Search This Blog

Tuesday, September 6, 2011

MARSH AWAMWAGIA UPUPU MAKOCHA WA KIGENI




Kocha msaidizi wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars Syllvester Marsh amesema moja ya sababu inayochangia timu ya taifa kufanya vibaya ni ubishi wa makocha wa kigeni.

Akihojiwa na Sports xtra ya Clouds fm, Marsh alisema kuwa kitendo makocha wa kigeni kudharau ushauri wa wazawa kinatokana na wao kuamini wazawa hawajui chochote kuhusu masuala ya soka.

Alisema kuwa alibaini kuwepo kwa fikra hizo zilizotawala miongoni mwa makocha wazungu wakati alipokuwa akifanya kazi na aliyewahi kuwa kocha wa timu za taifa za vijana, Marcus Tino baada ya kumwambia kwamba anashangaa kuona Tanzania ina makocha wazuri.

"Niseme ukweli kwamba, kuna tabia ya makocha wakigeni wanaokuja hapa kudharau ushauri wa wazawa, hii inatokana na wao kuamini pengine sisi hatujui chochote kuhusu soka.

"Ukweli makocha wakigeni wanaamini kwamba mpaka wao wanachukuliwa maana yake labda hapa hakuna kocha mzuri, kumbe si hivyo, Congo juzi tu wamemtimua kocha wao kwa sababu hizo hizo kwamba hashauriki.

"Kwa mfano wakati ule nafanya kazi na Tinoco aliwahi kuniambia kwamba kumbe Tanzania kuna makocha wazuri akionekana kushangaa, lakini sio suala la kulaumu kwasababu pengine mazingira ndiyo wanayakuta yanawafanya wafikiri hivyo,"alisema Marsh.

Marsh pia alizungumzia tabia ya makocha wa kigeni kutodumu muda mrefu kwa kusema kuwa, hilo linasababishwa hasa pale wanapokutana na mazingira tofauti na yale waliyoyategemea kuyakuta wakati wanatoka kwao.

"Mimi ni mzawa ninaweza kuvulimia kwasababu naijua vizuri hali halisi ya nchi yangu, lakini wao inakuwa vigumu kwasababu unakuta amezoea kupata kila kitu huko kwao sasa anapohitaji kitu fulani hasipotimiziwa hawezi kukaa,"alisema

Marsh amekuwa kocha msaidizi kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa takribani miaka mitano tangu enzi za kocha Mbrazil Marcio Maximo, pia amewahi kuifundisha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys akiwa kocha msaidizi wa Abdalah Kibadeni pamoja na kuzifundisha timu kadhaa za ligi kuu ikiwemo Kagera Sugar.



No comments:

Post a Comment