasi kwa wachezaji wengine ambao walikuwa wanatazamana na lango . Kama utakumbuka bao alilofunga Haruna Moshi kwenye mchezo dhidi ya Yanga kwenye ngao ya hisani ilikuwa hivyo hivyo kama nafasi aliyopata Uhuru, Felix Sunzu alitoa pasi kwa Haruna ambaye alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga na ndio alichotakiwa kufanya Uhuru lakini ni kama kichwani kwake alikuwa anataka kumuonyesha kocha kuwa anao uwezo wa kufunga na badala yake akajiharibia kabisa kwani lazima kocha atakuwa amemuona kama mchezaji mbinafsi asiye na msaada kwenye timu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Umechambua vizur sana, yaani nimesoma na kuuelewa mchezo kama vile nami nilikuwa uwanjani vile. Hongera sana kaka
ReplyDelete