Wakati nyota wa soka la Cameroon Samuel Eto’o Fils akianza hatua nyingine kwenye safari yake ndefu ya maisha yake ya soka hebu tutazame nyuma kwenye matukio mbalimbali ambayo yameliweka soka lake kwenye ramani.
Etoo hivi karibuni alikamilisha usajili wake toka Inter Milan kwenda kwenye klabu ya Urusi Anzhi Makhachkala .Thamani ya Ada ya uhamisho haijatajwa rasmi ila inaaminika kuwa kwenye maeneo ya Euro Milioni 25 au 28 , huku mshambuliaji huyo akisaini mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo ya Urusi.
Mshambuliaji huyu alisajiliwa Inter Milan mwaka 2009 kama sehemu ya uhamisho wa Zlatan Ibrahimovic toka Inter kwenda Barcelona alikotoka Etoo na huko alifanya vizuri ambako alitwaa ubingwa wa Ulaya , Serie A na kombe la Italia. Alikuwa mfungaji bora kwa Inter msimu uliopita ambapo alifunga jumla ya mabao 37 kwenye michuano yote na aliibeba klabu hiyo kutwaa Kombe la italia.
Maisha ya soka la Etoo yamedumu kwa karibu miaka 15 ambapo amefanikiwa kutwaa mataji mbalimbali akiwa na vilabu na timu yake ya taifa pamoja na tuzo mbalimbali binafsi katika muda wote huo.
Wakati Eto’o akianza kuzoea maisha mapya huko Urusi tunatazama nyakati tano bora katika maisha ya soka ya Eto’o .
UBINGWA WA KOMBE LA MATAIFA IN 2000
Etoo aliingia kwenye soka la kimataifa akiwa na timu yake ya taifa ya Cameroon mwaka 2000 ambapo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ya taifa ya Cameroon The Indomitable Lions .
Cameroon ilizitoa Algeria na Tunisia kuelekea kwenye fainali ambako ilicheza na mahasimu wao wa miaka yote Nigeria . Cameroon iliwafunga Nigeria kwa penati baada ya sare ya 2-2 kwenye dakika 90 na muda wa nyongeza . Etoo hakupiga penati lakini alifunga kwenye hatua za robo fainali , nusu fainali na kwenye fainali pia ambapo alimaliza michuano hiyo akiwa na jumla ya mabao manne akiwa nyuma ya mfungaji Bora Shaun Bartlett kwa bao moja.
Etoo alikuwa na umri wa miaka 18 wakati huo na juhudi zake zilimpa tuzo ya mchezaji bora kijana na Cameroon yote ilitambua kuwa shujaa mpya amepatikana.
MATAJI MATATU AKIWA NA BARCELONA 2008/09.
Msimu wa mwaka 2008/09 ulikuwa wa aina yake kwa Etoo. Akiwa na timu yake ya Barcelona Eto’o aliisaidia kutwaa mataji matatu La Liga , Copa Del Rey na lile la ligi ya mabingwa .
Mchango wa Etoo ulikuwa mkubwa pengine kuliko mtu yoyote na mnamo Oktoba 25, Eto’o alifunga hat-trick ya haraka kwenye historia ya klabu ya Barcelona baada ya kufunga mabao matatu ndani ya dakika 23 katika mchezo dhidi ya Almeria . Etoo pia alifunga mabao manne kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo dhidi Real Valladolid siku chache zilizofuata.
Etoo alifunga mabao 30 kwenye La Liga na alitoa pasi nne za magoli kwa wachezaji wengine , mabao yake hayo yaliisaidia Barca kutwaa ubingwa wa La Liga huku mabao yake manne kwenye Ligi ya Mabingwa ya ulaya yakiisaidia klabu yake kutwaa taji hilo .
MATAJI 3 NA INTER MILAN
Mwaka uliofuata baada ya kuipa taji Barca, Etoo alihamia Inter Milan na hakupoteza muda kwani msimu huo huo aliipa Inter mataji matatu ya Ligi ya mabingwa , Coppa Italia na Serie A.
Kutwaa mataji matatu mara mbili mfululizo ni rekodi ya kipekee kwa Etoo na juhudi zake kwenye msimu wa mwaka 2009/10ulikuwa ushahidi tosha wa kumpa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka 2010.
Eto’o alifunga mabao 12 na kutengeneza mengine matano huku bao lake lingine akifunga kwenye Coppa Italia na kwenye ligi ya mabingwa alifunga kwenye ligi ya mabingwa katika msimu ambao Inter waliweka na kuvunja rekodi nyingi.
UBINGWA WA KOMBE LA DUNIA LA KLABU
Mabingwa wa Ulaya na Italia Inter pia walitwaa ubingwa wa Dunia kwa vilabu baada ya kuwafunga mabingwa wa Afrika Tp Mazembe 3-0 kwenye fainali mwezi desemba mwaka 2010.
Inter walitwaa ubingwa huu kwa mabao ya kipindi cha kwanza yaliyofungwa na Goran Pandev, Samuel Etoo na Jonathan Biabiany.
Kwa mara nyingine Eto’o alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake akitengeneza bao la kwanza kabla ya kufunga la pili mwenyewe.
TUZO YA 4 MCHEZAJI BORA WA AFRIKA
Etoo alitwaa taji bora kwenye orodha ya mataji ya CAF kwa wachezaji binafsi baada ya kutunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka 2010, Hii ilikuwa mara ya nne kwa Etoo kutwaa tuzo hii baada ya kuitwaa kwenye miaka ya 2003,2004 na 2005.
Katika wachezaji waliokuwa kwenye orodha ya wachezaji wanaowania tuzo hii Etoo alikuwa anastahili kuliko wenzie Didier Drogba na Asamoh Gyan. Etoo aliifungia timu yake ya Taifa mabao mawili kwenye kombe la dunia lakini ilikuwa mchango wake kwenye klabu yake uliompa tuzo hii.
Taji la Serie A , Ligi ya mabingwa , Coppa Italia ,na lile la Super Coppa Italia yaliongeza idadi yake ya mataji pamoja na lile la kombe la dunia kwa vilabu.
No comments:
Post a Comment