Search This Blog

Thursday, September 29, 2011

CAMEROON NA NIGERIA ZAALIKWA CECAFA CHALLENGE CUP


Timu za soka za Cameroon na Nigeria zinatarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ya mwaka huu.


Miamba hiyo itashiriki kama timu mwalikwa katika michuano hiyo inayotarajiwa kufanyika Tanzania Bara kuanzia Novemba 24 mpaka Desemba 9, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye kwenye vyombo vya habari vya Rwanda na Kenya, tayari wameshafikia muafaka juu ya ushiriki wa timu hizo na kwamba Baraza lake limetafuta timu nyingine kubwa ili kuifanya michuano iwe na ushindani zaidi.

Mali, Zambia na Malawi zinakamilisha idadi ya timu za kigeni zitakazoshiriki michuano hiyo. Hata hivyo, habari kutoka Nairobi zinasema tarehe hiyo ya kuanza kwa michuano itawaweka kwenye wakati mgumu kwani Ligi Kuu ya Kenya inatarajiwa kumalizika Novemba 26.

Lakini Musonye alisema: “Ratiba imebana na hakuna la kufanya zaidi ya kuipeleka mbele mechi ya kwanza ya Kenya, lakini nahofu inaweza kuwa Novemba 27.

“Hakuna tarehe nyingine ya kupanga kuanza kwa michuano hiyo, fainali zitafanyika Desemba 9, siku ya Uhuru wa Tanzania,” alisema.

Tanzania inakuwa mwenyeji wa michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuiandaa mwaka jana, hiyo ni mara ya kwanza kutokea katika historia ya michuano hiyo.

Katika michuano ya mwaka jana, timu ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ilitwaa taji lake la tatu la Chalenji baada ya kuifunga Ivory Coast bao 1-0 katika fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Cameroon ilionesha nia ya kushiriki mwaka jana, lakini haikuthibitisha mpaka dakika za mwisho ratiba ilipoapangwa. Musonye alisema wameamua kufanya michuano hiyo Tanzania kwa mara ya pili mfululizo baada ya mwaka jana kufanyika kwa mafanikio makubwa.

Nchi nyingine zinazotarajiwa kushiriki michuano hiyo ni Rwanda, Sudan, Djibouti, Eritrea, Kenya, Ethiopia, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan, Zanzibar, Uganda na wenyeji Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment